24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CHAGUZI NDOGO ZA MADIWANI, WABUNGE HUKUZA DEMOKRASIA

Na BARTHOLOMEW WANDI


Wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kuraUCHAGUZI wowote ule, uwe mkubwa au mdogo ni muhimu kwa lengo la kukuza demokrasia na kutoa fursa kwa wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Katika makala hii, nitaelezea umuhimu wa chaguzi ndogo za udiwani na ubunge.

Chaguzi ndogo kisheria zinafanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kupita na hauendelei kufanyika baada ya kubakia mwaka mmoja na miezi sita.

Tanzania ina aina mbili za chaguzi ndogo ambazo ni za madiwani na wabunge wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania.

Ili kuonyesha kwamba uchaguzi mdogo wa madiwani ni muhimu kwa kukuza demokrasia, kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura ya 292) Ibara ya 13(a-e), uchaguzi mdogo wa udiwani utafanyika iwapo Waziri mwenye dhamana wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais (PO), atatangaza kiti wazi cha diwani kilicho wazi atakapopewa taarifa ya maandishi na Mwenyekiti wa Halmashauri husika.

Uchaguzi mdogo wa udiwani unafanyika pale ambapo diwani amefariki au kujiuzulu na hii ni kwa mujibu wa maelezo yaliyo chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Sura ya 292).

Sababu nyingine ni uchaguzi wa mjumbe wa udiwani, unatangazwa kuwa batili au kiti cha ujumbe wa udiwani kinachukuliwa  na kuwa wazi chini ya Sheria za Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura ya 292) au mjumbe wa udiwani anakoma kuwa mjumbe wa udiwani wa chama cha siasa ambacho kilimdhamini mjumbe wa udiwani huo kuwa mgombea.

Aidha, kama nilivyoeleza hapo awali, uchaguzi mdogo wa mjumbe wa udiwani hautafanyika ikiwa imebakia miezi sita kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Januari 22, mwaka huu, itakuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 20 zilizopo katika halmashauri 19 katika mikoa 15, baada ya wajumbe wawakilishi hao kufariki, kujiuzulu na kupoteza sifa.

Pia kuonyesha kwamba uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge ni muhimu kwa kukuza demokrasia, kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343) Ibara 37(3), inaeleza kwamba “Endapo Mbunge anajiuzulu, kufariki au anaachia ofisi kwa sababu nyingine tofauti na zile zilizopo chini ya kifungu cha 113, Spika kwa maandishi kwa Mwenyekiti wa Tume na kwa taarifa itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, atatangaza kwamba kuna nafasi katika kiti cha ubunge”.

Uchaguzi huu wa kiti cha ubunge utafanyika katika Jimbo la Dimani lililopo Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi- Zanzibar, Januari 22, mwaka huu.

Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litawekwa wazi katika vituo vyote vya kupigia kura katika kata 20 na Jimbo la Dimani lililopo Wilaya ya Magharibi ‘B’ katika Mkoa wa Mjini Magharibi-Zanzibar, siku nane kabla ya siku ya uchaguzi yaani kuanzia Januari mpaka Januari 21, mwaka huu.

Siku hiyo ya Uchaguzi, wapiga kura wote wanatakiwa kwenda katika vituo vya kupigia kura wakiwa na kadi zao za kupigia kura. Mpiga kura anashauriwa kutunza kadi yake na kuitumia siku hiyo ya uchaguzi katika kupiga kura na katika chaguzi nyingine zijazo na siku ya uchaguzi, mpiga kura hatakiwi kuvaa nguo zinazoashiria itikadi ya chama fulani cha siasa.

Atakayeruhusiwa kupiga kura ni yule ambaye ni raia wa Tanzania aliyeandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na mwenye kadi ya kupigia kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mpiga kura anatakiwa kufika kwenye kituo cha kupiga kura katika muda uliotangazwa na NEC. Muda uliopangwa na Tume utakapoisha, hakuna mtu mwingine yeyote atakayeruhusiwa kupiga kura ila tu kwa wale ambao muda utakapoisha wapo kwenye mstari, hao wataruhusiwa kupiga kura.

Pamoja na hayo, NEC inawatakia kila la heri viongozi walioteuliwa kushiriki chaguzi za viti vya udiwani na ubunge.

Mwandishi ni Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles