24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KIGAMBONI YATAFUTA WAWEKEZAJI UTALII

img_2483

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

WILAYA ya Kigamboni ni moja ya wilaya mpya za Jiji la Dar es Salaam yenye vivutio vingi vya utalii ingawa havitumiki vilivyo na hivyo kukosa watalii.

Moja ya utalii huo ni uwepo wa fukwe kubwa zenye mchanga mweupe na zenye utulivu wa hali ya juu ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kuwa vivutio kusaidia kuinua uchumi wa Kigamboni.

Moja ya kivutio kikubwa ni kuwapo kwa kisiwa cha Sinda kikiwa mojawapo ya visiwa sita kwenye miliki ya Wilaya ya Kigamboni ambacho kina maajabu na malikale nyingi.

Kisiwa hicho kipo Mashariki mwa makao makuu ya wilaya hiyo ikiwa ni kilomita chini ya kumi kutokea katika barabara ya Mjimwema.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashimu Mgandilwa, ametembelea kisiwa hicho akiwa na waandishi wa habari na kikundi cha mazoezi cha Feri ikiwa ni kampeni yake ya kuinua utalii.

Baada ya kujionea vivutio vilivyopo kisiwani hapo, Mgandilwa anasema kuwa Watanzania wengi hawajui vivutio vilivyopo kisiwani hapo.

“Kama tulivyoona kuna vivutio vingi hapa lakini wageni hasa Watanzania wanaofika hapa ni wachache, hii inatudhihirishia kuwa eneo hili halijatangazwa vya kutosha,” anasema Mgandilwa.

Anasema eneo hilo lina ufukwe mkubwa uliotulia ambao unafaa kwa mapumziko.

“Kuna jengo ambalo linadaiwa kuwa ilikuwa hoteli iliyojengwa na wakoloni wa Kijerumani miaka 200 iliyopita kwa kutumia mawe na chokaa,” anasema.

Mgandilwa anasema eneo hilo lina mazalia ya kasa ambao hutoka baharini na kuingia kwenye matumbatu yaliyopo kisiwani hapo kwa ajili ya kuzaliana.

Aidha, anasema Sinda  kuna mbuyu mkubwa unaofanana umbo na chupa ya shampeni (kama inavyoonekana pichani)  ambayo huvutia wengi wanaofika kisiwani hapo.

“Gharama za kutembelea maliasili zilizopo hapa ni ndogo sana kwani kwa Mtanzania analipia shilingi 2,000 na mgeni kutoka nje analipa dola za Marekani 10 (sawa na shilingi 20,000) hii ni gharama ya chini,” anasema Mgandilwa.

Anasema changamoto iliyopo katika kisiwa hicho ni kwamba hakijatangazwa vya kutosha kuweza kupata watalii  wa nje  na wa ndani wengi.

“Changamoto nyingine hapa ni upatikanaji wa usafiri wa kutoka Kigamboni kwenda kisiwani kwa kuwa ni lazima ukodi boti,” anasema Mgandilwa.

Mgandilwa anasema juhudi zinafanyika kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuona namna ya kuboresha mazingira na usafiri ili idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje kufika katika kisiwa hicho.

“Tatizo lingine hapa ni upatikanaji wa chakula na vinywaji ambavyo mgeni hulazimika kuja navyo ama kuagiza siku moja kabla ya kuja hapo,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa kikundi kinachohifadhi eneo hilo, Uwesu Rashid, anasema eneo hilo ni salama na halina viumbe hatari kwa binadamu.

“Hakuna vitisho vyovyote katika eneo hili kwa kuwa walinzi wetu hulala hapa na hawajawahi kuripoti tatizo lolote,” anasema Rashidi.

Anasema wamekuwa hapo tangu mwaka 2007 na kupokea wageni mbalimbali wengi wao wakiwa ni kutoka nchi ya Nigeria.

“Tunapokea wengi wenye umri kati ya miaka 30 na kuendelea ambao hutembelea eneo hilo kati yao Watanzania ni wachache,” anasema Rashid.

Kwa upande wake baharia, Rashid Hamis ambaye huwasafirisha watalii kwenda kisiwani hapo kwa kutumia boti anasema kazi hiyo imempa mafanikio japokuwa haina wateja wengi.

“Kazi hii imeweza kuniendeshea maisha yangu ya kila siku na kwa kuwa nimezoea baharini sitamani kufanya kazi nje na bahari,” anasema.

Akizungumzia changamoto alizonazo ni uhaba wa wateja wanaokwenda visiwani kutokana na utalii wa ndani kutokutangazwa vya kutosha.

“Kama visiwa hivi sita vingetangazwa vizuri naamini kuwa tungepata wateja wengi na kuboresha ajira zetu,” anasema Hamis ambaye ni baharia anayesafirisha  abiria kwenye boti kati ya Sinda na Kigamboni na visiwa vingine.

Mwenye jukumu la kutangaza ni Serikali na Bodi ya Utalii.

Naye mwanamama mwanamuziki wa miondoko ya kufokafoka kutoka nchini Marekani, Akua Naru, aliyekuja kutalii  Tanzania anasema eneo la Kigamboni ni sehemu tulivu hasa kwa mtu anayetaka kupumzika. Akua alishiriki katika zoezi la kufanya usafi ufukweni Kigamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles