24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Machali kutogombea ubunge Kasulu Mjini

OLYMPUS DIGITAL CAMERANa Mwandishi Wetu, Kigoma
MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ametangaza rasmi kwamba hatagombea tena ubunge wa jimbo hilo wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amesema ingawa alikuwa na nia ya kuendelea kuongoza jimbo hilo, amelazimika kuacha kwa kuwa baadhi ya viongozi wa chama chake wilayani Kasulu wanachafua jina lake bila sababu.
Machali alitangaza msimamo huo juzi mjini Kasulu alipohutubia mkutano wa hadhara.
“Kuna baadhi ya viongozi wachache wenye mawazo ya kijinga wanaotoka Jimbo la Kasulu Vijijini wanashirikiana na Diwani wa Kata ya Kasulu Mjini, Issack Rashid maarufu kama Mkemwema, kunitangaza kwamba nimechukua uamuzi huu kwa sababu Mkemwema anataka kugombea ubunge katika jimbo langu.
“Hiyo siyo kweli, ugomvi wangu mkubwa na hao watu umekuja kwa sababu ninapiga vita ufisadi na mafisadi waliopo Wilaya ya Kasulu wanaojali masilahi yao badala ya wananchi.
“Mimi sipendi usumbufu na wananchi ingawa wengine wanatembea huku na huko wakisema ‘Machali hatujali’… hivi mnafikiri atatokea mbunge atakayemaliza shida zenu zote?
“Kama atatokea huyo mbunge basi njooni mniombe silaha yangu mnipige risasi nife kwa sababu naamini mbunge huyo hayupo na hatatokea katika dunia hii.
“Watu wananipiga vita bila sababu kwa vile napingana nao, yaani wanataka na mimi nipige madili kama wao, hiyo haiwezekani kwa sababu siko tayari kuchafua jina langu.
“Wananisingizia mambo ya uongo, kama tatizo ni ubunge, basi nimeamua sitagombea ili historia ije inihukumu kwa sababu ninapopinga ufisadi, mafisadi na watu wa shetani wananipinga,” alisema Machali.
Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kutoa kauli hiyo, alikumbana na upinzani mkali baada ya baadhi ya wananchi kupingana naye huku baadhi wakilia.
Baadhi ya wananchi hao walisikika wakisema hawako tayari kukubaliana na mbunge huyo kwa kuwa wanaridhishwa utendaji kazi wake.
“Usiache kugombea maana wewe ndiyo kimbilio letu kwa sababu umetusaidia katika maeneo ya Kagerankanda wakati tulipokuwa tukinyanyaswa na Mkuu wa Wilaya mstaafu, Dan Makanga.
“Wewe ulisimama na sisi na leo Makanga hayupo tena, kwa hiyo, kama usipogombea sisi wanyonge tutatetewa na nani,” walisikika baadhi ya wananchi wakisema.
Baada ya wananchi hao kusema hayo, Machali alisimama tena na kuomba apewe muda atafakari maombi yao.
“Naomba nipewe muda wa kutafakari, wazee wangu nimewasikia, vijana wenzangu nimewasikia na akina mama nimewasikia pia. Niacheni nitafakari kwa sababu sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,” alisema Machali.
Katika mazungumzo yake, Machali alimshutumu pia Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogela (NCCR-Mageuzi), kwamba wanachangia kukiharibu chama hicho wilayani Kasulu.
“Viongozi wa Jimbo la Kasulu Vijijini hawawezi kunifanya mimi na wana NCCR-Mageuzi Kasulu Mjini kuwa watumwa wa fikra zao mgando kwa sababu nilikwenda darasani kusoma ili nielimike na elimu yangu niitumie kwa manufaa na maendeleo ya jamii yangu.
“Ukweli unauma na wakati mwingine unatuponza wachache, kwa hiyo, sitaogopa kusema ukweli na kutetea ninachokiamini hata kama nawaudhi baadhi ya wenzagu,” alisema.
Pia aliwataka polisi wilayani Kasulu wasiwakamate ovyo waendesha bodaboda kwa kuwa bodaboda zimekuwa msaada mkubwa katika jamii.
Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi, Jimbo la Kasulu Mjini, Benedickt Rukubigwa, alisema viongozi mzigo wa jamii ya Mkemwema, wanatakiwa kuvuliwa madaraka kwa kuwa wanakiharibu chama chao.
“Mke Mwema ni bora akaombe uongozi CCM ambako kuna watu wa aina yake kuliko kuendelea kukigawa na kukivuruga chama chetu,” alisema Rukubigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles