28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi waua majambazi wawili, wakamata bunduki tisa

 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani

Na AMINA OMARI, LUSHOTO

JESHI la Polisi mkoani Tanga kwa kushirikiana na kitengo cha operesheni na mafunzo kutoka makao makuu ya jeshi hilo   Dar es Salaam, limewaua watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi   walipojibizana kwa risasi.

Wakati wa tukio hilo  Oktoba 18 mwaka huu  wilayani hapa,   polisi wawili walijeruhiwa kwa risasi katika   misitu ya Kitongoji cha Kitui, Kata ya Kwemshashi  wilayani Lushoto.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, alisema jana kuwa wakati wa operesheni hiyo zilikamatwa  bunduki tisa zikiwamo SMG saba, shotgun moja na rifle moja iliyoporwa na majambazi hivi karibuni katika Chuo cha Sekomu.

“Tulikamata pia risasi 425 za SMG na nyingine saba za shortgun, radio saba za mawasiliano ya upepo, bendera nne zenye maandishi ya kiarabu  na mavazi manne ya kuficha sura,” alisema Marijani.

Aliwataja majambazi waliouawa kuwa ni Murdick Abdi,   maarufu kwa jina la Osama ambaye ni mfanyabiashara pamoja na Sultan Abdallah,   mkazi wa Kiembesamaki kisiwani Zanzibar.

“Kabla majambazi hao hawajauawa, walikamatwa na kuwapeleka polisi mahali walipoficha silaha.

“Wakati wako njiani kuelekea eneo hilo, ghafla jambazi mmoja alitamka maneno ya kiarabu kama ishara ya kuwashtua wenzake ambao   walikurupuka kutoka mafichoni na   kuwashambulia polisi.

“Polisi nao walijibu mapigo na kuwaua majambazi wawili ingawa pia polisi wawili walijeruhiwa kwa risasi,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alisema operesheni hiyo ni mwendelezo wa hatua za    kukabiliana na wahalifu.

Kamanda Wakulyamba aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kukabiliana na wahalifu popote walipo mkoani hapa.

Wakati majambazi hao wakiuawa mkoani Tanga, juzi  Dar es Salaam, polisi waliwaua majambazi sita katika eneo la Mbezi kwa Yusuf, Makondeni, wilayani Kinondoni.

Majambazi hao waliuawa  walipokuwa wakijibizana kwa risasi na askari wa kikosi maalum cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha.

Pia, Oktoba 17 mwaka huu, majambazi wawili waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki   namba   MC 370BEY wakiwa na   shortgun walivamia duka eneo la Tegeta na kupora fedha na vocha za mitandao ya simu.

Wakati hayo yakiendelea, hivi karibuni majambazi yaliwaua polisi kadhaa eneo la Mbande wilayani Temeke na kupora bunduki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles