27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CUF WATEMBEZA BAKULI KUSAKA FEDHA ZA KAMPENI

salim-abdallah-bimani

NA ASHA BANI

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaidai Serikali ruzuku ya zaidi ya Sh milioni 600 na kuwapa wakati mgumu katika kipindi cha uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar.

Kukosa ruzuku kwa chama hicho kunatokana na mgogoro uliotokana na kurudi kwa Profesa Ibrahim Lipumba katika nafasi yake ya uenyekiti licha ya kujiuzulu Agosti, mwaka juzi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Kwa sasa Profesa Lipumba anatambulika na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ni mwenyekiti halali jambo lililozua mgogoro na kusababisha kesi ya kumpinga kufunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa CUF, Salim Bimani, alisema kukosa ruzuku si shida kwao kwa kuwa CUF ni taasisi.

Bimani alisema kwa sasa wananchi na viongozi mbalimbali wa chama hicho wanaendelea kujichangisha kwa lengo la kufanikisha kampeni za uchaguzi huo na mwingine wa madiwani unaofanyika Januari 22, mwaka huu.

Alisema tayari wameanza kuchangishana na kila jimbo kati ya majimbo 54 yametakiwa kutoa kiasi cha Sh 300,000.

Pia alisema kila wilaya kati ya 11 imepewa maagizo ya kupeleka kiasi cha Sh 100,000.

“Chama hiki ni cha watu, chama ni taasisi na wananchi wamesema watakichangia kwa nguvu zao zote kuhakikisha wanafanikisha uchaguzi huo,” alisema Bimani.

Juzi CCM walizindua kampeni hizo na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, alimnadi mgombea wa chama hicho, Juma Ali Juma na kurusha makombora CUF.

Kesho CUF kupitia Katibu Mkuu wake, Seif Shariff Hamad, watazindua kampeni hizo pamoja na kumnadi mgombea wao, Abdulrazak Khatibu Ramadhani.

Uchaguzi huo unarudiwa kutokana na kifo cha mbunge wake, Hafidhi Ali Twahir.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles