24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Jinsi ‘magaidi’ kumi walivyonaswa Moro

Na Waandishi Wetu

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kukamata watu tisa waliokuwa na milipuko, sare za jeshi na silaha za jadi msikitini mkoani Morogoro, imebainika kuwa walikamatwa saa tatu kabla ya kutoka kwenye eneo hilo na kwenda kutekeleza azma yao.
Ingawa haijajulikana kuwa watu hao walikuwa waende wapi, habari hizo zimebainisha kwamba walipanga kuondoka saa 11 alfajiri, lakini polisi wakawakamata saa nane usiku.
Mwandishi wa gazeti hili alivyofika kwenye Kijiji cha Chikago, Kata ya Kidatu wilayani Kilombero, alibaini kuwa watu hao walifika kwenye msikiti huo – Masjid Salah Al–Fajih – saa nne usiku na kuingia ndani huku wenyeji wakiwa hawapo.
Ilibainika kuwa katika msikiti huo wa Sunni kuna watoto wanne wenye umri kati ya miaka 12 na 16 huwa wanalala, lakini wakati wahalifu hao wanafika hawakuwapo.
Watoto hao ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema wakati watu hao wanaingia msikiti hapo, wao walikuwa wameenda kutafuta chakula cha usiku.
“Tulivyorudi tulikuta kuna watu wamelala kwenye mikeka, tukawasalimia ‘assalam alaykum’ wakatuitikia. Hatukuendelea kuwasemesha kwa sababu tulijua watakuwa wageni wa Imamu. Wa msikiti.
Kwa mbele kuna mlango huwa tunaufunga wakati tukitaka kulala, lakini siku hiyo tulipotaka kuufunga ili tulale walitukataza wakasema kuwa wataondoka alfajiri kwa hiyo tusiufunge,” alisema.
Watoto hao walisema kati ya mazungumzo machache waliyoweza kufanya na watu hao, walibaini kuwa baadhi wanatoka Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Singida.
Walisema kabla ya kufika asubuhi, majira ya saa nane usiku walifika polisi kwenye msikiti huo na kuwakamata vijana hao.

ALIYEWAPELEKA MSIKITINI
Alphonce Maurus ambaye ni dereva wa bajaji aliyewapeleka watu hao kwenye msikiti huo, alisema juzi majira ya saa tatu usiku akiwa Kidato kwenye eneo lake la kusubiri abiria, watu 11 walifika hapo wakihitaji usafiri.
Alisema kati ya watu hao, yeye aliwabeba watano akiwamo Hamad Makwendo ambaye aliuawa alipokuwa akijaribu kupambana na askari.
Maurus alisema baada ya kuwapakia watu hao pamoja na Makwendo aliyekuwa mwenyeji wao, wengine sita walipanda kwenye bajaji nyingine na kuwafuata hadi kwenye msikiti wa Sunni ulio kwenye kijiji hicho.
Alisema wakati wote wa safari yao, mwenyeji wao ndiye alikuwa akizungumza kuelekeza njia huku wengine wakiwa kimya.
Maurus alisema watu hao walikuwa wamebeba mabegi, lakini hakuweza kujua ndani kulikuwa na nini.
“Tulivyofika pale msikitini tuliukuta uko wazi, wao wakaingia ndani,” alisema.
Alisema usiku Makwendo alitoka akiwa na bajaji akienda kuchukua watu wengine na walipofika njiani ndipo wakakutana na askari.
“(Makwendo) alishuka kwenye bajaji akawa anakimbia na askari wakamkimbiza, alivyofika sehemu akadondoka, alivyodondoka kuna askari alikuwa anamkimbiza alivyojaribu kumkamata, akachomoa sime akamkata shingoni na kwenye mkono.
“Yule askari akapiga kele wenzake waliokuwa nyuma wakampiga risasi yule jamaa kisha wakampakia kwenye gari lao wakataka kuondoka naye.
“Kutokana na zile kelele wananchi walijaa wakawaambia askari wasipomshusha yule mtu watachoma gari moto, na kweli wakafanikiwa kumshusha wakampiga na kumchoma moto,” alisema.
Maurus alisema baadaye askari walimshika na kumtaka awapeleke kwenye eneo walipo watu wengine.

Mwenyekiti wa kitongoji

Mweyekiti wa Kitongoji cha Ikera, Kata ya Kidatu, Mohamed Libaha, alisema siku ya tukio hilo, majira ya saa 8 usiku, askari walifika nyumbani kwake na kumuhoji kama ana taarifa za wageni walio kwenye kitongoji chao.
Alisema baada ya kuwaambia kuwa hawana ugeni wowote, polisi waliwakamata watu hao na kiongozi wa msikiti huo, Ustaadh Maulid Sultani.
Katibu wa msikiti huo, Mohamed Manze, alisema wao kama viongozi na waumini wa msikiti huo hawakuwa na taarifa zozote za ujio wa watuhumiwa hao, na kwamba katika msikiti huo wapo vijana wanne ambao huwa wanalala na kujisomea hapo.
Alisema siku ya tukio watuhumiwa hao walifika msikitini hapo majira ya saa nne usiku ambapo tayari ibada ya mwisho ilikwishafanyika na waumini kutawanyika.
Manze alisema walitumia mwanya huo kuingia na kujihifadhi bila taarifa zozote kwa uongozi wa msikiti huo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu za msikiti huo.
Alisema wao kama waumini wa msikiti huo hawakupendezwa na suala hilo na kwamba limewachafua na kuwaharibia sifa waumini na msikiti wao.

Chanzo cha askari kujua siri ya watu hao

Manze alisema hivi karibuni kwenye eneo hilo mtu mmoja alikamatwa akihusishwa na matukio ya ugaidi yaliyotokea mkoani Arusha na mapango ya Amboni mkoani Tanga.
“Baada ya lile tukio wananchi waliweka ulinzi shirikishi, ikawa kila kitu wanawaambia polisi,” alisema.

IGP: Watanzania wanaofanya ugaidi nje hawatuhusu
Akizungumza na Mtanzania jijini Dar es Salaam jana juu ya Watanzania ambao wamehusishwa na matukio mbalimbali ya ugaidi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, alisema jeshi hilo linashughulikia matukio yaliyotokea ndani ya nchi na si yale ya nje.
“Hayo matukio yametokea nje ya nchi hata kama yamehusisha Watanzania, zile ni ‘jurisdiction’ (utawala) nyingine sisi tunashughulikia ya ndani tu,” alisema IGP Mangu na kukata simu.
Awali akizungumza na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu, IGP Mangu aliwataka kukemea vitendo vya uhalifu nchini na kuzitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto wao ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza kwenye uhalifu.
IGP Mangu alisema viongozi wa dini wana dhamana kubwa katika kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa nchini kwa kuwaelimisha waumini wao na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu pamoja na kuwapa mafundisho yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama.
Alisema wahalifu wa sasa wana mbinu nyingi, hivyo kitu kikubwa kitakachoweza kusaidia katika mapambano hayo ni mshikamano wa dhati kutoka kwa viongozi hao katika kuwafichua ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwakilishi wa Mufti
Mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba katika kikao hicho, Sheikh Abubakar Zuber, alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani ambazo zimeanza kujitokeza hapa nchini.
Alisema ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye misikiti, familia zao na hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kubaki salama kwakuwa amani tuliyonayo ni neema ambayo tunapaswa kuilinda kwa nguvu kubwa.
“Vilevile hatuna budi kuimarisha malezi katika familia zetu maana tunaposhindwa kuwalea watoto wetu vizuri ndiyo chimbuko la kushamiri kwa vitendo vya uhalifu wa aina mbalimbali, hivyo tujielekeze katika kutoa mafunzo bora katika familia,” alisema Sheikh Zuber.

WANAZUONI WA KIISLAMU
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Khamis Mataka, alisema uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yoyote na hata ndani ya msikiti, hivyo ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua wahalifu walio ndani ya misikiti.

DK. KITOJO
Mhadhiri wa Chuo cha Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Dk. Wetengere Kitojo, alisema sababu zinazochangia baadhi ya Watanzania kujihusisha na vitendo vya ugaidi ni pamoja na imani za dini na kukosa mafundisho ya uzalendo.
“Baadhi ya watu wanaamini kuwa wakifanya vitendo hivyo ni kueneza dini, inabidi viongozi wa dini wawadhibiti waumini wao.
“Tumeacha mafunzo ya uzalendo, hasa kwa vijana kuipenda nchi yao kiasi kwamba vijana wanashawishika kujiingiza kwenye vitendo vya ugaidi. Vilevile hali ya maisha ya watu imekuwa ngumu mno, vijana wengi hawana kazi, wanadhani wakiingia huko watafanikiwa.
“Inabidi tuwe na mkakati wa kudhibiti watu wetu, vinginevyo nchi yetu itapoteza sifa kama ilivyokuwa ikijulikana kama kisiwa cha amani,” alisema.

TAMKO LA AL-SHABAAB
Kutokana na uvumi uliosambaa kwenye baadhi ya vyombo vya habari juu ya uwezekano wa wanamgambo wa Al-Shabaab kuishambulia Tanzania, kiongozi wa kundi hilo…. Amezikanusha.
Inadaiwa kiongozi huyo alitoa tamko hilo alipokuwa akihojiwa na kituo cha Radio cha Yarat FM ya Somalia.
Kiongozi huyo alisema: “Al Shabaab kamwe hawajawahi kufikiria kushambulia nchi ya Tanzania kwa kuwa hawana sababu ya kufanya hivyo.”
Alisema mbali ya kuzingatia kuwa Tanzania ina raia wengi ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu, pia wanajua na kutambua msaada wa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995 alipotoa tani 500,000 za mahindi kipindi ambacho Somalia ilikumbwa na baa la njaa.
Kiongozi huyo alisema sababu nyingine ya kutoshambulia Tanzania ni kuwa haijapeleka jeshi lake Somalia kama zilivyofanya Kenya na Uganda.
Wanajeshi wachache Watanzania walioko Somalia ni wa jeshi la Umoja wa Afrika (AU).

UMMUL-KHAYR SADIR ABDUL
Machi 30, mwaka huu vyombo vya usalama vya Kenya vilitangaza kumkamata Mtanzania Ummul-Khayr Sadir Abdul (19) na wenzake wawili raia wa Kenya wakiwa mpakani mwa taifa hilo na Somalia, wakidaiwa kuwa njiani kwenda kujiunga na kundi la Al-Shabaab.
Taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El –Wak nchini Kenya, Nelson Marwa, ilisema Mtanzania huyo alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika kilichoko nchini Sudan.
Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ambaye anaelezwa kuwa kiongozi wao, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir.
“Hawa wasichana watatu inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” alisema Kamishna Marwa.
Alisema ingawa nyaraka za wasichana hao zote zinaonyesha kuwa ni wanafunzi, lakini bado walibanwa kwa maswali kuhusu sababu inayowapeleka nchini Somalia.
Alisema raia hao wawili wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichopo Thika, Jimbo la Kiambu na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya Burhania iliyopo Malindi, Kilifi.
“Serikali imepata taarifa kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki ili wakajiunge na makundi ya ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa usalama wamepata taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana hao,” alisema Kamishana Marwa.
Ummul-Khayr alimaliza madarasa ya Quran Zanzibar na baadaye alipata elimu yake ya juu katika Shule ya SOS kabla ya kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu nchini Sudan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles