27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ulinzi Dar si wa kawaida

kovaVeronica Romwald na Tunu Nassoro, Dar es Salaam
HALI ya ulinzi katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam sasa si ya kawaida, kutokana na askari wa Jeshi la Polisi kuonekana kutanda katika maeneo mbalimbali.
MTANZANIA Jumamosi limebaini jana kuwapo kwa idadi kubwa ya askari wa Jeshi la Polisi ambao wamesambaa katika maeneo mbalimbali ya jiji, zaidi wakiwa na silaha kama bunduki na virungu.
Baadhi ya maeneo ambayo gazeti hili limeshuhudia ulinzi wake kuwa si wa kawaida ni pamoja na Mlimani City, Posta na Namanga.
Pia lilishuhudia magari ya Jeshi hilo (Defender) yakizunguka na kushusha askari wake katika maeneo hayo ambapo wengine walianza kusambaa katika mitaa mbalimbali, hususan eneo la Posta Mpya.
Si hivyo tu, katika siku za hivi karibuni eneo la Mlimani City ulinzi umeonekana kuimarishwa zaidi kuliko ilivyo kawaida.
Kundi la askari limekuwa likionekana karibu na jengo hilo la Mlimani, hasa karibu na zilipo ofisi za benki ya Twiga Bancorp.
Askari hao pamoja na wengine ambao wamekuwa wakionekana nje ya lango la kuingilia eneo hilo, baadhi yao wamevalia vifaa ya kuzuia risasi (bullet proof) na wakati mwingine wakiwa na magari yao.
Katika eneo la Namanga, askari walionekana wakiwa wamesimama katikati ya makutano ya barabara na wengine wakiwa wamesimama karibu na miti iliyopo pembezoni mwa barabara hiyo, wakiwa wamebeba silaha zao.
Gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, kuhusiana na hali hiyo ambapo alisema wapo katika operesheni maalumu ya kupambana na uhalifu ndani ya jiji hilo.
Alisema Jeshi hilo limeamua kuweka askari wake kwa wingi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kwa nia ya kuimarisha usalama.
“Kwanza nashukuru ndugu mwandishi kwa kuona jambo hili, tumelazimika kufanya hivyo kuanzia leo, hii ni kutokana na mahitaji yaliyopo, tupo makini na imara, tunapambana na uhalifu wa aina zote,” alisema.
Alisema operesheni hiyo imelenga kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo kwa nia ya kupambana na matukio au jaribio lolote la uvunjifu wa amani ndani ya jiji hilo.
“Hii inaitwa ‘High Police Visibility’, tunajua kwamba uwepo wa mwonekano wa askari kwa wingi unasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea uhalifu.
“Kazi kubwa tunayofanya ni kudhibiti aina yoyote ya tukio au jaribio lolote la uvunjifu wa amani na tutawakamata wahalifu wa aina zote mpaka wapiga debe,” alisema.
Hivi karibuni kundi la kigaidi la Al Shabaab limekuwa likitoa vitisho kwa nchi zilizoko ukanda wa Afrika Mashariki.
Kundi hilo tayari limefanya mashambulizi nchini Kenya, ambapo hivi karibuni lilivamia katika Chuo Kikuu cha Garissa, nchini humo na kuua zaidi ya watu 100.
Hali hiyo imezifanya nchi hizo kuanza kujihami kwa kuimarisha ulinzi wake katika baadhi ya maeneo yake, hasusan yale yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Tanzania ni moja kati ya nchi zilizoko katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles