30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYEMWEKA REHANI NDUGUYE PAKISTANI AACHIWA HURU

*Awekwa ndani kwa miezi minne, giza latanda


 

Pakistani kwa Sh bilioni 1.5.Na Kulwa Mzee- Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Mfanyabiashara Juma Mwinyi maarufu ‘Neti’ aliyekuwa akidaiwa kumweka reheni mdogo wake nchini Pakistani kwa Sh bilioni 1.5.

Uamuzi huo wa mahakama umetolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya kupitia hoja mbalimbali za kisheria na kujiridhisha kwamba mshtakiwa alikamatwa bila kufuata utaratibu.

Juma aliachiwa huru ikiwa ni miezi minne tangu kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akishtakiwa kwa kosa la kusafirisha binadamu kwani alishtakiwa Agosti 3, mwaka jana na aliachiwa huru Desemba 19, 2016.

Awali akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Peter Njike alidai kati ya Desemba Mosi mwaka 2015 na Julai 15 mwaka 2016 jijini Dar es Salaam mshtakiwa alitenda kosa la kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.

Njike alidai Juma alijifanya anakwenda kumpa mafunzo Adam Akida Mkazi wa Magomeni, Mtaa wa Chemchem na Idrisa na badala yake alimsafirisha kwenda nchini Pakistan kwa ajili ya kumweka reheni.

Mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Agosti mwaka jana na kufunguliwa kesi namba 276/2016 ambayo ilifutwa Novemba 11, mwaka jana kwa kutumia kifungu cha sheria namba 225 (5) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kukamatwa tena.

Juma alikuwa chini ya mikono ya Polisi tangu alipokamatwa tena Novemba 1, mwaka jana hadi Novemba 14 ambapo alishtakiwa tena kwa mashtaka haya hayo katika kesi namba 411 ya mwaka 2016.

Wakili wa mshtakiwa huyo Hudson Ndusyep, aliwasilisha hoja mahakamani hapo Desemba 7, mwaka jana akidai mteja wake ameshtakiwa kimakosa kwa sababu sheria za ukamataji zimekiukwa kwani alikamatwa bila kuwepo kwa hati ya kumkamata, hivyo aliomba kesi ifutwe mshtakiwa aachiwe huru.

Akijibu hoja hizo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hellen Mosha, alipinga hoja za utetezi na kuiomba mahakama isimwachie huru mshtakiwa na kwamba hoja ya hati ya kumkamata itaangaliwa wakati kesi inaendelea na hoja za utetezi haziko katika msingi wa kisheria.

Akisoma uamuzi Desemba 19 mwaka jana baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Mkeha alisema mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la kusafirisha binadamu chini ya kifungu namba 4(1)(a)na (5) cha Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Binadamu namba 6 ya mwaka 2008.

Katika sheria hiyo kifungu namba 12 (1) kinasema wazi kwamba polisi hawezi kukamata mtu kwa kosa lolote lilipo chini ya sheria hiyo bila kuwa na kibali cha kukamata, hivyo mahakama ilikubaliana na hoja za utetezi kwamba utaratibu wa kumkamata mtuhumiwa ulikiukwa.

“Kwa mujibu wa sheria hakuna njia nyingine zaidi ya kuondoa mashtaka dhidi ya mshtakiwa na kumwachia huru mshtakiwa.

“Naushauri upande wa mashtaka wakati wowote wanapofuata taratibu za ukamataji wamfikishe mshtakiwa mahakamani,” alisema Hakimu Mkeha.

Mwanzo wa sakata la Juma

Hatua ya kukamatwa kwa Juma, ni matokeo ya gazeti hili kuripoti habari za Mtanzania kushikiliwa ughaibuni kutokana na biashara ya dawa za kulevya Julai 18, mwaka jana.

Habari hizo ziliripotiwa baada ya kipande cha video kusambaa katika mitandao ya kijamii Julai 17, mwaka jana ikimwonesha Adamu Akida amewekwa chini ya ulinzi na maharamia hao wenye silaha.

MTANZANIA lilifuatilia tukio hilo na kubaini kuwa Adamu alikuwa amewekwa rehani kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 kwa kile kilichoelezwa kuwa ilikuwa ni utekelezaji wa mpango wa biashara ya ‘unga’.

Kutokana na hatua hiyo, timu ya MTANZANIA iliamua kuchimbua suala hilo ili kujua ukweli wa namna kijana Adamu Akida, alivyokuwa kwenye mateso hayo.

Akisimulia tukio hilo kaka yake aliyejitambulisha kwa jina la Hemed Abdallah (si jina lake halisi) alisema, Adamu alikwenda kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma na kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya kinyozi haikuwa ikilipa na hali ya maisha ilikuwa ngumu.

Alisema baada ya kueleza shida yake, Juma alimuhoji kama yupo tayari kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi na Adamu alikubali kufanya kazi ya aina yoyote ili mradi aweze kupata fedha.

“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma na kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya hali hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka wakiwa wameandamana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye jina lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.

“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko na angerudi mwezi wa tisa au wa nane.

“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui kama tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni, tulikuwa tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi sana hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia magari,” alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.

Mke alivyohama
Julai 19, mwaka jana chanzo cha uhakika kililiambia MTANZANIA kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.
Mke huyo wa Adamu, alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.

 

Kauli ya Mwenyekiti wa Mtaa

Akizungumza na Mtanzania, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Idrissa, Issa Mpangile, alisema askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika nyumba ya baba mdogo wa Adamu.

Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia Mtaa wa Idisa, ambaye ndiye baba mdogo wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo yake.
Akizungumzia kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa wa Idrissa, Kata ya Magomeni.

Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.

Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.

Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba atakwenda kuripoti kituo cha polisi.

Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.
Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani kwao kuhoji kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.

Inasemekana kijana huyo aliwekwa rehani kwa ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles