26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Lubuva ajibu mapigo ya Ukawa BVR

Jaji LubuvaMauli Muyenjwa na Maneno Selanyika, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, amewataka wanasiasa waache kutumia changamoto za mfumo wa kielektroniki wa uandikishaji wapigakura (Biometric Voter Registration-BVR) ili kujipatia umaarufu wa kisiasa.
Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kumuonya na kudai kamwe chama chake hakitakubaliana na vitendo vya hujuma ambavyo tayari tume hiyo imeanza dhidi ya upinzani.
Mbowe, alimtaka Jaji Lubuva asiwe adui wa demokrasia kwa kutoa uamuzi kama suala hilo ni la nyumbani kwake wakati nchi nzima iko kwenye ‘tension’ kuhusu daftari la wapigakura na mfumo wa BVR.
Akizungumza jana mjini Makambako wakati wa uzinduzi wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo wa BVR, Jaji Lubuva, alisema hoja za wanasiasa ambao wanapinga mchakato huo hazina uzito.
Alisema hata kama wangekata rufaa mahakamani, hoja zao zingetupwa kwa kukosa uzito.
“Pamoja na changamoto tulizokutana nazo katika mchakato huo, lakini tumefanya vizuri kwa kuwa zoezi hili ni zito na hakuna yeyote ambaye atafika kujiandikisha na akaachwa, wote watakaofika wataandikishwa.
“Ni vema wanasiasa waache kutumia changamoto za BVR kwa lengo la kujitafutia umaarufu, hili jambo si sawa hata kidogo,” alisema Jaji Lubuva.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipongeza kazi hiyo na kusema kuwa ilitegemewa siku ya kwanza ya uandikishaji wangeandikishwa watu 1,850 lakini NEC imefanikisha na kuandikisha watu 3,014 jambo ambalo ni la kupongezwa.
Kutokana na mafanikio hayo, aliwataka wanasiasa kuacha kauli za kuikatisha tamaa NEC, huku akiwataka kutoa ushirikiano kwani mfumo wa BVR umekuwa na mafanikio na umeshatumika katika nchi nyingi.
“Aprili 30, mwaka huu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa itapigwa kwa kutumia daftari linaloboreshwa sasa kwa mfumo huu wa BRV, na mabadiliko haya yamefanyika ili kuboresha ufanisi na kutoa haki sawa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na sio vinginevyo,” alisema Pinda.
Alisema NEC na Serikali wamejipanga vizuri katika mchakato huo, ambapo aliwaomba viongozi wa dini kutumia muda wao kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote litakapopita daftari la wapigakura.
Aliongeza kuwa vituo vya kupigia kura vimeongezeka na kufikia 40,150 ikilinganishwa na kipindi kilichopita ambapo vilikuwa 24,919.
“Kuongezeka kwa vituo hivyo kutachangia kuboresha upigaji kura katika sahemu mbalimbali, kwani kuanzia ngazi ya vitongoji, kata na vijiji vitakuwa na mashine hizi ili kupunguza msongamano na kutembea umbali mrefu ili kupiga kura,” alisema Pinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles