33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwaka mmoja Halotel wajizatiti ukuaji wa mtandao

1Na MOHAMED MHARIZO

KAMPUNI  ya simu za mkononi ya  Halotel Tanzania, ni kampuni mpya inayokuja kwa kasi na sasa imetimiza mwaka mmoja tangu ilipoanza kutoa huduma zake nchini.

Kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja, Halotel imeweza kufikia malengo yake kwa kiasi kikubwa ikiwamo kuongeza idadi ya watumiaji wa mtandao wake.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Septemba mwaka huu, ilikuwa na watumiaji wa mtandao huo wapatao milioni tatu na nusu na wanazidi kuongezeka kwa kasi.

Lakini pia, ripoti ya robo ya kwanza na ya pili ya mwaka huu ya TCRA inaonesha kuwa, Halotel imekua kwa kasi kwa upande wa ongezeko la wateja.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Tanzania, Lee Van Dai, anasema mafanikio ya kampuni hiyo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya wafanyakazi pamoja na ubunifu binafsi wa kibiashara wa kampuni hiyo.

Anasema kwa sasa  Halotel ndiyo kampuni pekee inayotoa huduma bora za mawasiliano (IT) kwa kampuni kubwa  zikiwamo CRDB, NMB, BOA, FINCA, EXIM, SNV-Southern Netherlands na Development Organization.

Kwa mujibu wa Lee, Halotel ina vifurushi mbalimbali kwa wateja wake kama vile Halo, virushi vya wanafunzi, huduma maalumu kwa waajiri wa makundi mbalimbali kama vile waajiriwa serikalini, wanajeshi, askari polisi na walimu ambapo wanapata dakika 15 za mawasiliano bure kila siku.

“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawapiku washindani wetu katika soko na ndio maana huduma zetu zimekuwa zikipokewa vizuri sokoni. Tunajivunia kuwa kati ya kampuni bora katika utoaji wa huduma za mawasiliano nchini.

“Kutokana na hali hiyo, tunaelekeza nguvu zetu zote katika kuboresha miundombinu yetu. Kwa mfano, hadi sasa tumekwisha jenga zaidi ya kilometa 20,000 za mkongo wa mawasiliano na zaidi ya vituo 2,700, kwa ajili ya kupokea mawasiliano. Tumepeleka mitambo maalumu ya kuboresha mawasiliano katika vijiji 3,000 ambavyo awali havikuwa vimeunganishwa.

“Hiyo ni hatua ya kwanza ya kuhakikisha mawasiliano yanaenea nchini Tanzania,” anasema.

Anasema wanalenga kuongeza idadi ya watumiaji kufikia milioni saba, ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017 na milioni tatu kwa watumiaji wa Halopesa.

Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo anasema huduma ya Halopesa waliyozindua ambayo imeenea sehemu kubwa nchini na ni ya haraka pia.

Anasema ili kutumia huduma hiyo, mtumiaji anatakiwa kupiga  namba *150*88#, kisha kufuata maelekezo.

“Kwa kutumia Halopesa, mteja anaweza kufanya malipo mbalimbali kama vile kutuma na kupokea fedha, kupokea au kutuma fedha kupitia benki na kulipia huduma nyingine kama luku, Dawasco, na malipo ya TV kwa Zuku, GEPF, TCU na Polisi,” anasema.

Anasema Halotel imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii. Hadi sasa kampuni  hiyo imetoa ajira za moja kwa moja zipatazo 25, 000 na 1,300 za moja kwa moja kwa Watanzania.

Anasema kampuni inaboresha miundombinu ya kijamii kama vile utoaji wa huduma ya bure ya mtandao wa intaneti kwa shule 450 zenye umeme kwa miaka mitatu ijayo.

Anasema kumekuwapo pia na ujenzi wa vyumba vya kompyuta kwa ajili ya huduma ya intaneti kwa kutumia ‘modem’ katika mikoa ya Pwani na Katavi.

Anasema pamoja na huduma wanazotoa za mawasiliano, lakini kampuni hiyo imekuwa ikisaidia jamii katika mambo mbalimbali ya kijamii, ambapo hivi karibuni Halotel imetoa Sh milioni 15 kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Kagera waliokumbwa na tetemeko la ardhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles