24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mjane aliyejiweka sokoni pamoja na nyumba yake

1

Na Joseph Hiza,

SEHEMU kubwa ya mali zisizohamishika zinapowekwa sokoni hasa majengo kwa kawaida huambatana na maelezo kuhusu vitu vilivyomo.

Huhusisha vitu vya kawaida kama vile idadi ya vyumba, bafu, vyoo, ukubwa wa bustani, gereji na mengineyo kama hayo.

Lakini hii tunayoielezea hapa chini ina tofauti kidogo.

Mwanamke mmoja nchini Indonesia mapema mwaka jana, ambaye mumewe alifariki dunia akiwa anakabiliwa na matatizo ya kifedha aliamua kuiweka sokoni nyumba yake sambamba na yeye mwenyewe.

Aliamua kutoa ofa hiyo ya ziada kama kichocheo cha kuvutia wanunuzi watakaopenda kuinunua nyumba yake hiyo, kwa maana kwamba mnunuzi amuoe yeye pia.

Mama huyo mjane, Wina Lia mwenye umri wa miaka 41 anauza nyumba yake kwa pauni za Uingereza 51,000 sawa na Sh milioni 130.

Ina vyumba viwili, mabafu mawili, eneo la wazi la kuegeshea magari na bwawa la samaki ikiwa karibu na Jiji la Yogyakarta, kisiwani Java.

Tangazo alilotoa linasomeka, “Mnunuzi ambaye hawajadili bei anaweza kumuomba mmiliki amuoe,’ tangazo hilo liliongeza kuwa kuna masharti ya kufanya hivyo.

Na ijapokuwa hilo lilianza kama tangazo dogo, ofa hiyo ilisambaa mno katika mitandao ya jamii na kuvutia wengi, ambao walikuwa wakifuatilia mwisho wake.

Wakala wake Dian Purna Dirgantara aliliambia gazeti la Time kuwa tangazo lake hilo lilifanikiwa sana kutokana na simu nyingi zisizo na idadi kupigwa mfululizo.

Na amefafanua kuwa suala la kununua nyumba na kumuoa mmiliki si sharti la lazima bali hiari ya mnunuzi.

“Iwapo mtu anachotaka ni nyumba tu anaweza kuipata baada ya kukubaliana bei,’ alisema.

Wina aliuambia mtandao wa habari wa Kompass kwamba baada ya kuishi zaidi ya mwongo mmoja bila mume, anatamani sana kuwa na mwenzi mpya.

Alisema: “Dian alitoa maoni yake kuwa katika tangazo  niandike hivi; ‘Nunua nyumba na oa mmiliki pia.’ Na nilisema Sawa kwa vile natafuta mume kwa kweli.”

Sasa, haikuchukua siku nyingi baada ya tangazo hilo Wina Lia alipata mteja aliye makini, ambaye si tu alikuwa tayari kuinunua nyumba hiyo bali pia kumuoa.

Mfanyakazi wa kampuni ya umma, Redi Eko mwenye umri wa miaka 46 ndiye mteja aliyejitokeza.

Wakati akijitambulisha mwanzoni, alisema kwamba aliwahi kuoa kabla ya kutengana na mkewe na kwamba alikuwa akilea watoto wawili peke yake.

Wakati Wina akiwa na matumaini ya kumpata mwanaume huyo wa ndoto yake, akiwa katika harakati za harusi, akajitokeza mwanamke mwingine aliyedai kuwa yu mke halali bado wa mteja huyo.

Wina, alishangazwa na kushtushwa mno. “Huyu mwanamume mwongo, kamwe hakuniambia ukweli,” alikaririwa akisema.

“Ndio nilishangazwa kusoma katika vyombo vya habari kuwa alikuwa tayari na mke. Nilisikitika na kukata tamaa.”

“Alipokuja kwangu Eko alidai awali alikuwa akitafuta mke wa kusaidiana kulea watoto na kuishi pamoja. Na wakati aliposikia matatizo yangu, alijitokeza na kuahidi kunisaidia pamoja na kunioa,” alisema.

“Aliniambia kwamba atauza nyumba yake huko Lampung, Sumatra na kutumia fedha hizo kunisaidia na kuja kuishi hapa na watoto wake, ambao alidai wanapenda sana kuhamia katika jiji hili.

“Tukaanza maandalizi ya ndoa na taratibu nyingine,” alieleza, lakini kumbe ni mwanamume mwongo,” anasema.

Anayedai kuwa mke wa Redi, Endang Titin Wapriyustia, ambaye kama Wina, anajipatia kipato kwa kuendesha biashara ya saloon ya urembo, pia alieleza kushangazwa wakati aliposikia mumewe anataka kuoa mwanamke mwingine.

Endang alisema yeye na Redi walioana Machi 8, 2014 na walikuwa wakifahamiana tangu utotoni na wakaungana baada ya ndoa ya kwanza ya Redi kuvunjika na mumewe Titin kufariki dunia akimuacha na watoto watatu.

Wenzi hao hawaonani mara kwa mara kwa sababu mume anaishi Lampung, wakati mke akiishi katika mji wa katikati mwa Java wa Solo — si mbali na Yogyakarta, anakoishi Wina.

Endang alisema hatomzuia mumewe kumuoa Wina, iwapo watatalikiana.

Lakini ana matumaini kuwa Wina atafikiria upya mpango wa kuoana na Redi.

“Mwanamume huyu alinipa ahadi nyingi kabla ikiwamo kuninulia nyumba ya kifahari, gari na kunipeleka kuhiji Mecca, lakini hadi sasa sioni utekelezaji wowote,” Endang alisema.

“Tangu tuoane Machi 2014, hajawahi kunipa fedha mbali ya rupia 300,000 sawa na Sh 46,000 kwa sikukuu ya Eid al-Fitr na rupia milioni 10 sawa na Sh milioni 1.5  kwa harusi.

Suala hili limemfanya Wina aahirishe mipango yake ya ndoa ili afikirie upya cha kufanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles