30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi Zesco kumjadili George Lwandamina

lwandaminaNa ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

SIKU mbili baada ya kocha mkuu wa timu ya Zesco United ya nchini Zambia, George Lwandamina kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu ya Yanga, uongozi wa klabu hiyo umekuja juu ukidai kuwa bado unamtambua kocha huyo kwani ana mkataba unaotakiwa kumalizika Januari 17 mwakani.

Tamko hilo la Zesco limekuja kufuatia Lwandamina kuwasili nchini Jumapili iliyopita na kumalizana na Yanga ili kuwafundisha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hali iliyopelekea aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Hans van Pluijm kujiuzulu.

Kwa mujibu wa taarifa ya klabu ya Zesco iliyotolewa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Richard Mulenga, wanatambua kuwa Lwandamina bado ni kocha mkuu wa timu hiyo.

“Tunachotambua kwa sasa Lwandamina aliomba ruhusa kwenda kwao kuhudhuria msiba wa familia na alipewa na Meneja wetu, Mabvuto Banda, lakini kumbe amekwenda kwenye mambo yake.

“Tulikuwa tukimshawishi Lwandamina kuongeza mkataba wa kuifundisha timu, lakini alikuwa hatoi ushirikiano wa kutosha, hivyo taarifa hizi ni za ghafla kwetu kwa kuwa uongozi haukuwa na taarifa juu ya safari hiyo,” alisema Mulenga.

Katibu huyo aliongeza kuwa Lwandamina alitarajiwa kurudi Zambia kuiandaa timu kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Zambia dhidi ya Nkwabi FC jijini Lusaka, lakini mpaka wanatoa taarifa hakuwepo.

Hata hivyo, uongozi huo ulisema kama taarifa zinazomhusu kocha huyo ni za kweli, klabu hiyo inategemea Lwandamina kuwa muungwana kwa kuwapa taarifa na hatimaye kuvunja mkataba wake ingawa wanasikitishwa na utaratibu ulivyokwenda.

“Uongozi wa Zesco unazidi kumkumbusha kocha huyo kukumbuka vema vipengele vya mkataba na timu hii endapo upande mmoja utahitaji kuvunja mkataba,” alisema Mulenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles