24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tutegemee makubwa kutoka ATCL  yachagizwa kujiendesha kibiashara

atclNa LEONARD MANG’OHA

MAPEMA mwezi uliopita Rais Dk. John Magufuli alitimiza ahadi yake ya kununua ndege kwa ajili ya kulifufua Shirika la ndege  za serikali nchini ATCL kwa kununua ndege mbili aina Bombadier Q400.

Ndege hizo zilizotengenezwa na kampuni ya Bombadier Commercial Aircraft ya nchini Kanada zina uwezo wa kubeba abiria 76 na mizigo ya uzito wa tani moja na kilogram 600 huku zikielezwa kuwa na uwezo wa kutua hata katika viwanja visivyo na lami huku zikielezwa kutumia mafuta kidogo ukilinganisha na ndege zingine zinazotoa huduma hapa nchini.

Ujio wa ndege hizi unaweza kuwa unaonekana wazi kwa wengi kuwa ni juhudi za  kulifufua shirika hilo lililoonekana kupoteza dira katika miaka ya karibuni baada ya kile kinachoelezwa kuwa ni uongozi mbovu uliofanywa na viongozi wasio waaminifu ndani ya bodi ya ATCL.

Kutokana na ndege hizo kuwa na uwezo wa kutua katika viwanja vya vumbi ni wazi kuwa zitasaidia kutoa huduma ya usafiri wa anga katika mikoa ambayo huduma hiyo haikuwa ikipatikana hapo awali.

Ndege hizo zimenunuliwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 130  taslimu zinazoelezwa kutolewa na serikali.

Katika kuangalia faida zinazoweza kupatikana kutokana na kufufuliwa kwa ATCL kwa kununua ndege mbili kwa kutumia pesa ya serikali nilimtafuta Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha mkoani Morogoro Kampasi ya Dar es Salaam Profesa Prosper Ngowi, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi kuweza kupata ufafanuzi wake juu ya hilo.

Ngowi anasema kuifufua ATCL kutaiwezesha serikali kujipatia mapato kupitia huduma ya usafirishaji wa anga ndani na nje ya nchi.

Alisema kwa kununua moja kwa moja ndege hizo kutasaidia ATCL kujiendesha kwa faida na kuepuka gharama kubwa za kulipia ndege za kukodi ikiwa serikali ingeamua kutumia mfumo wa kukodi ndege badala ya kununua.

Profesa Ngowi anasema ikiwa serikali itaongeza ndege hizo kama ilivyoahidi kuleta ndege nyingine zitakazokuwa zikifanya safari kutoka Dar es salaam kwenda China na Marekani na maeneo mengine ya dunia kutasaidia kuinua uchumi hasa kupitia sekta ya utalii.

Anasema idadi ya watalii itaongezeka kwa sababu ndege hizo zitakuwa  ni utambulisho tosha wa taifa hivyo watalii kuwa na uhakika wa usafiri wa moja kwa moja kutoka kwao hadi nchini na bila kulazimika kupitia nchi nyingine.

Pia zitasaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa wafanyabiashara wa ndani kwa kuwawezesha kufika maeneo mbalimbali ya nchi na kwa haraka.

Kufufuliwa kwa ATCL kutakuwa na faida kwa walaji (abiria) kutokana na ndege hizo kutoa huduma kwa gharama za chini kama ilivyoelezwa na kuwezesha wafanyabiashara na watu wengine kwa sababu watakua na uhakika wa safarai zao na kwa haraka ukilinganisha na hali ilivyo sasa. Vilevile utaongeza ushindani na hivyo bei ya nauli kupungua.

Anasema ili kuhakikisha  shirika linajiendesha kibiashara wadau katika sekta husika wanapaswa kufanya uchunguzi kuhusu masuala mbalimbali kuhusu usafirishaji wa anga ili kufahamu changamoto zilizopo katika uendeshaji wa biashara hiyo.

Moja ya mambo ambayo Profesa Ngowi anaeleza kuwa yanapaswa kuangaliwa ni pamoja na sababu zilizosababisha ATCL kushindwa kufanya kazi na zaidi analiangalia suala la upatikanaji wa abiria (demand side) kuwa ni suala linalopaswa kupewa uzito unaostahili.

Hii itasaidia kufahamu kiasi cha uhitaji wa huduma ya usafiri huo ni wa kiasi gani katika maeneo ambayo ndege hizo zitakuwa zikitoa huduma na kuongeza ushawishi kwa wananchi kutumia usafiri huo ikiwa nauli zitakazotozwa zitakuwa nafuu ili kuongeza idadi ya abiria.

Kuimarika kwa ATCL kutaongeza ushindani katika usafirishaji wa anga kati ya shirika hilo na mashirika binafsi yanayotoa huduma hiyo nchini na hata kusababisha kushuka kwa nauli hata katika mashirika binafsi ikiwa ATCL watatoza nauli ya chini mashirika hayo yatalazimika kupunguza gharama za usafirishaji.

Wakati jitihada hizi zikiendelea kuchukuliwa kuiimarisha ATCL ni vema pia baadhi ya taratibu za usafirishaji kuangaliwa upya ili kuwa rafiki kwa wafanyabiashara kutoa huduma kwa gharama za kawaida ikiwa ni pamoja na tozo za viwanja zinazoelezwa kuwa kikwazo kikubwa na kusababisha mashirika mengi kutoza gharama za juu hivi sasa.

Sambamba na hilo bado ziko changamoto kadhaa katika usafiri wa anga kubwa ikiwa ni mazingira mabovu ya viwanja vya ndege nchini kutokuwa rafiki kwa ndege kutua nyakati zote za mwaka  au usiku.

Viko baadhi ya viwanja  ndege haziwezi kutua wakati wa mvua kutokana na kuwa katika hali mbaya hivyo ndege ikishindwa kutua, hii ni moja ya changamoto zinazopaswa kurekebishwa ili kuhakikisha ndege za            ATCL zinatoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Mamlaka ya usafiri wa anga TCAA kwa kushirikiana na mamlaka ya viwanja vya ndege TAA wanapaswa kuhakikisha mazingira mazuri ya viwanja na kutoa taarifa  sahihi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Hadi sasa ni viwanja 10 pekee nchini vilivyo na uwezo wa kutoa huduma kwa kiwango cha kuridhisha ikiwa ni baada ya kufanyiwa marekebisho uwanja wa ndege wa Mwanza baadhi ya viwanja hivyo ni Julius Nyerere (Dar), Kilimanjaro(Arusha, Moshi), Zanzibar, Songwe (Mbeya) Mtwara, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Mwanza na Songea.

Si rahisi kujenga viwanja vipya kwa sasa katika maeneo mengi ya nchi kutokana na ufinyu wa bajeti lakini kinachopaswa kufanyika ni kuhakikisha viwanja vilivyopo vinaboreshwa kuruhusu ndege kutua bila usumbufu.

Hapo kabla ATCL ndiyo ilikuwa mtoaji mkuu wa huduma ya usafiri wa anga katika miji mikubwa nchini kabla ya makampuni binafsi, bila shaka ujio wa mashirika hayo umeleta mabadiliko kadhaa katika sekta hivyo hivyo basi kinachopaswa kufanywa na ATCL baada ya kufufuka tena ni kujiendesha kibiashara zaidi na kuepuka kuendesha mambo  kiholela na kwa mazoea.

Mahusiano

Kwa mujibu wa Meneja Uratibu na Mawasiliano wa kampuni ya Precision, Hillary Mremi, kama alivyonukuliwa na gazeti moja la kila wiki alisema kuwa gharama za uendeshaji wa mashirika ya ndege ziko juu sio tu nchini bali duniani kote na kusema kuwa biashara ya usafiri wa ndege sio rahisi kwa sababu faida yake in ndogo na ukicheza kidogo inaathiri mtaji wako na mwendeshaji kutetereka kibiashara.

Alisema kuwa mazingira ya hapa nyumbani ni magumu kwa biashara hiyo kutokana na kodi kuwa nyingi na baadhi ya watu wamejijengea akilini kuwa usafiri huo ni wa anasa (‘luxury’) tabia ambayo anadai kuwa hata viongozi wa serikali wamechangia kuwapo kwa hulka hiyo potofu na kulundika kodi nyingi huko.

“Kwamfano ukipanda boti kwenda Zanzibar utalipa kodi shilingi 3,000/= lakini ukipanda ndege kwenda hukohuko Zanzibar kodi ni shilingi 13,000/=. Kwa hiyo unaona hata serikali wanatafsiri kuwa usafiri huu ni  kwa wale wenye uwezo tu na ni  starehe (luxury,)” alisema Mremi.

Mremi alisema kuna ulazima wa kuwa na juhudu za pamoja za kufanya mapinduzi ya sekta ya usafiri wa anga nchini kutengeneza mazingira rahisi kwa wananchi kupanda ndege.

Mtikisiko katika mashirika ya ndege hutokea mara nyingi pindi wanapojaribu kuwasikiliza wateja kuwa tiketi ni gharama kubwa, lakini mwisho wa siku inagharimu kampuni pindi wanapopunguza bei za tiketi kwa sababu gharama za uendeshaji ni kubwa.

Anasema kurudi kwa ATCL kutasaidia kutatua baadhi ya changamoto hizo kwa sababu kwa muda mrefuhakukuwa na shirika la taifa ambalo ni nembo na uwekezaji kwenye sekta ulidumaa.

Anaamini kuwepo kwa ATCL kutasaidia sana kukua kwa sekta ya usafiri wa anga kwa sababu watasaidiana pamoja kutetea mambo yanayoisibu sekta hiyo.

“Tukikaa kwa pamoja tukafanya mapinduzi katika sekta hii, serikali inaweza kusema kuna viwanja havijachangamka mfano Musoma, Simiyu, Mpanda au Songea. Tukizungumza  na serikali  na ikasema itapunguza kodi kwa kiasi hiki, na mashirika yakapunguza gharama za tiketi hivyo watu wengi wakasafiri na kuona umuhimu wa kusafiri  haraka na salama kutumia usafiri wa anga na hivyo maendeleo kupatikana haraka kama shughuli za M-pesa’” alisema.

ATCL imetangaza  nauli zake  kwa maeneo mbalimbali na zinaonesha kukosa unafuu wowote  ukifananisha na mashirika mengine na huku ikionesha kuwa gharama kwenda Kigoma ndio za juu zaidi  ingawa huko wasafiri wa DR Kongo na Burundi wanatumia dola kulipa nauli ilitegemewa wangefikiriwa vilivyo.

Taarifa ya ATCL iliyochapishwa na vyombo mbalimbali vya habari  inaonesha viwango vya nauli kwa safari za maeneo mbalimbali kuwa  ifuatavyo;  kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha ni 180,000/= na 360, 000/= kwenda na kurudi,  Dar-Mwanza 160,000/= kwenda pekee huku kwa tiketi ya kwenda na kurudi ikigharimu 320,000/=.

Safari ya kwenda  mkoani Kigoma ni shilingi 395,000/= wakati kwenda na kurudi ni 610,000/= , safari ya Dar hadi Zanzibar  123,000/= kwenda tu na kwa tiketi ya kwenda na kurudi itakuwa 246,000/= na safari ya moja kwa moja kutoka Arusha hadi Zanzibar itatozwa shilingi 249,000/=.

Wataalamu wa usafiri wanasema kuwa sera ya kutoza kwenda na kurudi kwa kuzidisha mara mbili sio sahihi kwani inafukuza wateja ila ingekuwa iwe chini kidogo ya kuwa mara mbili ilikuonesha  ubora wa kuwa mteja vnginevyo abiria wata kimbilia  sehemu nyingine kwa vile hakuna motisha ya kurudi na ndege hiyo hiyo.

Wakati ATCL wakitangaza bei hizo shirika moja la binsfsi (jina tunalihifadhi kwa sababu za kibiashara) linalotoa huduma hiyo hapa nchini, linatoza kati ya shilingi 319,045/= na 470,971/= kwa tiketi kutoka Dar es salaam kwenda Mwanza pekee huku likitoza kati ya 44700 na 603,364 kwa tiketi ya kwenda Kigoma pekee.

Bei ya tiketi katika kutoka Dar kwenda Arusha ni kati ya shilingi 200,000 na 266,000 kwa safari ya kwenda pekee wakati bei ya tiketi ya kutoka Arusha hadi Zanzibar ikifikia 527,400/= kwenda tu.

Kwa sababu ATCL wameamua kuivaa vita hii wanapaswa kutumia changamoto zilizopo kwa kuzigeuza kuwa fursa kwao ili kuongeza idadi ya abiria hasa kwa kuweka ruti za asubuhi na jioni katika mikoa kama vile Kigoma ambako licha ya kuwa na safari chache kwa wiki pia safari hizo mara nyingi huwa asubuhi au mchana tu.

Pia kuhakikisha usafiri wa kuaminikakati ya Zanzibar na Arusha ili kuruhusu watalii wanaokendwa visiwani humo na kutaka kwenda Arusha wawe na uhakika wa usafiri.

Kwa kufananisha tu Precison Air inatoza kiasi cha; Dar Mwanza … na kurudi ni… wakati Dar –Arusha/Moshi  ni sh … na kurudi ni sh …..na Dar –Songwe (Mbeya ) ni … na kurudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles