31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

GESI INAPOGONGANISHA WAKUBWA

w 001

Na Markus Mpangala,

LEO nitakuchambulia kitabu cha ‘Msako’, kilichoandikwa na mwandishi Japhet Nyang’oro Sudi.  Mwandishi huyo anavyo vitabu vingine ‘Ni Zamu yako kufa’, ‘Heka Heka’, ‘Bei Halali ni Kifo’, ‘Mchezo’, ‘Kisasi’, ‘Mkono wa Shetani’, ‘Jacob Matata’ na ‘Patashika’.

Hiki ni kitabu cha kwanza, ama niseme mara yangu ya kwanza kusoma kazi za mwandishi huyu. Kitabu hicho kimechapwa mwaka 2016 na kupewa nambari ISBN 978-9987-79-09-6.

UTANGULIZI

Kitabu hiki kimeanza kutoa dokezo juu ya yanayotarajiwa kujitokeza kitabuni. Mwandishi ametumia mfululizo wa visa vya moja kwa moja kukamilisha riwaya yake.

Kwa mujibu wa mwandishi amepata kunifahamisha kuwa wazo la kuandika kitabu hiki alilipata baada ha kuhudhuria mkutano wa masuala ya gesi asilia huko nchini Hispania.

Msingi mkuu wa riwaya hii ni vita vya gesi baina ya mataifa mbalimbali pamoja na hujuma dhidi ya wataalamu wa ujasusi waliopelekwa mafunzoni huko nchini Cuba.

Mwandishi anaelezea kwa kina juu ya uvumbuzi wa nishati ya gesi asilia unavyowatamanisha na kuwahangaisha wenye uchu wa utajiri kutoka ughaibuni.

Aidha, anatuonesha namna mataifa yetu yanavyokosa wazalendo ambao moja kwa moja unaigusa Ikulu ya nchi. Na namna maisha binafsi ya viongozi yanavyoweza kuathiri kwa njia hasi ndani ya taifa.

MANDHARI

Mwandishi amechagua maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, hususani maeneo ya Masaki na viunga vyake. Katika maeneo hayo anabuni swali; kwanini watu waovu wengi huishi maeneo ya kifahari kama Masaki, jijini Dar es Salaam?

MAUDHUI

Mwandishi anatuonyesha kuwa uvumbuzi wa gesi huko mkoani Mtwara ulivyowahangaisha mataifa makubwa ya Marekani, China, Uingereza na Ufaransa kwa kuyataja machache.

Anaonyesha dhana ya laana ya rasilimali ambapo baadhi ya viongozi akiwamo Waziri Mkuu Noel Makere wanatumika kuhujumu nchi zao kwa dhumuni la kupata madaraka.

Ugunduzi wa gesi huko Mtwara unasababisha mataifa shindani yahangaike kuharibu sifa ya Tanzania. Ili kuhakikisha hujuma inatamalaki, wahujumu wanatumia kila mbinu ikiwamo mauaji ya kutisha baada ya kuitungua ndege iliyobeba wataalamu wa gesi.

Mwandishi anatuonyesha namna wazalendo na waadilifu wanavyoshughulikiwa ili kulinda maslahi ya mabwanyenye. Anamtumia mhusika mkuu Jacob Matata kama mpelelezi mkuu wa sakata hilo pamoja na Mkuu wa Idara ya Usalama Bi. Anitha.

Waama, anatukumbusha tofauti za wanasiasa na wataalamu. Tunaonyeshwa namna nchi inavyokosa wataalamu kiasi cha kumtegemea mtu mmoja, Judith Muga kukamilisha ripoti za ugunduzi wa gesi.

Lakini Judith Muga amepata kuwa na uhusiano wa kimapenzi na rais wa nchi hiyo, Jovin Sekendu. Jambo hilo linampa mwanya Judith kutoa sharti kwa rais ambaye amepata kuzaa Naye mtoto. Hilo linaleta songombingo katika madaraka ya urais.

DHAMIRA

  1. Uzalendo, utaalamu na uadilifu ni vitu tofauti. Mwandishi anasema; “Unaweza kuwa na jasusi mzalendo lakini si mtaalamu. Vilevile unaweza kuwa na mtaalamu lakini si mzalendo.
  2. Usaliti na hujuma hupikwa ndani ya taifa husika, huku wageni wakiwa wadhamini tu.
  3. Mapenzi. Kama ilivyoada mwandishi anamtumia Nanalungu Binti Muhsin kuwa mhusika anayeyachuna mabuzi. Ni mabuzi hayo baadaye yakamdhulumu na kuchagiza kifo cha waziri wa ulinzi.
  4. Alama nyeti (Code names). Katika kanuni za ujasusi zipo nyingi ikiwamo namna ya kuwasiliana. Mwandishi anamtumia Jacob Matata pale anapoandika sentesi kwenye kikaratasi iliyosomeka, “I Trust no one ….”

Nukta hizo 4 zilikuwa na maana nzito kwa mkuu wa idara ya usalama Bi Anitha. Kwa namna nyingine jasusi huwa hamwamini hata rais wa nchi (Sponsor).

  1. Vita vya rasilimali na masoko ni vikubwa, watu wapo tayari kuangamiza roho na kuzichafua nchi zenye neema ya utajiri ili zionekane hazifai. Hapa vinanikumbusha Kitabu cha Trade Is War kilichoandikwa na Prof Yash Tandon.

HITIMISHO

Mwandishi amefaulu kunadi kisa chake kwa kukiwekea nakshi mbalimbali. Kwa maoni yangu kisa hiki kinashabihiana na vingi vilivyomo namna wenye madaraka wanavyotumia nguvu hizo kuhujumu nchi zao ikiwemo kuharibu maisha ya baadhi ya watu.

Ninampatia changamoto mwandishi kuongeza umahiri na utajiri wa maneno, misemo na viungo kama biriyani, binzari, nyanya na vitunguu vya kunogesha simulizi zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles