24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mkuu wa Mkoa Arusha azomewa

mrisho-gamboNa ELIYA MBONEA, ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, jana alikuwa katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto   mjini hapa.

Tukio hilo lilitokea wakati kiongozi huyo alipozungumzia mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo na kudaiwa kupotosha ukweli wa mradi huo.

Katika maelezo yake, Gambo alisema eneo la hospitali hiyo lilitolewa na familia ya Nyaga Mawalla, jambo ambalo   wananchi walilipinga wakishirikiana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema).

Hospitali hiyo itakayogharimu Sh bilioni tisa, inajengwa kwa wafadhili ambao ni Taasisi ya Maternity Afrika, Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF)  na Mbunge   Lema.

Kabla mkuu huyo wa mkoa hajazomewa, alipewa nafasi ya kuzungumza na ndipo alipoeleza jinsi familia ya Mawalla ilivyotoa eneo hilo.

Wakati akitoa kauli hiyo, Lema ambaye alikuwapo mahali hapo, alisimama na kupaza sauti akisema, “mkuu wa mkoa anapotosha ukweli wa mradi huu”.

Hatua hiyo ya Lema  kulalamika kwa sauti, iliwafanya wananchi nao  kumzoea Gambo huku baadhi yao wakimtuhumu kuingiza siasa katika shughuli za maendeleo.

Kutokana na zomeazomea hiyo,  polisi waliokuwapo mahali hapo  wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi, walilazimika kusogea eneo la meza kuu huku wengine wakimzunguka Gambo aliyekuwa akiendelea kubishana na Lema kuhusu ukweli wa mradi wa hospitali hiyo.

“Huyoo, acha kupotosha ukweli wewee, usilete siasa kwenye maendeleo, huyooooo,” zilisikika sauti za wananchi kutoka upande wa pili wa meza kuu huku Lema naye akisikika akihoji kwa nini mkuu huyo wa mkoa alikuwa akisema uongo.

Katika hotuba yake ambayo pia ilikatishwa baada ya kutokea kelele hizo, Gambo aliishukuru familia ya marehemu Mawalla kwa kile alichosema ilitoa eneo hilo na kuwatafuta wafadhili wa kujenga hospitali hiyo.

“Hili wazo lilikuwa ni la familia ya Mawalla kwa sababu  ardhi ni mali yao na walikuwa na maono ya kujenga hospitali hii.

“Kwa hiyo, Serikali itakuwa pamoja nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnafanikiwa,” alisema Gambo huku akizomewa na wananchi.

Wafadhili kutoka Ulaya waliokuwa kwenye uzinduzi huo, walijikusanya makundi na kumkumbatia Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maternity Afrika, Andrew Brown, wakimpa pole kwa kile kilichotokea.

Hata hivyo, baadhi ya wafadhili hao walianza kulia wakionyesha ni kwa kiasi gani hawakuridhishwa na mvutano kati ya mkuu wa mkoa, mbunge na wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi huo, Lema alisema mkuu huyo wa mkoa alifanya makosa kuupotosha umma kuhusu mradi huo.

“Mkuu wa mkoa alitakiwa kufika saa 4.00 asubuhi lakini hakuonekana kwa madai kwamba asingeweza kuja kama mimi nipo.

“Ilipofika saa saba kasoro bila kumuona, nikampigia simu Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi kumweleza suala hili, naye akampigia simu Katibu Mkuu Tamisemi.

“Inavyoonekana Tamisemi walimpigia simu mkuu wa mkoa ndipo akaamua kuja akiwa amechelewa.

“Kwa hiyo, kilichofanyika hapa kinaonyesha aina ya viongozi walioaminiwa na Rais John Magufuli wamsaidie kuongoza nchi.

“Wafadhili walimualika kuipa heshima Serikali, lakini hakuonekana hadi alipopewa maagizo.

“Kwa faida ya wasiofahamu ni kwamba mimi kupitia ArDF ndiyo tuliotafuta ardhi kwa marehemu Nyanga Mawalla.

“Kibaya zaidi, alipofika hapa akaagiza ratiba ibadilishwe mimi nisizungumze kwa sababu anazozijua yeye.

“Ushahidi wa ratiba hiyo ni kwamba, ilipangwa azungumze mtendaji mkuu wa Maternity Afrika, kisha mkurugenzi wa ArDF, baadaye mimi mbunge pamoja na Mawalla kutoa historia ya mradi na mwisho mkuu wa mkoa.

“Lakini, ratiba hiyo haikufuatwa na badala yake alifanya anavyojua yeye  mradi tu nisizungumze.

“Sasa, hivi unawezaje kuwalazimisha  Maternity Afrika wasinilete mimi wakati kwenye mkataba wa hili eneo mimi na ArDF ndiyo wasimamizi wa mradi?” alihoji Lema.

Mwenyekiti wa ArDF, Elifuraha Mtoi, alisema Taasisi ya ArDF kwa kushirikiana na Lema ndiyo waliofanikisha mradi huo.

“Hizi ni jitihada binafsi za ArDF kwa sababu  baada ya kupata wafadhili, tuliwaunganisha na Mawalla Trust ambao ndiyo wamiliki wa maeneo haya.

“Kwa hiyo, kilichofanywa na mkuu wa mkoa kimetufedhehesha mbele ya wafadhili,” alisema Mtoi.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Maternity Afrika (Brown), alisema fedha za ujenzi wa hospitali hiyo zitatokana na michango mbalimbali ya wafadhili na sadaka kutoka makanisani.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa ambaye pia ni mmoja wa waaanzilishi wa Taasisi ya ArDF, alimtangaza Gambo kama adui wa maendeleo mkoani Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles