31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CHUNGWA LINAWEZA KUZUIA MAWE KWENYE FIGO

chungwa

Na HERIETH FAUSTINE,

CHUNGWA ni kati ya matunda yanayopendwa kutokana na kuwa na ladha tamu wakati wa kulila. Tunda hili hulimwa kwa wingi duniani.

Watu wengi wamekuwa wakila  machungwa kama kiburudisho bila kujua kama tunda hilo lina faida katika mwili wa binadamu.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa kwenye tunda la chungwa, iligundulika kuwa tunda hilo lina uwezo mkubwa wa kuponya matatizo mbalimbali ya kiafya kwa sababu lina mkusanyiko mkubwa wa virutubisho vya Phytonutrients.

Jarida la Masuala ya Lishe la Nchini Uingereza (British Journal of Nutririon), liliandika kuwa tunda hilo husaidia kujikinga na ugonjwa wa kupatwa na mawe kwenye figo na lilisema  wanawake waliokunywa nusu lita mpaka lita moja ya juisi ya machungwa  kila siku, usafishaji wa njia ya mkojo uliongezeka na hivyo kuondoa kabisa hatari ya kuwa na mawe kwenye figo (calcium oxalate stones).

Pia katika utafiti mwingine uliofanywa na Kitengo cha Virutubisho vya Binadamu cha Chuo Kikuu, Milan, Italia ulisema glasi moja ya juisi ya machungwa hutoa kinga sawa na vidonge vya vitamin C.

Utafiti huo ulisema juisi halisi ya machungwa ina faida nyingi za kinga katika mwili kuliko kula vidonge vyake (food supplement)

Pia tunda la chungwa ni chanzo kizuri cha ufumwele (fiber) ambapo hutoa asilimia 12.5 kwa kila chungwa.

Vile vile kirutubisho hiki kimeonekana  kuwa na  uwezo mkubwa wa kupunguza mafuta mabaya mwilini (cholesterol) na kinasifika  kwa kudhibiti kiwango cha sukari mwilini. Hivyo, chungwa ni muhimu kwa wagonjwa wa kisukari, hasa wanapokula pamoja na nyama zake.

Sukari ya asili inayopatikana kwenye chungwa (fructose), inaweza kusaidia kudhibiti kupanda kwa kiwango cha sukari mara baada ya mgonjwa kula chakula.

Mbali na hilo, machungwa pia hutoa nafuu kwa watu wanaosumbuliwa na tumbo au ugonjwa wa kuharisha.

Tunda hili pia lina kiasi cha asilimia 10 ya ‘folic acid’ inayohitajika mwilini kila siku ambapo madini hayo ni muhimu kwa afya ya ngozi na ukuaji wa ubongo kwa ajili ya kuimarisha kumbukumbu na uwezo wa mtu wa kufikiri.

Vitamin C iliyomo kwenye chungwa huimarisha uzalishaji wa seli nyeupe ambazo ni muhimu kwa uimarishaji wa kinga ya mwili, unapokuwa na  kinga imara huwezi kusumbuliwa na magonjwa mara kwa mara kama malaria.

Kutokana na tunda hili kuwa na wingi wa virutubisho vya kinga, husaidia kuepusha kuwa na magonjwa ya kuambukiza kama mafua, ambayo hivi sasa yanawasumbua watu wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles