27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

BENKI YA WANANCHI MWANGA YAPANGA KUJIUNGA DSE

Jengo la Benki ya Wananchi Mwanga
Jengo la Benki ya Wananchi Mwanga

Na FERDNANDA MBAMILA, DAR ES SALAAM

MIAKA 16 toka kuanzishwa kwa Benki ya Wananchi Mwanga (MCBL) iliyopo Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, sasa ipo katika mchakato wa kuongeza mtaji wake ambao ndio muhimu katika kuomba kibali kuendesha shughuli zake nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCBL, Abby  Ghuhia, anasema tayari suala hili limeingizwa katika mpango wa kibiashara wa miaka mitano na mpango wa ukuzaji mtaji.

“Benki yetu ipo katika mchakato wa kuanzisha huduma za kibenki za kiuwakala ambazo tutakuwa tukizitoa kupitia kwa mawakala watakaokuwa sehemu mbalimbali muhimu na sehemu za vijijini mkoani Kilimanjaro na kwingineko,” anasema Ghuhia.

Hata hivyo, kupitia matawi yaliyopo mkoani Moshi, Same, Hedaru  na Mwanga, bado benki hiyo inayo idadi kubwa ya wateja, ikiwa sambamba na amana kutokana na akaunti za akiba zilizofunguliwa.

“Wigo wa huduma zetu unaokua unategemea  wateja wetu wa vijijini kupitia vikundi vya akiba na mikopo (Vicoba), kupitia huduma hizi, benki yetu imeweza kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini, hasa maeneo ya vijijini ambako asilimia 7 tu ya watu wazima wanahudumiwa na mfumo rasmi wa huduma za kibenki,” anasema Ghuhia.

Aidha, Ghuhia  anasema wanaongeza kasi kuwafikia wanajamii kwa kutoa huduma za kifedha zenye tija kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi huyo ameongeza kusema kuwa MCBL ipo katika mchakato wa kujiunga kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

“Bodi ya benki yetu pamoja na wanahisa tayari wameshaidhinisha hatua hiyo ya kujiunga kwenye Soko la Hisa na tupo katika hatua za awali za kuusoma mchakato huo na kufanya mipango ambayo ilianzishwa mwaka 2000 kama kitengo cha mkoa cha taasisi ya kifedha iliyosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), kufanya shughuli zake katika Wilaya ya Mwanga.

Historia

Wazo la kuanzisha benki za kijamii nchini Tanzania lilitokana na Benki Kuu Idara ya Wajasiriamali (Bank of Tanzania Microfinance Department) ikichukulia mfano kutoka nchini Ghana. Mkakati  ulikuwa ukitaka kutoa huduma za kifedha kwa jamii vijijini  kwa gharama nafuu.

Hii inafuatia huduma za kifedha zikitolewa na benki za biashara kuwa ni ghali na zikitolewa mijini pekee.

Kutokana na hilo, mwaka 2009 Benki ya MCBL ilisajiliwa kufanya shughuli zake mkoani Kilimanjaro kama benki ya kijamii ya mkoa. Hivi sasa MCBL ina matawi 4 ambayo ni Mwanga, Same, Hedaru na Moshi.

MCBL ina wanahisa 5,255 na wateja wapatao 70,769, huku ikijumuisha  wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo na wakubwa, Vicoba na Saccos.

Benki hiyo ina jumla ya mali isiyohamishika yenye thamani ya S bilioni 8.3 na MCBL imekuwa ikipata faida na kutoa gawio kwa wanahisa wake tangu mwaka 2005.

“Mwaka 2000 ilikuwa ni benki ya kwanza wilayani  Mwanga kutoa huduma za kisasa za kibenki kwa njia ya kidijitali na imeboresha zaidi huduma zake zikiwemo huduma za ATM, SIM banking, huduma za kibenki  kwa njia ya kiwakala,” anasema Ghuhia.

Anaongeza kuwa mkakati wa maendeleo wa MCBL ni kukuza mtaji wake na amana zake ambazo ni rasilimali nyingine ili kuweza kutoa huduma za kiushindani ndani ya soko la sasa na kwingineko zaidi.

Kwa kutumia huduma za kibenki kwa njia ya simu na za kiwakala, MCBL itaongeza utumiaji wa bidhaa zake katika mikoa na kwingineko, hasa katika maeneo ya vijijini.

Kuhusu dhima ya MCBL, anasema  ni kutoa huduma bila ubaguzi bila kujali tofauti za kimawazo na kuongeza kuwa benki hiyo inaaminiwa ndani ya jamii kwa sababu ya kanuni yao ya uwazi na uaminifu.

Pia filosofi hii imeiweka MCBL katikati ya jamii kama  taasisi yao wenyewe inayoangalia mahitaji yao ya kifedha kwa gharama nafuu na kuongeza kuwa hiyo ndiyo nguvu ya benki hiyo na kichocheo cha ukuaji kwa miaka yote 16 iliyopita.

“Nimekuwa nikifanya kazi kama mkurugenzi mtendaji wa benki hii kwa zaidi ya miaka kumi. Katika miaka hiyo tumeweza kupata mafanikio mengi lakini nitaelezea machache. Wanahisa watarajie maendeleo makubwa ambayo mimi na timu yangu tumepanga kuyaleta kwenye taasisi yetu,” anasema Ghuhia.

“Tupo katika mchakato wa kupanua huduma zetu nchi nzima kupitia huduma za kiwakala, wateja wetu kwa sasa wanaweza kuzifikia akaunti zao kwa wakati mwafaka kupitia mtandao wa Umoja ATM ambao kwa sasa upo karibu nchi nzima, jukwaa la huduma za kibenki kupitia simu za viganjani, ambapo kupitia usajili wa bure wa kodi  namba USSD ya *150*56, wateja wanaweza kumaliza  miamala yote ya kibenki na kulipa bili mbalimbali kupitia simu zao za viganjani.

“Ndani ya mpango wetu wa biashara wa miaka mitano, benki yetu imeweka mikakati ya ukuaji kwa kuongeza wigo wa soko, uwekezaji wa teknolojia na kujenga uwezo ikiwamo wa mtaji,” anaongeza.

Ndani ya mpango wetu wa biashara wa miaka mitano (2015-2020), MCBL imeweka mikakati ya ukuaji ikiwemo kuongeza wigo wa soko na uwekezaji wa teknolojia na kujenga uwezo.

Ushindani katika sekta ya kibenki nchini  uko juu zaidi kwani benki ni nyingi, mpya na taasisi nyingine za kifedha zimekuwa zikianzishwa na hivyo MCBL bado inaboresha bidhaa na huduma zake ili kukidhi mahitaji ya soko.

Ghuhia anazungumzia changamoto zinazoikabili MCBL kuwa ni pamoja na benki hiyo kufanya shughuli zake katika mkoa mmoja pekee.

“Kutokana na ukweli kwamba tumepewa kibali kufanya shughuli zetu katika Mkoa wa Kilimanjaro pekee, hatuwezi kufungua matawi katika masoko mengine yanayovutia kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na kadhalika. Kwa hiyo, hatuwezi kubadili  mazingira ya kiuchumi kwa ajili ya ukuaji wa benki,” anasema Ghuhia.

Njia za kujikwamua dhidi ya changamoto hizo ni benki za kiwakala ambazo kinadharia zitaondoa mipaka na MCBL ipo kuongeza mtaji wake ili kupewa kibali kuwa benki ya kijasiriamali ambayo inaruhusiwa kufanya shughuli zaidi ya mkoa mmoja.

Changomoto nyingine ni ukwasi  ambapo mahitaji ya mikopo yapo juu zaidi kuliko ukuaji wa akiba.

“Baada ya kufungua vituo vya huduma, wateja wengi wameongezeka kutoka 24,000 hadi 70,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu,” anasema na kuongeza kuwa ukuaji uliongeza mahitaji ya bidhaa ya mikopo ikilinganishwa na ukuaji katika amana.

“Wateja huweka fedha zao katika akaunti zao tu ili waweze kukidhi vigezo vya kupewa  mikopo. Hali  hii iliongeza msukumo wa kiukwasi ambayo ilitulazimu kukopa  fedha kutoka taasisi nyingine za kifedha kwa kiwango cha riba za juu ili kukidhi mahitaji,” anasema Ghuhia.

MCBL inajaribu kupunguza changamoto hii kwa kutangaza bidhaa zake za kifedha zinazokidhi mahitaji ya jamii.

MCBL imekuwa ikitembelea nyumba hadi nyumba kwa wateja wake watarajiwa kukuza bidhaa za benki pamoja na kuuza  bidhaa nyingine zinazotolewa na benki kama vile huduma za bima, huduma za utumaji fedha wa kimataifa na nyinginezo kama hizo.

Aidha, Ghuhia anasema sekta ya kibenki ni muhimu  kwa ukuaji uchumi wa nchi kwa utoaji mitaji kwa sekta binafsi kupitia utoaji mikopo kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Ghuhia anasema wajibu wa Serikali ni kutoa mazingira ya kiuwezeshaji kupitia sera za kiuchumi, kifedha na kikodi, ili kuleta mabadiliko katika uchumi wa kijijini, Serikali inapaswa kuziunga mkono taasisi za kifedha zikiwemo benki za kijamii zifanyazo kazi maeneo ya vijijini na kutoa mitaji kwa wakulima   kupitia mikopo  kwa uzalishaji wa mazao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles