28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI MPYA YA MAREKANI ITAKAVYOATHIRI MZANIA WA DUNIA

Donald TrumpSAA chache zimesalia kabla ya kuingia kesho kutwa ambapo kitakachojiri nchini Marekani kitasababisha taswira tatu pacha, kwanza ni kuapishwa kwa Rais Mteule Donald Trump kutoka Chama cha Republican kuchukua nafasi ya Rais anayemaliza muda wake, Barack Obama, kutoka Chama cha Democratic.

Taswira ya pili ni mabadiliko ya sera zinazotarajiwa baada ya Serikali mpya ya taifa hilo kuanza kazi kutokana na Trump kupania ‘kupindua’ mengi kati ya aliyoyasimika Obama katika kipindi chake cha utawala lakini kuna mvuto wa kipekee, kwa kuwa familia mbili zinazotofautiana za anayetoka na kuingia zinapishana katika lango kuu la Ikulu ya Marekani (White House), Obama akiwa na familia ndogo ya watu wanne na Trump akiingia na familia kubwa kuliko ya mtangulizi wake.

Obama ambaye ni rais wa 44 wa Marekani, ana familia yenye asili ya mchanganyiko wa Luo (Kenya), Marekani (Negro), Scotland, Ireland, Ufaransa, Ujerumani na Uswiss kutokana na asili ya nasaba za wazazi wake, huku mkewe Michelle ni mzaliwa wa Chicago, Illinois na wakiwa na mabinti wawili Malia (18) na Sasha (15).

Obama amelelewa na mama yake Ann Stanley Dunham akishirikiana na Bibi na Babu zake (wazazi wa mama yake) Stanley na Madelyn Dunham, familia iliyochanganya nasaba za Uingereza, Ujerumani, Ireland, Scotland, Wales, Uswiss na Ufaransa lakini baba yake ni Mluo wa Jimbo la Nyanza Magharibi nchini Kenya.

Asili yake inaanzia kwa babu yake upande wa baba (Hussein Onyango Obama) aliyezaliwa asubuhi kama maana ya jina Onyango ilivyo kwa Kiluo, Nyaoke ndiye mama aliyemzaa akiwa mke mkubwa kati ya wake watano na baadaye alikuwa mpishi wa wamisionari na tabibu asilia kabla ya kujiunga na jeshi na kupigana vita kuu ya kwanza ya dunia.

Mzee Onyango aliyebadili dini kutoka ya kijadi na kuwa Mkatoliki kisha kuwa Muislamu na kuitwa Hussein na kurithisha jina hilo kwa watoto lakini hakuwarithisha dini yake mpya, alizaa mabinti wawili (Sarah na Auma) na mtoto wa kiume Barack (baba yake Rais Obama) kupitia mkewe wa pili Habiba Akumu Nyanjoga.

Kwa hiyo Rais Obama kwa jina jingine ni ‘Junior’ kwa kuwa baba yake ndiye Barack mkubwa (Senior). Anayekuja kumpokea madaraka, Rais Mteule Donald Trump, asili ya awali ya nasaba yake ni Ujerumani na jina lake la ukoo limetoholewa kutoka neno ‘drum’ ambalo kwa Kijerumani hutamkwa ‘Drumpf’ lakini likihusishwa pia na matoholeo ya Kifaransa kwa Kiingereza likimaanisha ‘mtengeneza matarumbeta’ kwa hiyo usishangazwe na hulka ya Rais mteule kupuliza tarumbeta za kauli za kisiasa kwa kuwa imo katika nasaba ya jina lake.

Ukoo wa Trump una asili ya Kallstadt, Rhineland-Palatinate nchini Ujerumani tangu mwaka 1608 ulikojihusisha na kulima zabibu za mvinyo na baadaye mwaka 1840 walihamia Marekani, wakiwa kizazi kinachotokana na Elizabeth Christ Trump ambapo kuna mlolongo mrefu wa uzao kutoka Henry J. Heinz mwanzilishi wa kampuni ya Heinz ambaye ni mjukuu wa Charlotte Louisa Trump wa Kallstadt hadi kwa wazazi wa Donald, Bwana na Bibi Frederick Christ na Mary Anne Trump, waliomzaa mnamo Juni 14, 1946 jijini Newyork.

Donald amewahi kuoa mara nne akifunga ndoa na Ivana Zelnickova, Marla Maples na Melania Knauss akiwa na watoto wanne kutokana na ndoa zake mbili za awali, Donald Jr, Ivanka na Eric aliozaa na Ivana na Tifanny Trump aliyezaa na Marla na akiwa na mtoto mmoja (Barron) kutokana na ndoa yake ya sasa na Melanie.

Wanawe watatu kwa mkewe wa kwanza (Ivana) ndiyo wanaosimamia biashara za kifamilia za ‘Trump Organization’ ambao Rais mteule alibainisha atawaachia hatamu atakapoanza kutumikia nafasi ya Urais aliyochaguliwa.

Inawezekana nasaba ya kifamilia isiwe na maana yoyote kwenye mashiko ya kisiasa lakini kuna ukweli kuwa hulka ndiyo huakisi mashiko ya mwenendo wa mtu akiwemo Rais, kwani kwa taifa la Marekani dira na ushawishi wa Rais aliye madarakani huvuta pia sera za chama chake na kubainisha mustakabali wa uongozi utakavyokuwa licha ya kulazimika kuzingatia taratibu za kiutawala zilizowekwa.

Unaweza kutathimini dhamira ya Rais mteule kutengua mengi aliyosimika mtangulizi wake, pia namna anavyoteua mabilionea wenzake katika nafasi nyeti za uongozi na akicheza turufu za mabadilishano ya ‘kuchimbana’ na mataifa hasimu na Marekani ikiwemo China na Urusi, ambayo ilibaini ilivyobinywa na Obama na kutetereka kiuchumi hivyo kujijengea mashiko kwa Rais ajaye (Trump) kwa kujipenyeza na kujipendekeza na sasa inaelekea kama mataifa hayo mawili yana mtazamo mmoja kwenye baadhi ya masuala, ambayo zamani yalikuwa yakivutana bila kufikia muafaka wala ufumbuzi wa aina yoyote katika kutunishiana misuli kimya kimya kwenye wigo wa vita baridi.

Hakuna shaka yoyote kuwa mabadiliko yajayo ya serikali mpya ya Marekani yataathiri mzania wa dunia, kutokana na sera za taifa hilo kubwa litakavyoshirikiana na mataifa tajiri na masikini duniani wakati familia mbili zinazotofautiana nasaba zitakapopishana kutoka na kuingia katika Ikulu ya Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles