33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa kuvujisha mtihani kidato cha nne

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja

Na Pendo Fundisha-Mbeya

MWALIMU wa Shule ya Sekondari Hasanga, iliyopo wilayani Mbozi mkoani Songwe na wafanyabiashara wawili, wanahojiwa na vyombo vya usalama mkoani Mbeya kwa tuhuma za kuhusika na utengenezaji wa mitihani feki ya kidato cha nne.

Watuhumiwa hao, James Kapinga (36) ambaye anadaiwa kufanya kazi Shule ya Sekondari ya Hasanga pia anajitolea kufundisha Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Sangu, Baraka Mwazambe (28), mfanyabiashara na mkazi wa Tunduma na mtaalamu wa masuala ya Tehama (IT), Alex Mochi.

Watu hao kwa pamoja inadaiwa walikamatwa juzi usiku baada ya mwanafunzi mmoja ambaye jina lake na la shule vimehifadhiwa kukutwa na mtihani wa somo la Kiingereza na alipobanwa, inadaiwa aliwataja wahusika hao.

“Mwanafunzi huyu ni wa shule nyingine tena si ya Mbeya, alikutwa na mtihani feki wa somo la Kiingereza, alipohojiwa alieleza mtihani huo ulitoka Mbeya na Serikali ilipofuatilia iliwabaini wahusika ambao walikuwa wanasambaza mitihani feki,” kilisema chanzo kimoja cha habari hii.

Akizungumzia sakata hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alikiri ofisi yake kupokea taarifa juu ya uvujaji wa mitihani na walipofuatilia walibaini mitihani hiyo ni feki.

“Mbeya hakuna mitihani iliyovuja kama inavyoelezwa katika mitandao, ukweli ni kwamba suala hilo lilifuatiliwa ilibainika mitihani inayosambazwa si ile iliyochapishwa na Baraza la Mitihani la Taifa, ni feki na baadhi ya wahusika wanahojiwa na vyombo vya dola,” alisema.

Naye Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Benedict Sandy, alisema hakuna mitihani iliyovuja.

“Mitandao imekuwa ikitoa taarifa za upotoshaji eti mitihani imevuja, mitihani iliyosambaa na kukutwa na baadhi ya wanafunzi tena si wa Mkoa wa Mbeya ni feki na wahusika wanaodaiwa kuisambaza wamekamatwa.

“Nawaomba wanafunzi wazingatie yale waliyofundishwa, mitihani hiyo inakuja kwa lengo baya la kuwapotezea muda wao na mwisho wa siku kuishia kufeli, watu wanaofanya kazi hiyo wapo kimasilahi,” alisema.

MTANZANIA lilizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, ambaye alisema msemaji wa taarifa hiyo ni ofisi ya elimu mkoa.

“Hili ni suala la elimu na msemaji ni ofisa elimu mkoa, polisi hatuwezi kulisemea neno lolote, ninawashauri mumtafute ofisa elimu alitolee ufafanuzi suala hilo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles