23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YATOA MAFUNZO KODI KWA WASANII

Kaimu Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA , Diana Masala akifafanua jambo wakati wa mkutano
Kaimu Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA , Diana Masala akifafanua jambo wakati wa mkutano

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea na mpango mkakati wake wa kuhakikisha inatoa elimu ya kodi na inamfikia kila mdau ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kodi na uhiyari wa kuilipa.

Hivi karibuni mamlaka hiyo ilikutana na wasanii mbalimbali wa maigizo na muziki ili kuwafundisha kuhusu masuala mbalimbali ya kodi pamoja na umuhimu wa kulipa.

Suala la ulipaji wa kodi lilikuwepo tangu enzi za zamani ambapo hata katika vitabu vya dini huzungumzia kuhusu kodi.

Kodi ni kitu muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi na kwamba maana yake ni makato ya lazima ambayo kila mtu mwenye kipato lazima alipe kwa mujibu wa sheria za nchi na si ombi.

Pia kodi ni tozo ambayo inapatikana kutokana na vyanzo vitatu ambavyo ni ajira, biashara pamoja na uwekezaji na kwamba inatozwa kwa mamlaka ya sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.

Sheria hiyo ya kodi inaunda upya mfumo wa kodi ya mapato kulingana na mahitaji ya kisasa na kubatilisha sheria ya kodi ya mapato ya 1973.

Mafanikio mengi katika nchi mbalimbali zilizoendelea duniani yametokana na makusanyo ya kodi ambapo huiwezesha nchi kuboresha huduma mbalimbali za maendeleo.

Katika semina na wasanii hao, TRA iliwafundisha kuhusu Kodi ya Mapato pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kwamba kila mtu mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Sambamba na kuwapa elimu ya kodi, pia ilipokea maoni mbalimbali kutoka kwa wasanii hao ili kuweza kujua changamoto wanazokabiliana nazo waweze kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya kazi zao zitakazowapatia kipato ambacho watatakiwa kukitumia kulipia kodi.

Kila mafanikio ambayo Serikali imekuwa ikiyapata hutokana na makusanyo ya kodi ambazo wananchi hulipa mfano ujenzi wa barabara, shule, hospitali nk.

Wasanii ni wadau muhimu katika nchi kutokana na mchango mkubwa katika ulipaji wa kodi na kwamba Serikali inatakiwa kuhakikisha inawatengenezea mazingira mazuri ya ufanyaji wa kazi zao ili waweze kufaidika lakini pia Serikali iweze kupata mapato kutoka kwao.

Lakini pia wasanii wote ambao hawajajisajili wanatakiwa kuhakikisha wanajisajili katika ofisi za TRA kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) na baadaye atakadiriwa kodi anayostahili kulipa kulingana na namna anavyopata mapato yake.

Kila msanii ambaye mauzo ghafi yake hayafikii milioni 20 kwa mwaka atahesabika kama mlipa kodi mdogo ambaye atakadiriwa kodi kulingana na mauzo yake au faida aliyoipata.

Ikumbukwe kuwa watu wanaotakiwa kulipa kodi ni vyombo pamoja na watu binafsi.

Chombo kinaweza kuwa shirika au mfuko na kwamba haijalishi kimesajiliwa au hakijasajiliwa pia kinaweza kuwa cha watu au chama.

Kwa upande wa watu ambao si wakazi, utozwaji wake wa kodi ni kwa chanzo cha mapato ya Tanzania tu na si vinginevyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Diana Masala, anasema kila msanii mwenye sifa za kulipa kodi anatakiwa kulipa na kwamba huduma nzuri zinazotolewa na Serikali zitatumiwa na kila Mtanzania bila kubagua.

Anasema Serikali imedhamiria kutengeneza mazingira mazuri ambayo yatarahisisha maisha ya wananchi wake hivyo kila anayestahili kulipa kodi anatakiwa kulipa ili aweze kufaidika na huduma hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles