31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NYUMA YA PAZIA SAKATA LA WAMACHINGA MWANZA

 RAIS Dk. John Magufuli
RAIS Dk. John Magufuli

NA JOHN MADUHU, MWANZA

RAIS Dk. John Magufuli, hivi karibuni alitoa uamuzi mgumu, ambao kwa miaka mingi uliwashinda baadhi ya watangulizi wake.

Ametengua uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wa kuwaondoa wamachinga kutoka katikati ya Jiji, operesheni ambayo inadaiwa kugharimu mamilioni ya fedha.

Katika taarifa yake, Rais Dk. Magufuli alisema kuwa, aliamua kuchukua uamuzi huo kutokana na viongozi wa jiji, wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushindwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo aliyoyatoa wakati wa mkutano wa hadhara alioufanya katika viwanja vya Furahisha, katikati ya mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa, Rais Magufuli alitoa miezi mitatu kwa viongozi wa Jiji hilo, Manispaa ya Ilemela kusitisha mara moja mpango wa kuwaondoa wafanyabiashara hao katikati ya Jiji na kuhakikisha kwanza wanawatengea maeneo rafiki wamachinga hao.

Aliwataka viongozi kuketi na wafanyabiashara hao na kuondoa changamoto zilizopo katika maeneo yaliyotengwa, lakini katika hali ya kushangaza, viongozi wa Jiji pamoja na Manispaa ya Ilemela walishindwa kutekeleza.

Kabla ya Rais kuamua kusitisha operesheni ya kuwaondoa wamachinga, tulishuhudia namna wakuu wa wilaya za Ilemela, Dk. Leonard Masale na wa Nyamagana, Martha Tesha wakitoa kauli za ubabe, vitisho na kejeli dhidi ya wafanyabiashara hao.

Pia, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, kupitia vyombo vya habari alijiapiza kuwa lazima wafanyabiashara hao waondoke kwa nguvu, kwani walikuwa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa namna yoyote.

Niandikapo makala haya nilitarajia kuwa viongozi wote waliokuwa mstari wa mbele katika zoezi la kuwaondoa wangelikuwa wameachia nyadhifa zao badala ya kusubiri kutumbuliwa na Rais Dk. Magufuli.

Viongozi hao wamemwaibisha Rais, aliyewaamini na kuwateua kuwa wasaidizi wake, kuendelea kubaki katika nafasi walizonazo ni kutomtendea haki Rais Dk. Magufuli.

Viongozi hao walishindwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Rais ya kuhakikisha yanatengwa maeneo yenye mazingira rafiki kwa ajili ya wamachinga kuhamia, maana yake ni kuwa viongozi hao hawakuwa na uhalali wa kutekeleza operesheni waliyoifanya ya kuwaondoa wamachinga, hilo ni kosa la kwanza ambalo linawapotezea sifa na uhalali wa kuendelea kukalia nafasi walizonazo.

Viongozi hao wametumia fedha za walipa kodi kuendesha operesheni mfu, fedha hizo zingeliweza kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo, inadaiwa kuwa zaidi ya Sh milioni 150 zilitumika katika operesheni hiyo.

Rais Dk. Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuwataka watendaji wa serikali kuhakikisha wanabana matumizi ili fedha ambazo zingetumika kwa shughuli zisizo na tija ziweze kuokolewa na kupangiwa matumizi mengine.

Leo hii baadhi ya vituo vya afya havina dawa za kutosha kutokana na ukosefu wa fedha, kutumia Sh milioni 150 na zaidi kwa ajili ya zoezi la kuwaondoa wamachinga ni ufujaji wa fedha, ndiyo maana Gumzo la Rock City linahoji kwa mshangao, wateule hao wanasubiri nini.

Viongozi hao lengo lao lilikuwa ni kumchonganisha Mkuu wa nchi na wafanyabiashara hao, kutumia kauli mbiu ya hapa ni kazi tu iliyokuwa ikitumiwa na Dk. Magufuli wakati wa kuomba kura kuwaondoa wamachinga hao ni sawa na kumkejeli Rais.

Nilijaribu kuzungumza na baadhi ya madiwani wa Jiji la Mwanza baada ya agizo la Rais Magufuli kusitisha zoezi la kuwaondoa wamachinga katikati ya jiji, baadhi ya madiwani walinieleza waziwazi kuwa, hawakushirikishwa katika uamuzi wa kuwaondoa wamachinga hao.

Madiwani hao walisema wamechoshwa na ubabe na jeuri zinazofanywa na Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba pamoja na Mkuu wa Wilaya, Martha Tesha, walieleza kuwa viongozi hao wamejaa kiburi na dharau.

Kama madiwani ambao ndio wenye halmashauri wanalalamika kuhusu staili za viongozi wao, hii inajenga picha kuwa, viongozi wanaolalamikiwa wameshindwa kumwakilisha Rais ipasavyo katika maeneo yao.

Gumzo la Rock City linapongeza uamuzi wa Rais Dk. Magufuli wa kusitisha operesheni hiyo, huku akikemea utaratibu wa kuwatenga wananchi kwa kufuata matabaka, alisema kamwe hatakubali kuona hilo linatokea katika utawala wake.

Kuna mambo makubwa mawili ambayo yamejificha nyuma ya pazia kuhusu operesheni hiyo na nyingine ambazo zimekuwa zikifanyika mara kwa mara na kuhatarisha usalama wa wananchi kutokana na vurugu zinazotokea.

Moja, sehemu kubwa ya wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia wamekuwa wakiishi katikati ya Jiji la Mwanza, wafanyabiashara hao wamekuwa wakiendesha biashara zao katika maeneo wanayoishi, siku zote wamekuwa mstari wa mbele kushinikiza wamachinga wanaondoshwa katikati ya jiji.

Baadhi ya viongozi wetu wamekuwa watumwa wa kundi hilo, kundi hilo limekuwa likitumia nguvu kubwa kuwa karibu na viongozi, ushawishi wa kundi hilo kwa viongozi umekuwa ukisababisha mvutano wa mara kwa mara baina ya vyombo vya dola na wafanyabiashara ndogo.

Pili; baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa mstari wa mbele kuwapiga vita wamachinga kwa madai kuwa wanawaharibia biashara kutokana na kuuza bidhaa kwa bei ya chini mbele ya maduka yao.

Wafanyabiashara hao nao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ushawishi kwa viongozi ili wamachinga waondolewe, ndiyo maana kila vurugu zinapotokea wamachinga wamekuwa wakilenga kuhujumu biashara za wafanyabiashara.

Ili kukomesha vurugu na mitafaruku ya mara kwa mara kuhusu suala la wamachinga, Serikali inapaswa ijitazame upya na kujipanga ili iweze kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili.

Wamachinga tusiwachukulie kuwa ni Watanzania wa daraja la chini, hawa ni Watanzania wenzetu, ni mama zetu, ni baba zetu, dada na kaka zetu, lazima nao waishi maisha bora kama wanavyoishi Watanzania wenzao.

Kundi hili tusilichukulie kuwa ni kundi la Watanzania walioshindwa maisha, hapana, hili ni kundi muhimu, kundi hili ndilo sehemu ya uamuzi wa mustakabali wa nchi yetu, hasa inapofika wakati wa kupiga kura.

Kundi la wazito ambalo limekuwa likiwachongea wamachinga ili waondolewe mjini ni kundi ambalo miaka yote limekuwa likikwepa kujitokeza kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa nchi hii.

Kundi hilo kila uchaguzi unapokaribia limekuwa likienda nje ya nchi kwa hofu ya kuogopa kutokea vurugu na machafuko, kamwe Gumzo la Rock City halitakubali kuona Watanzania wanyonge wanabaguliwa katika nchi yao.

Rais Dk. Magufuli una vyombo vyako, nina hakika ukitaka kupata taarifa zote muhimu kuhusu mienendo ya wasaidizi wako utaweza kuzipata ndani ya muda mfupi.

Gumzo la Rock City linawakumbusha viongozi kuwa watafakari kwa kina kauli ya Ris Dk. Magufuli ya kuwataka wajitafakari na kama wameona wameshindwa waachie ngazi.

Tunamwomba Rais Dk. Magufuli azidi kuwatetea Watanzania wanyonge, yeye amekuwa kimbilio lao tangu ameingia madarakani, nina hakika atafanikiwa, Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.

  Naomba kuwasilisha.

 [email protected] 0784 642 602, 0767 642 602

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles