23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yakubali kufutwa

kambayaNA AGATHA CHARLES
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimekubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wa kukifuta katika orodha ya vyama vya siasa kwa sababu hakiko tayari kuvunja vikundi vyake vya ulinzi vinavyojulikana kwa majina ya Blue Guard na White Guard.
Kimesema kwa sasa licha ya kuwepo zuio la kuvitumia vikundi hivyo kutoka kwa Jaji Mutungi na Mkuu wa Jeshi la wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kitaendelea kuvitumia vikundi hivyo katika ziara zake za kichama zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni katika mikoa ya Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa.
Uamuzi huo wa CUF umetolewa jana na Mkurugenzi wa Uenezi, Abdual Kambaya katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyikia makao makuu ya chama hicho.
Kambaya ametangaza msimamo huo ikiwa ni siku chache baada ya Jaji Mutungi kupiga marufuku vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama, kwa kile alichoeleza kuwa kwa sababu uwepo wake ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotoa jukumu la ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa Jeshi la Polisi.
Jaji Mutungi alitoa agizo la kufutwa kwa vikundi hivyo katika mkutano wake na vyama vya siasa pamoja na Jeshi la Polisi, kwa kuvitaka vyama vya siasa ambavyo Katiba zake zinatambua uwepo wa vyama hivyo, virekebishe kwa kuviondoa kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, Kambaya alisema agizo hilo la Jaji Mutungi halitekelezeki kwa sababu vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vipo kwa mujibu wa sheria na Katiba inavitambua na hata ofisi ya msajili ya vyama ina taarifa za uwepo wake.
Kambaya alisema iwapo Ofisi ya Msajili imedhamiria kusimamia agizo lake hilo inapaswa kukipatia CUF Sh bilioni moja ambacho ndicho kiasi kinachohitajika kwa ajili ya kuitisha mkutano mkuu utakaoamua kufutwa kwa vikosi hivyo.
“CUF tunaona kauli za msajili wa vyama vya siasa na IGP Ernest Mangu ni za kuchekesha kwa sababu wanachokitaka hakiwezekani, vikundi hivi vipo kisheria na Katiba ya nchi inavitambua.
“Kama kweli Jaji Mutungi anamaanisha anachokisema, basi utaratibu wetu wa kufanya hivyo anaujua kwani Katiba ya chama inarekebishwa na wanachama kupitia mkutano mkuu wa taifa, hivyo atupatie bilioni moja ambayo ni bajeti yetu ya kuitisha mkutano huo,” alisema Kambaya.
Akizungumzia majukumu ya vikundi hivyo alisema havipo kwa ajili ya kupambana na polisi, bali kulisaidia kufanikisha kazi ya usalama wa raia kwa sababu limeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika shughuli za kisiasa.
“Iwapo IGP anataka kushughulikia vikosi vya ulinzi na usalama aanze na vile vya kigaidi na uhalifu wakati wa uchaguzi vinavyomilikiwa na CCM kama vile vya Janjaweed na GreenGuard na Chinjachinja, ambavyo ni maarufu kwa kufanya uhalifu,” alisema Kambaya.
Alisema chama chake kitavitumia vikundi vyake vya ulinzi na usalama katika ziara kinazokusudia kuzifanya hivi karibuni kwenye mikoa ya Kanda ya Kusini zitakazoongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Profesa Ibrahim Lipumba na mikoa mingine kuanzia Dodoma itaongozwa na Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Bunge, Shaweji Mketo.
Aidha, Kambaya alisema Tume ya Uchaguzi imehodhi mchakato wa kutoa elimu kuhusu kura ya maoni ambao ulipaswa kutekelezwa na asasi za kiraia (NGOs).
Msimamo huu wa CUF unafanana kwa kiwango kikubwa na ule uliotolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe aliyesema kuwa litakuwa jambo la kiuwendawazimu kuvifuta vikundi hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles