24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

TAIFA LENYE NJAA WATU WAKE HAWAWEZI KUFIKIRI SAWA SAWA

njaaSIKU za hivi karibuni kumekuwa na mjadala unaoashiria huenda Taifa likawa na njaa au likakumbwa na upungufu wa chakula siku za usoni.

Si jukumu langu kutangaza njaa katika Taifa lakini suala la njaa liwepo au lisiwepo; mjadala wenyewe wa uwepo au kutokuwepo kwa njaa unaashiria matatizo makubwa katika mfumo wa usalama wa chakula hapa nchini.

Nchi yetu ni Taifa kubwa na idadi ya watu hivi sasa inafikia milioni 50 na ushehe. Makadirio ya idadi ya watu si jambo la kushitukiza, ni jambo la kisayansi linalofanywa kwa njia ya sensa ya watu na makazi kila baada ya miaka 10.

Makadirio ya idadi ya watu hufanywa ili kuliwezesha Taifa kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kipindi cha muda mrefu.

Hivyo kuwa na viashiria vya njaa au upungufu wa hifadhi ya chakula ni dhahiri kuwa hata kama mipango ya maendeleo ipo basi haina ushirikiano na tafiti na takwimu kama hizi za sensa.

Uwepo tu wa mijadala ya kuwepo kwa njaa au kutokuwepo ni ishara ya wazi kuwa Taifa linaweza kukumbwa na majanga ya kibinadamu na majanga ya asili kwa pamoja bila kutarajia, aidha ni ishara kuwa huenda Taifa halina mkakati wa kukabiliana na majanga ya asili na ya kibinadamu.

Upungufu wa chakula kutokana na janga la ukame katika nchi ni uzembe na ni janga la kibinadamu kwa kuwa linakuwa limesababishwa na uzembe wa binadamu kutoweka mikakati ya kukabiliana na ukame katika uzalishaji wa chakula.

Nchi yetu ina mito mfano wa mto Kilombero ambayo inatiririsha maji kuanzia mwanzoni mwa mwaka mpaka mwisho wa mwaka, hivyo ni uzembe unaosababishwa na binadamu kutokuwa na chakula cha kutosha.

Kinachoitwa miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo ilitimia Desemba 9, 2016 inakuwa haina maana sana kama tunakuwa hatuwezi kuzalisha chakula cha kutosha, kwa ngazi ya kaya, kijiji, kata, wilaya mpaka Taifa.

Uhuru wa Taifa unakuwa na maana kama watu wake wataishi maisha ya utoshelevu wa chakula, utoshelevu wa kiuchumi na utoshelevu wa huduma za kijamii.

Muda huu si muda wa Taifa kupambana na upungufu wa chakula ni muda ambao Taifa lilipaswa kuutumia kupambana kupeleka vijana wetu kufanya uchunguzi wa kisayansi katika mwezi au sayari nyinginezo.

Badala yake bado tunapambana watu wale chakula na maisha yao kustawi. Tukubali kuwa bado tuna safari ndefu na huenda hata viongozi wetu hawajui wanatupeleka wapi, achilia mbali kujua tutafikaje huko tuendako.

Viongozi wetu waliopewa dhamana ya kusimamia ustawi wa wananchi wanapaswa kujitafakari upya kama wameshindwa kusimamia suala dogo la chakula cha kutosha kwa Taifa wataweza vipi kulivusha Taifa kufikia kwenye uchumi wa kipato cha kati?

Ipo sifa ambayo viongozi wa kisiasa wamejichukulia kwa kudai uchumi wa nchi unakuwa kwa asilimia saba lakini ukuaji huo wa uchumi hauna uhusiano na hali ya maisha ya wananchi.

Sifa hii ndiyo inayowafanya wananchi wengi kuwa masikini huku viongozi wao baadhi wakijinasibu kuwa watetezi wa masikini hao.

Jibu rahisi ni kuwa lazima ninyi masikini muendelee kuwa masikini ili viongozi wenu wanaojinasibu kuwa viongozi wa masikini waendelee kubakia madarakani kwa kisingizio cha kuwa viongozi wa masikini.

Masikini ni pamoja na wale wote wanaoshindwa kupata milo mitatu tu kwa siku! Kwa hiyo ipo haja ya wananchi kuongeza juhudi za kujiongezea kipato na kuwa matajiri ili kuwanyima sababu viongozi wanaotumia umasikini wao kutoa hoja za kuendelea kuwatawala milele, haya ndio mabadiliko yatakayomweka kila mwananchi huru na umasikini unaosimamiwa na viongozi wao!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles