23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kituo ch Mabasi Ubungo dhahabu inayonufaisha wachache

ubungoKoku David na Faraja Masinde, Dar es Salaam

KITUO cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo, (UBT), kilifunguliwa Desemba 6 mwaka 1999, lengo likiwa ni kutoa huduma nzuri kwa wasafiri na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kufunguliwa kwa kituo hicho, kati ya mwaka 2004 mpaka 2008, ziliibuliwa tuhuma mbalimbali za ufisadi zikiwamo upotevu wa mapato, zilizokuwa zikiihusu Kampuni ya Smart Holdings ya familia ya kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru. Tuhuma hizo baadaye zilikanushwa na Serikali.

Tofauti na ilivyokusudiwa, mapato mengi yaliyokusanywa kwenye kituo hicho yaliishia kunufaisha watu wachache.
Machi 15 mwaka 2009, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliagiza ufanyike ukaguzi maalumu kwenye kituo hicho kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zimeibuliwa.
Julai 28 mwaka 2009, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali wa wakati huo, Ludovick Utouh, alikabidhi ripoti yake kwa Waziri Mkuu ikieleza ukusanyaji mbaya wa mapato ikiwa ni pamoja na tuhuma za ubadhirifu wa mapato ndani ya kituo hicho cha mabasi.
Baada ya ripoti hiyo, Kampuni ya Smart Holding iliyokuwa ikikusanya mapato kwenye kituo hicho, ilisimamishwa na jukumu lake likachukuliwa na halmashauri ambayo iliweka watumishi wake kukusanya mapato.
Hali ya kituo kwa sasa

Ili kubaini hali ya kituo hicho, MTANZANIA limefanya uchunguzi kwa siku kadhaa na kubaini matatizo mbalimbali yakiwamo ubadhirifu wa fedha unaofanywa na waliopewa majukumu ya kukusanya mapato.
Kwa kiasi kikubwa, kituo hicho kwa sasa kimefanywa kama mradi wa watu wachache wanaokusanya mamilioni ya fedha kila siku huku wananchi wanaokamuliwa fedha hizo, wakiwa hawana hata sehemu ya kujisitiri kwa jua ama mvua.
Katika kituo hicho, mabasi ya abiria takriban 400 hadi 650 huingia na kutoka kila siku na kila moja hutozwa ushuru wa Sh 2,000. Idadi hiyo inatofautiana kutokana na msimu wa biashara.
Pia watu wanaokadiriwa kufikia 10,000 huingia kwenye kituo hicho kila siku na kila mmoja hulipa Sh 200.
Vijana wanaosukuma matroli ya mizigo ndani ya kituo hicho ni takriban 300 ambao hutozwa kila mmoja Sh 4000 kwa siku.
Wafanyabiashara waliopanga kwenye mabanda mbalimbali, wanakadiriwa kufikia 150 na kila mwezi wanalipa Sh 100,000.
Kutokana na vyanzo hivyo vya mapato ndani ya kituo hicho, MTANZANIA lilibaini kuwa kwa kila Sh 2,000 inayopatikana kutokana na kadirio la chini la mabasi 400 yanayoingia na kutoka kituoni hapo, Sh 800,000 hukusanywa kila siku.
Ukipiga hesabu ya mwezi mi kuwa Sh milioni 24 hupatikana na Sh milioni 288 kwa mwaka, zinakusanywa.
Fedha zinazopatikana kutokana na watu wanaoingia na kutoka kwenye kituo hicho ni Sh milioni 2 kwa siku ambazo ni Sh milioni 60 kwa mwezi na Sh milioni 720 zinapatikana kwa mwaka mmoja.
Kwa upande wa kodi ya wafanyabiashara, takriban Sh milioni 15 hupatikana kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh milioni 180 kwa mwaka.
Wasukuma vitoroli ambao hulipa Sh 4,000 kila mmoja kwa siku, fedha zinazokusanywa kutoka kwao ni wastani wa Sh milioni 1.2 kwa siku ambazo kwa mwezi ni Sh milioni 36.
Gazeti hili pia lilibaini kuwa takriban magari madogo 250 huingia na kutoka kwenye kituo hicho kila siku na kila moja hulipa hadi Sh 5,000 hivyo kwa siku moja Sh milioni 1.2 ambazo ni wastani wa Sh milioni 36 kwa mwezi hupatikana.
Mbali na fedha zinazotozwa kwenye mabango ya biashara na ofisi zinazotumika na kampuni mbalimbali za mabasi kituoni hapo, zaidi ya Sh bilioni moja hukusanywa kwa mwaka kituoni hapo.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wafanyakazi wa halmashauri walisema fedha nyingi huishia kwenye mifuko ya wachache huku kiasi kidogo tu ndiyo kikipelekwa katika halmashauri.
Hali hiyo inaendelea huku sehemu kubwa ya kituo hicho ikiwa imevunjwa kwa maelezo kwamba kituo kingine kitajengwa eneo la Mbezi, lakini mpaka sasa hakuna taarifa yoyote juu ya maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kipya.

Itaendelea kesho,

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles