30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo Bandari kortini kwa rushwa ya mil. 8/-

vigogo*Asota mahabusu tangu Ijumaa na wenzake watatu

Na Kulwa Mzee – Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, ameburutwa tena mahakamani akikabiliwa na kesi mpya ya kuomba rushwa ya Dola za Marekani milioni nne (zaidi ya Sh milioni 8).

Mgawe na wenzake watatu ambao walikuwa mahabusu tangu Ijumaa, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi, aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Uhandisi TPA, Bakari Kilo, Meneja wa Manunuzi TPA, Theophil Kimaro (54) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya DB Shapriya Ltd, Kishor Shapriya.

Kishenyi alidai mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu wanadaiwa kati ya mwaka 2009 na 2012 mahali pasipojulikana, wakiwa katika nyadhifa zao, kupitia wakala wa Kampuni ya DB Shapriya Ltd waliomba rushwa ya Dola za Marekani milioni nne.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuomba kiasi hicho cha fedha kama kishawishi cha kuiwezesha kampuni hiyo kupata zabuni ya kuweka boya la kushushia mizigo (SPM) na bomba la mafuta RAS TPA, Mji Mwema.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa wa nne, Shapriya, anadaiwa kati ya mwaka 2009 na 2012 alitoa rushwa kwa Mgawe, Kilo na Kimaro, ikiwa ni kishawishi cha kupata zabuni hiyo.

Washtakiwa walipotakiwa kujibu mashtaka hayo, wote walikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Upande wa Jamhuri ulidai hauna pingamizi kwa washtakiwa kupata dhamana, isipokuwa watimize masharti watakayopewa na mahakama.

Hakimu Simba alikubali kuwapa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 500 na washtakiwa wanatakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.

Walitimiza masharti ya dhamana na kesi iliahirishwa hadi Novemba 7, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Mgawe anakabiliwa na kesi nyingine katika mahakama hiyo ambayo iko katika hatua ya kutolewa hukumu.

Katika kesi hiyo, Mgawe na wenzake wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC), bila ya kutangaza zabuni.

Januari 2013, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliwaondoa katika nyadhifa zao Mgawe na wenzake baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Mbali na Mgawe, wengine waliotimuliwa kipindi hicho ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu, Julius Mfuko, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ngamilo na Meneja Kituo cha Kupakulia Mafuta, Tumaini Massaro.

Dk. Mwakyembe alidai Mgawe alizembea na kuruhusu kuwapo kwa muda mrefu utaratibu usiofaa wa upokeaji na uondoshwaji bandarini wa mafuta machafu.

Katika tuhuma hiyo, Mgawe anadaiwa kuachia kiasi kikubwa cha mafuta safi kuibwa na kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji wa mafuta machafu bandarini kinyume na mikataba iliyopo.

Tuhuma ya pili iliyomwondoa Mgawe ni ufanisi duni ambao Dk. Mwakyembe alifafanua kuwa alishindwa kudhibiti wizi wa mizigo na mali ya mamlaka uliokithiri bandarini.

Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, pia alikiuka sheria na utaratibu. Anadaiwa kuingia mkataba na CCCC bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.

Pia anadaiwa kuongeza mishahara kwa asilimia 15 bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi, hivyo kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria.

Tuhuma zilizomng’oa Koshuma kwa mujibu wa Dk Mwakyembe ni nne, ikiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka.

Anadaiwa pia kuruhusu michakato ya zabuni bila kufuata utaratibu kwa kisingizio cha miradi mikubwa, kuwa na ufanisi duni, ambapo akiwa Mjumbe wa Bodi ya Zabuni, alishindwa kuijulisha Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi ya Umma (PPRA), kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi.

Ukiukwaji huo ulifafanuliwa kuwa ni wa kuruhusu Mamlaka kuingia mkataba wa kibiashara na CCCC bila kushirikisha Bodi ya Zabuni na kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles