26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo Ikulu aburuzwa Madili kwa Escrow

mnikuluNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
KIGOGO wa Ikulu (Mnikulu), Shabani Gurumo, amelishangaza Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kusema hakufahamu sababu za kuwekewa kiasi cha Sh 80,850,000 kwenye akaunti yake.
Mnikulu huyo alipinga madai ya yeye kupewa fedha na Kampuni ya VIP Engineering ila alipewa na James Rugemalira kutokana na urafiki wao walionao kwa muda wa miaka 10 na hazihusiani na mgawo.
Alisema wakiwa katika mazungumzo na rafiki yake Rugemalira, alipewa maelezo ya kumtaka aende kufungua akaunti katika Benki ya Mkombozi ambapo baada ya siku moja alikuta ameingiziwa kiasi hicho cha fedha ambapo alihisi ni za kuuguza mgonjwa wa saratani aliyekuwa naye.
Gurumo alitoa kauli hiyo jana mbele ya Baraza la Maadili alipokuwa akijitetea kutokana na tuhuma za kuwa mmoja wa viongozi waliopokea fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambapo muda wote alijikuta akibanwa na wanasheria wa baraza hilo.
Kauli hiyo ya Gurumo ilikuja baada ya kusomewa mashtaka na Wakili wa Sekreterieti ya Maadili, Hassan Mayunga, ambaye alisema kosa la kigogo huyo ni kuchukua fedha kinyume na maadili ya watumishi wa umma pamoja na kuomba fadhila za kiuchumi.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji mstaafu Hamis Msumi, alimtaka Gurumo kutoa utetezi wake ambapo muda wote alikuwa akiongozwa na wakili wake Lucas Kamanija, ambaye alikuwa akipambana na mawakili wa baraza hilo wakiongozwa na Getrude Cyriacus na Mayunga.
Mahojino kati ya Gurumo na mawakili yalikuwa kama ifuatavyo:
Getrude: Ulifahamu sababu na malengo ya kuwekewa hizo fedha?
Gurumo: Sikuelewa sababu za kuwekewa fedha hizo na ndiyo maana nilizitumia kwa matumizi yangu.
Getrude: Nikirejea taarifa yako uliyotoa katika Tume ya Maadili, ulisema kuwa inawezekana fedha hizo Rugemalira alikupatia baada ya kupata taarifa kwamba una mgonjwa wa saratani unayehitaji kumpeleka India, je ni sawa?
Gurumo: Sikuzitumia fedha hizo peke yake kwenda India kwa sababu ninamiliki fedha nyingi zaidi ya hizo na wala sikupewa masharti ya jinsi ya kutumia.
Getrude: Ulipopata fedha hizo ulitoa taarifa kwa ofisa masuhuli kama sheria ya maadili inavyosema?
Gurumo: Ndiyo nilitoa kwa mkurugenzi wangu.
Getrude: Kwani mkurugenzi ndiye ofisa masuhuli wa Ikulu au ni Katibu Mkuu.
Gurumo: Sikumwambia kwa sababu fedha hiyo haikuwa zawadi ila ilikuwa fedha yangu halali na matumizi yake hakuhitaji mtu kunipangia kutumia.
Getrude: Kama haikuwa zawadi ilikuwa nini?
Gurumo: Aulizwe Rugemalira aliyenipa zilikuwa za nini?
Getrude: Unafahamu kwamba VIP Engineering iliyokupatia fedha ilikuwa na hisa IPTL?
Gurumo: Nimesema tangu mwanzo aliyenipatia fedha alikuwa Rugemalira na si Kampuni ya VIP ambayo nilijua baada ya kuitwa kwenye Tume ya Maadili ndipo nikaambiwa kwamba zimetoka VIP.
Baada ya Getrude kumaliza kumuhoji, wakili mwingine wa Tume ya Maadili, Hassan Mayunga, aliendelea kumuhoji na mahojiano yalikuwa hivi:
Mayunga: Umekuwa ukijaza fomu ya maadili ya kueleza mali, madeni na rasilimali?
Gurumo: Ndiyo nimekuwa nikiijaza kila mwaka.
Mayunga: Umesema mkurugenzi ndiye ofisa masuhuli wako?
Gurumo: Ndiyo.
Akitoa ushahidi wake, ofisa upelelezi wa sekretarieti, Mazingilo Mwanakachwe, alisema anaamini mtuhumiwa alipokea kiasi cha Sh milioni 80.8 kutoka kwa Kampuni ya VIP Engineering.
Sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa kigogo huyo, Lucas Kamanija na Mwanakachwe yalikuwa hivi:
Wakili: Umewahi kumfanyia uchunguzi mlalamikiwa?
Mwanakachwe: Ndiyo.
Kamanija: Taarifa za tuhuma dhidi yake ulianza kuzisikia wapi?
Mwanakachwe: Nilianza kuzisikia kwenye vyombo vya habari na mitandaoni.
Kamanija: Viliandika amepokea kiasi gani?
Mwanakachwe: Milioni 800.
Kamanija: Kwenye hati ya mashtaka anatuhumiwa kupokea shilingi ngapi?
Mwanakachwe: Hati ya mashtaka inasema alipokea kiasi cha Sh 80,850,000.
Kamanija: Kwahiyo yaliyoripotiwa yalikuwa ya uongo?
Mwanakachwe: Nusu kwa nusu, kupewa fedha ni kweli, lakini kiasi ndicho hakikuwa sahihi. Kwa mujibu wa kazi zetu tunapopata taarifa huwa tunazifanyia uchunguzi na kubaini ukweli.
Kamanija: Ni kweli mlalamikiwa aliomba fadhila za kiuchumi kwa Kampuni ya VIP Engineering kama nakala ya mashtaka inavyodai?
Mwanakachwe: Ndiyo, aliomba fadhila za kiuchumi kiasi cha sh 80,850,000.
Kamanija: Unataka kusema mlalamikiwa alipata fedha kwa watu wawili; James Rugemalira na VIP Engineering.
Mwanakachwe: Alipokea kwa chanzo kimoja ambacho ni Kampuni ya VIP Engineering inayomilikiwa na Rugemalira.
Kamanija: Unaweza kuonyesha baraza katika hati kama kuna sehemu inayosema Rugemalira ndiye mmiliki wa VIP Engineering, kama ipo sema ipo na kama haipo sema haipo.
Mwanakachwe: Kwenye hati hakuna.
Kamanija: Je, taarifa aliyoitoa kwenye Tume ya Sekretarieti ya Maadili kuna sehemu inaonyesha mtuhumiwa aliomba fedha hizo?
Mwanakachwe: Hapana, hakuomba ila alipokea.
Kamanija: Kwa uelewa wako kuna kosa gani mtu kuwekewa fedha?
Mwanakachwe: Kosa kwa huyu linakuja kutokana na ukweli kwamba ni kiongozi wa umma na sheria za maadili zinakataza kuomba, kupokea zawadi inayozidi kiasi cha Sh 50,000.
Kamanija: Kwa vipi alitumia wadhifa wake kujihusisha na mahusiano ya kibiashara?
Mwanakachwe: Kwa kutumia wadhifa, majukumu aliyonayo katika taasisi yake atakuwa anafahamu mambo mengi na siri nyingi za Serikali, hivyo angeweza kujiingiza katika mgongano wa kimasilahi.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Hamis Msumi, alisema atatoa uamuzi Machi 13, 2015 na kupelekwa katika mamlaka husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles