26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Spika Makinda apandisha joto la urais CCM

anne-makindaEVANCE MAGEGE NA AGATHA CHARLES

Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema mgombea uraisi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anatarajiwa kuteuliwa hivi karibuni.

Amesema katika kipindi cha siku chache zijazo vikao vya uteuzi vya CCM vitaanza vikao vyake na vitahitimishwa na mkutano mkuu ambao utateua mgombea wa chama hicho.

Spika Makinda aliyasema hayo jana, wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa siku moja wa Maspika wa Mabuge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliofanyikia Hotel Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.
Hii ni kauli ya kwanza kutolewa na Spika Makinda, ambaye ni mjumbe wa vikao vyote vya maamuzi vya CCM.
Mbali na kuzungumzia uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM, Spika Makinda alisema joto la uchaguzi mkuu sasa limezidi kupanda kwa wabunge ambao wako majimboni kwa wapiga kura wanakotafuta uugwaji mkono.
“Kwa bahati mbaya Katiba yetu hairuhusu mgombea binafsi, lakini ni suala la kawaida katika chaguzi mbalimbali kuvutia mambo mengi na wakati mwingine huibuka vitu vingi vya ajabu kipindi cha mchakato wa kampeni na hata baada ya kutangazwa matokeo, lakini tuna uhakika kwamba tutavuka daraja tukiwa salama.
“Tuombeeni ili tufanye uchaguzi kwa amani kama ilivyokuwa Kenya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013,” alisema Spika Makinda.
Kauli ya Spika Makinda imekuja huku kukiwa na hali ya sintofahamu kati ya makada wa CCM na wapambe wao wanaowania nafasi za kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Mbali ya hiyo, ipo pia sintofahamu kwa makada sita ambao wameadhibiwa na chama kwa kuanza kampeni za kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais mapema ambao umri wa kifungo chao hadi sasa umebaki kuwa kitendawili, jambo linalotia shaka kama wataingia kwenye mchujo au watatupwa nje.
Makada hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia , January Makamba.
Awali katika hotuba yake hiyo, Spika Makinda alizungumzia mchakato wa Katiba Mpya kwa kueleza kuwa ulifanyika vizuri kuanzia kwenye ukusanyaji wa maoni ya kupendekeza Katiba.
Alisema ingawa wajumbe 100 walijiondoa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, lakini akidi ilitimia, hivyo kulifanya bunge hilo kuendelea hadi mwisho.
Alisema baada ya Bunge Maalumu kumaliza kazi yake ya kupendekeza Katiba Mpya, ilitarajiwa Aprili 30 mwaka huu ipigwe kura ya maoni, lakini kutokana na uandikishaji wa daftari la wapiga kura kwa mfumo mpya wa BVR na changamoto za uwezeshaji, kazi hiyo imeshindwa kukamilika katika muda uliopangwa.
Wakati huo huo, kuna hali ya wasiwasi wa iwapo muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utasimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Wasiwasi huo umejitokeza waziwazi jana, wakati Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa NCCR – Mageuzi, Faustine Sungura, alipokuwa akimkabidhi fomu ya kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho, George Kahangwa, ambaye aliwakilishwa na Mawazo Athanas.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fomu hiyo, Sungura alisema taifa linapaswa kuongozwa na vijana na kuwataka wapiga kura kuacha kuwachagua wagombea wenye mvuto wa sura au majina, bali wachague vijana kwa sababu chama chake hakitarajii kuwa na rais mwenye umri zaidi ya miaka 64.
Kauli hiyo ya Sungura iliungwa mkono na Katibu Mkuu Kitengo cha Vijana cha NCCR – Mageuzi aliyepokea fomu ya kuwania urais kwa niaba ya Kahangwa, ambaye alieleza kuwa vijana wa chama hicho wamechanga Sh milioni moja ili kumwezesha kijana mwenzao kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea kwa sababu hawako tayari kuongozwa na wazee.
“Sisi vijana hatuko tayari kuona tunakuwa na kiongozi aliyezaliwa kabla ya uhuru, tumechanga kiasi cha Sh milioni moja ili kuchukua fomu ya urais, hili limetanguliwa na ushawishi ambapo Kahangwa amekubali kusimama kwa niaba ya vijana. Nasisitiza tu watu wasichoke tuendelee kushirikiana kama tulivyofanya ili mgombea wetu afike mbali,” alisema Athanas.
Kauli hiyo ya Athanas mbali na kuthibitisha msimamo wa vijana wa NCCR kuhusu matakwa ya mtu wanayetaka kuwa rais wao, ilibeba pia ujumbe uliotiliwa mkazo na Sungura, ambaye alieleza kuwa amefungua rasmi pazia la wagombea kuchukua fomu, lakini pia ni lazima chama hicho kifanye vizuri katika kuwania nafasi za juu za uongozi ndani ya UKAWA.
“Kati ya rais wa Bara, Zanzibar au Waziri Mkuu lazima atoke kwetu, hivyo tunatarajia kuwa na nafasi kubwa. Kuna wanaopotosha lakini Ukawa ni fursa ambayo lazima iwanufaishe NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema na NLD, lazima tugawane.
“Ukiangalia mbali na viongozi kama Patrice Lumumba ambaye alikuwa kijana, lakini hata mwalimu Nyerere aliachia madaraka akiwa na miaka 64, hivyo hatutarajii kuwa na rais aliyezidi hapo, hata wanaojitokeza wakiwa na umri mkubwa wajitafakari kwanza,” alisema Sungura.
Alisema kumbukumbu zinaonesha kuwa mbali na kuheshimu busara na hekima za wazee, viongozi wengi walioshika madaraka katika umri mdogo walifanikiwa zaidi katika uongozi wao.
Sungura alieleza zaidi kuwa huu ni wakati wa vijana kuchukua madaraka kupitia Ukawa, inayoundwa na vyama vinne vya upinzani ambavyo ni NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema na NLD.
Ingawa Sungura na Athanas hawakutaja majina ya viongozi wenye umri mkubwa waliokwishaonyesha nia au wanaotajwa kuwa wanaweza kuwa wagombea urais kupitia Ukawa, majina yanayotajwa kuwemo kwenye orodha hiyo ni pamoja la Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, mwenye umri wa miaka 68, Prof. Ibrahim Lipimba (63) na Maalim Seif Sharif (72).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles