23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simba sikio la kufa

3TIMU ya soka Simba jana ilishindwa kutamba mbele ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), huku beki Nassor Masoud ‘Chollo’ akikosa penalti dakika za majeruhi.
Simba ni kama sikio la kufa lisilosikia dawa, kwani licha ya kumtimua Mzambia Patrick Phiri kwa kuonekana mzigo na kuwa na kocha mpya Msebia, Goran Kuponovic, lakini suala hilo si tiba kwa timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, wanaendelea kuchapwa tu katika ligi.
Baada ya kushinda mechi ya Nani Mtani Jembe na kutwaa Kombe la Mapinduzi, Simba sasa inaitwa bingwa wa makombe ya Bonanza kwa kuwa inashindwa kufanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni muhimu.
Mchezo wa jana ni wa pili kwa Simba kupoteza tangu kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu, ikiwa tayari imecheza mechi 11 ambapo awali ilifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye uwanja huo.
Lakini kipigo cha Simba dhidi ya Mbeya City jana ni cha kwanza kwa kocha Mserbia, Kopunovic, ambaye tangu aanze kukinoa kikosi hicho ameshinda mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam FC.
Bao la pekee la Simba lilifungwa dakika ya 24 ya mchezo, kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajibu baada ya Awadhi Juma kufanyiwa madhabi karibu na eneo la hatari na beki wa zamani wa timu hiyo, Juma Nyosso, ambaye alionywa kwa kadi ya njano.
Ajibu ambaye nyota yake ilianza kung’ara wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika visiwani Zanzibar, ameanza kuonyesha makali yake Ligi Kuu baada ya kupewa nafasi na Goran ambaye ameonekana kuwaibua chupukizi wa timu hiyo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuwatoa Danny Sserunkuma, Simon Sserunkuma na Ajibu na nafasi zao kuchukuliwa na Elius Maguli, Ibrahim Twaha na Abdi Banda, mabadiliko ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda huku Mbeya City ikimtoa mshambuliaji, Themi Felix na kumwingiza, Peter Mapunda.
Ahmad Kitonyile aliifungia timu yake bao la kusawazisha dakika ya 76, baada ya kuachia shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari lililomshinda kipa wa Simba, Peter Manyika aliyejitahidi kuokoa bila mafanikio.
Mbeya City ilifanikiwa kupata penalti katika dakika ya 88 iliyopigwa kwa umahiri na Yussuf Abdallah, baada ya mlinda mlango wa Simba kumfanyia madhambi, Raphael Alfa katika eneo la hatari akiwa katika harakati za kuokoa.
Chollo alikosa penalti dakika ya 90, ambapo shuti alilopiga liligonga mwamba na kurudi uwanjani baada ya Mkude kuchezewa rafu na Yussuf Abdallah wa Mbeya City.
Kufuatia matokeo hayo, mshambuliaji hatari wa timu hiyo ambaye ni majeruhi Mganda, Emmanuel Okwi, aliingia uwanjani huku akiwa analia kutokana na kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.
Kwa matokeo ya jana, Mbeya City imefikisha pointi 15 baada ya kushuka dimbani mara 11 sawa na Polisi Morogoro na Ruvu Shooting huku Simba ikiwa imebaki na pointi 12.
Kikosi cha Simba kiliongozwa na Peter Manyika, Ramadhan Singano ‘Messi’, Nassor Masoud ‘Chollo’, Jonas Mkude, Danny Sserunkuma/Elius Maguli, Ibrahim Ajibu/ Abdi Banda, Simon Sserunkuma/ Ibrahim Twaha, Hassan Isihaka, Awadhi Juma, Jjuuko Murshid na Mohamed Hussein ‘Shabalala’.
Mbeya City ilikuwa Richard Peter, Yusuph Abdallah, Steven Mazanda, Themi Felix/Peter Mapunda, Cosmas Foed, Raphael Alfa, Paul Nonga, Deus Kaseke, Juma Nyosso, Ahmad Kitonyile na David Burhan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles