26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi la Polisi linavyotumia nguvu nchini

340677346Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KWA miaka kadhaa sasa yamekuwapo malalamiko kuhusu matumizi ya nguvu ya Jeshi la Polisi dhidi ya raia wakiwamo waandishi wa habari na viongozi wa upinzani nchini.
Matukio hayo ni kama lile la kutisha ambako mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi aliuawa Septemba 2, mwaka 2012 kwa bomu lililorushwa na polisi mkoani Iringa.
Mwangosi aliuawa kwa bomu la kutoa machozi lililorushwa na polisi waliotaka kulizuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufungua tawi katika Kijiji cha Nyololo.
Tukio jingine ni la mwaka 2005 wakati Mwandishi Christopher Kidanka na mwenzake walipopigwa na kuharibiwa vitendea kazi vyao walipokuwa kazini kuripoti tukio la kuhamishwa kwa wakazi wa nyumba za ATCL Ukonga, Dar es Salaam.
Misukosuko kwa viongozi wa siasa
Januari 27, mwaka 2001 Jeshi la Polisi lilitumia nguvu na kusababisha mauaji ya zaidi ya wafuasi 20 wa CUF visiwani Zanzibar ambao walikuwa wakidai Tume Huru ya Uchaguzi na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Jijini Dar es Salaam, polisi waliwapiga viongozi wa CUF akiwamo Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alivunjwa mkono na kuibiwa saa na watu wanaodaiwa kuwa ni askari.
Januari 5, 2011 watu watatu jijini Arusha waliuawa kwa risasi kwa kile lichodaiwa kudhibiti maandamano yasiyokuwa na kibali.
Polisi pia waliwakamata Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilibrod Slaa na wabunge watatu wa chama hicho na kuwafungulia mashtaka.
Mwaka 2012, polisi walimkamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mkoani Dar es Salaam kwa kutumia nguvu kubwa hali iliyozua taharuki kwa wananchi.
Agosti 26 mwaka 2013, muuza magazeti mkoani Morogoro aliuawa kwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa polisi waliokuwa wakidhibiti maandamano ya Chadema.
Mwaka 2013 Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuchochea vurugu za wafanyabiashara ndogondogo ambao walikuwa wakipinga kuhamishwa na manispaa katika maeneo ya mjini.
Machi 3, mwaka 2011 zikiwa zimepita siku tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuonya kile alichokiita ajenda ovu za Chadema kutaka kuvuruga nchi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa na wabunge wawili wa chama hicho walitiwa mbaroni na polisi na kuhojiwa kwa saa kadhaa kwa madai ya kufanya mkutano wa uchochezi katika Jimbo la Maswa Mashariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles