27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TABIA SABA ZITAKAZOKUWEZESHA KUTEKELEZA MALENGO UNAYOJIWEKEA – 2

hand writes with a pen in a notebook

Na CHRISTIAN BWAYA,

MAKALA iliyopita tuliona tabia nne zinazoweza kukukwamisha. Moja ni kujenga tabia ya kuyatazama mambo kwa malengo mrefu; kuacha visingizo na kuamua kuwajibika na kutokufanya mambo mengi kwa wakati mmoja; kujifunza kusema hapana kwa mambo yasiyoendana na mipango yako.

Katika makala haya, tunaangazia tabia nyingine tatu unazohitaji kuzijenga ili utekeleze malengo yako.

Jitenge na watu wasiokujenga

Upo ukweli kuwa kila mmoja wetu ni wastani wa watu wanne tunaotumia nao muda mwingi. Huwezi kuwa tofauti na watu wanaokuzunguka. Watu unaowasiliana nao kila siku ndio wanaotengeza wajihi wako. Kuwa makini na aina ya watu unaowapa nafasi ya kuhusiana na wewe katika maisha halisi na hata mitandao ya kijamii.

Chagua watu wanaofanana na malengo yako. Tafuta watu wanaoyaishi malengo uliyonayo. Kama unataka kuwa na familia imara mwaka huu, jenga urafiki na watu wenye familia imara. Utajifunza kwao. Kama unataka kufanya biashara fulani, jenga urafiki na watu wanaofanya biashara hiyo.

Usipoteze muda na watu wasiosaidia kutekeleza malengo yako. Usipoteze muda na watu walio kinyume na malengo yako. Huwezi kuwa na familia imara kwa kutumia muda mwingi na watu wasiojali familia zao. Utajikuta unabadilika hatua kwa hatua bila kujua. Maji ya moto hayawezi kuendelea kuwa moto kama yakichanganywa na maji ya baridi. Chagua marafiki kwa kuangalia malengo yako.

Hata hivyo, hii haimaanishi usiwe na uhusiano na watu wote. Unaweza kuhusiana na watu bila kuwafanya marafiki zako.

situmikishwe na mitandao ya kijamii

Tunaishi katika wakati ambao mawasiliano yamerahisishwa kuliko wakati mwingine wowote. Ni rahisi, kwa mfano; ndani ya dakika tano tangu unapoamka, kujua nini kimetokea duniani kote. Ukiwa kwenye mitandao kama Facebook, Twitter, Instagram na Whatsapp, huna sababu ya kuzitafuta taarifa, bali zinakufuata uliko.

Katika mazingira kama hayo, ni rahisi kupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii. Tafiti zinazonesha kuwa watu wengi wanapoteza muda mwingi kwenye mitandao hii. Mrejesho wa papo kwa hapo unaowezeshwa na mitandao hii, unajenga utegemezi. Ni aina fulani ya ulevi.

Usiposhinda utegemezi unaojengwa na mitandao hii, itakuwa vigumu mno kutekeleza malengo yako. Isipokuwa kama kazi zako zinategemea mitandao hii, jiwekee muda maalumu wa kuingia kwenye mitandao hii.

Usikate tamaa unaposhindwa

Wakati mwingine tunashindwa kutekeleza malengo yetu kwa sababu tunakuwa wepesi kukata tamaa pindi mambo yanapokwenda vile tusivyotarajia. Tabia hii ya kughairi mambo kirahisi haiwezi kukusaidia kutekeleza mipango yako. Jifunze kuwa imara hata pale mambo yanapoharibika.

Kama ulipanga kuanza kuweka akiba mwaka huu, si lazima uweze kuweka kiasi kamili cha fedha ulichopanga kuanzia Januari. Ukweli ni kuwa unaweza kufanikiwa kuweka kiasi kidogo au ushindwe kabisa. Usiwe mwepesi kughairi mpango huo kwa sababu tu ulifikiri ungeweza kuweka kiasi cha fedha ulichokipanga kirahisi.

Jifunze kuwa na nguvu ya uamuzi isiyoyumbishwa na matokeo hasi. Jipange upya kwa kutathimini kile ulichokosea na rudia tena na tena. Nguvu ya uamuzi ndiyo inayowatofautisha watu wanaotekeleza malengo yao na watu wanaoachana na mipango yao mara tu wanapoona dalili za kushindwa.

Wakati mwingine watu watakukatisha tamaa. Kwamba unachokifanya hakiwezekani. Usikubali kukatishwa tamaa.

Itaendelea

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles