27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa aukumbuka Uchaguzi Mkuu 2015

edward-lowassa*Aeleza ugumu wa maisha unavyowatesa Watanzania

Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ametoa tathmini ya mwaka mmoja tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu, huku akisema maisha yamezidi kuwa magumu.

Lowassa ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072,848, alitoa tathmini hiyo jana Oktoba 25 siku ambayo mwaka jana zaidi ya watu milioni 23 walipiga kura ya kuchagua Rais, wabunge na madiwani.

Katika uchaguzi huo Rais Dk. John Magufuli alitangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46

“Pamoja na mafanikio machache katika baadhi ya maeneo maisha yamezidi kuwa magumu na ajira imeendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka na kwamba elimu bure iliyoahidiwa siyo inayotekelezwa huku utumishi  wa umma umekuwa kaa la moto,” alisema Lowassa.

Alisema anasononeka kuona viongozi wanavyoshindana kuwasweka ndani madiwani na viongozi wengine wa kuchaguliwa hasa wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wabnanchi (UKAWA).

Akizungumzia kuhusu siku hiyo Lowassa alisema ilikuwa siku muhimu kwa Watanzania na kwake binafsi.

“Tarehe kama ya leo (jana) mwaka jana, ilikuwa siku muhimu sana kwa Watanzania na kwangu  binafsi. Niliwaongoza Watanzania kupiga kura nikiwa mgombea wa upinzani.

“Naamini nilileta sura na msisimko mpya katika siasa za Tanzania. Nilishirikiana na wenzangu kuionesha nchi yetu demokrasia maana yake ni nini,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Ninapogeuka nyuma kuingalia siku ile, nasikia faraja kubwa sana hasa kwa jinsi Watanzania walivyotuunga mkono na kuonesha matumaini makubwa kwetu. Ujasiri na ushapavu wa hali ya juu aliouonesha mke wangu Regina (Regina Lowassa) wakati wa kampeni, ulinipa nguvu kubwa.

“Chini ya Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe,tuliendesha kampeni za kiungwana kama tulivyoahidi. Upepo ule ulivuma kwa kasi mpaka visiwani ambako Maalim Seif (Aliyekuwa mgombea urais Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Sharif Hamad) aliporwa dhahiri ushindi,” alisema Lowassa.

“Kwa mujibu wa Tume isiyo huru ya uchaguzi, tulishindwa uchaguzi ule. Hatutaki kuendelea kuyalilia maziwa yaliyokwisha mwagika ambayo hayazoleki, lakini kile ambacho tulikisema wakati ule kwanini tunataka mabadiliko, hivi sasa kila mtu anakiona,” alisema.

Lowassa alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa imani waliyomwonyesha yeye pamoja na Ukawa.

“Kumalizika kwa uchaguzi ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwengine, kwa hiyo mapambano ndiyo kwanza yameanza. Kasi, nguvu, ari na hamasa niliyonayo ni kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” alisisitiza Lowassa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles