30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ugonjwa wa vitiligo sasa wawashambulia watoto wa kike ukeni

Mara nyingi ugonjwa wa vitiligo hushambulia kwenye viungo
Mara nyingi ugonjwa wa vitiligo hushambulia kwenye viungo

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

NGOZI ni sehemu muhimu ya mwili ambayo ina jukumu la kuukinga mwili na viungo mbalimbali.

Ngozi ina kazi nyingi kama vile kufunika vifaa vingine vilivyo ndani ya mwili na kusaidia kuvilinda visidhurike, ni kizuizi cha vijidudu kama vile bakteria na pia huzuia mwili kupoteza maji na vimiminika vingine.

Hata hivyo ngozi inaweza kudhurika na magonjwa na wataalamu wanaeleza kwamba yako magonjwa takribani 6,000 ya ngozi ambayo humpata binadamu na mengine pia huwapata wanyama.

Vitiligo ni aina ya ugonjwa unaoshambulia ngozi na ni kati ya magonjwa yanayowakabili watu wengi ambapo husababisha ngozi kubabuka katika sehemu mbalimbali za mwili.

Ugonjwa huo hushambulia nywele, ngozi, sehemu ya kinywa, bomba la mkojo, maeneo yanyozunguka mfumo wa chakula, njia ya uke na viungo vya ndani.

Ingawa unawashambulia watu wote lakini ugonjwa huo huonekana waziwazi kwa watu wenye ngozi nyeusi na huenea polepole.

Kwa muda mrefu ugonjwa huo umekuwa ukiwakabili vijana na watu wazima lakini hivi sasa unaonekana kuwashambulia watoto wa kike.

CHANZO CHA UGONJWA

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi katika Hospitali ya Rufaa Temeke, Claud Mango, anasema ugonjwa huo ambao pia huitwa leukoderma husababishwa na ukosefu wa chembe zinazotokeza rangi ya ngozi.

“Rangi ya ngozi ya kawaida huwa inatengenezwa na chembechembe zinazojulikana kama ‘melanocyte’ ambazo mtu anazaliwa nazo, hivyo ukizikosa ngozi inapoteza rangi yake.

“Sababu zingine ni za urithi lakini maana hasa ya ugonjwa huu ni kwamba wale askari waliokabidhiwa mwili waulinde wanakuwa hawalindi badala yake wanautafuna,” anasema Dk. Mango.

Anasema ugonjwa huo hauna dalili yoyote, hausababishi maumivu na wala hauambukizwi bali mtu huanza kuona madoa na mabaka meupe kwenye ngozi.

“Ugonjwa huu hautabiriki, leo unaweza kuja na mabaka machache lakini kesho vikasambaa, unaweza kuwa nab aka upande mmoja, pande mbili au pembezoni. Mara nyingi huwa unapendelea sana kushambulia kwenye viungo kuliko sehemu zingine za mwili,” anasema.

Dk. Mango anasema pia yako baadhi ya magonjwa ambayo yana uhusiano na ugonjwa wa vitiligo na kwamba mtu mwenye moja ya magonjwa hayo akipata vitiligo huwa haishangazi sana.

Anayataja magonjwa hayo kuwa ni goita, upungufu wa damu, watu wenye vipara na pumu ya ngozi.

“Mfano ukiwa na ugonjwa wa pumu ya ngozi unaweza kukufanya upate vitiligo, ngozi inakuwa na vipele vinavyowashwa mfululizo na unawapata watu ambao kwenye koo zao kuna pumu,” anasema.

WATOTO WA KIKE

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo ugonjwa huo ulionekana kuwashambulia hasa vijana au watu wazima, hivi sasa watoto wengi wa kike wamekumbwa na ugonjwa huo huku wakishambuliwa zaidi katika sehemu za siri.

Dk. Mango anasema katika hospitali hiyo wana kliniki ya magonjwa ya ngozi mara mbili kwa wiki lakini wagonjwa wengi anaowaona sasa ni watoto wa kike.

Kulingana na daktari huyo, watoto wa kike wanaoshambuliwa na ugonjwa huo wana umri kati ya miaka mitatu hadi 10 na kwa kila siku ya kliniki amekuwa akiona watoto kati ya watatu hadi watano wenye ugonjwa huo.

“Watoto wengi wa kike ambao wana umri chini ya miaka 10 wanapata sana ugonjwa huu kwasasa, wanaletwa watoto hapa ukiwafunua tu unaona mashavu yote ya uke yamebadilika rangi yamekuwa meupe, tunashindwa kujua sababu hasa ni nini.

“Huenda unasababishwa na mambo mengi, tunajiuliza pengine wanapata uambukizo, uchafu, UTI au suala la mazingira lakini tungefanya utafiti tungeweza kujua sababu…hakuna fungu la kufanya utafiti,” anasema Dk. Mango.

MATIBABU

Daktari huyo anasema ugonjwa huo una tiba nyingi lakini haziponyeshi bali zinazuia kusambaa kwa ugonjwa.

Anasema kuna dawa za kupaka na kumeza ambazo mara nyingi huagizwa kutoka nje na kwamba wakati mwingine dawa hizo husaidia kurudisha rangi ya ngozi kwenye sehemu zilizoathiriwa.

“Kila ugonjwa una tiba lakini tatizo huja kwenye kuponyesha na sisi hatuwezi kuacha kuwatibu eti kwa sababu tumeambiwa hauponi.

“Mtu anaweza akatumia dawa kwa miezi minne na kama zile za usoni wakati mwingine zinaweza kusaidia ngozi ikabadilika,” anasema Dk. Mango.

Anasema tiba nyingine pia ni jua la asubuhi kabla ya saa nne na jua hafifu la jioni ambalo husaidia kupata mionzi inayosaidia ugonjwa huo usisambae sana.

“Ugonjwa ukiwa sehemu ambazo zinakabiliana na jua tiba hii nzuri kwa sababu kwenye jua kuna kitu fulani kinaitwa VDL hiki kinasaidia ugonjwa usisambae.

“Wagonjwa wengine huchagua matibabu yanayoondoa rangi ya ngozi kwa kuchuna ngozi yote kama sehemu kubwa itakuwa imeathirika lakini kwa hapa kwetu maadili yetu hayaruhusi kufanya hivyo,” anasema.

ATHARI

Ugonjwa wa vitiligo unaweza kumfanya mtu afadhaike hasa unapoenea usoni.

“Huu ugonjwa unaondoa haiba ya mtu hivyo anaweza akajinyanyapaa mwenyewe au akawa hajiamini, ni ugonjwa unaomfanya mtu asijikubali. Utakuta wengine wanafunika mikono au mdomo wake kutokana na ngozi kubabuka,” anasema Dk. Mango.

Josephine Andrew (37) mkazi wa Buza Dar es Salaam, ambaye amepata ugonjwa huo uliosababisha viganja vyake kubabuka ngozi anasema; “Mimi nimeamua kujifunika tu mikono yangu kwa sababu unaweza kukutana na mtu unataka kumsalimia kwa kumpa mkono anasita kuupokea, wanafikiri kwamba nina ugonjwa wa kuambukiza.

Dk. Mango anashauri mtu anapoona baka lolote ambalo si la kawaida mwilini mwake ni vizuri akafika kwa wataalamu wa magonjwa ya ngozi.

“Ni vizuri ukafika kwa wataalamu wakueleweshe na kukutofautishia kwa sababu kuna magonjwa mengine kama ya fangasi, ukoma na mengine. Hata kwenye biblia wagonjwa wengi walioandikwa sana kwamba wana ukoma walikuwa na vitiligo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles