31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

OKWI mgonjwa (1)NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

HALI ya kiafya ya mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi inaendelea vizuri na anatarajiwa kuendelea kufanya mazoezi na wachezaji wengine wa timu hiyo leo, jijini Dar es Salaam.
Okwi alipoteza fahamu baada ya kugongana na beki wa Azam, Aggrey Morris, katika mchezo wa ligi uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa.
Taarifa za awali kutoka kwa Daktari Richard Yomba wa Chama cha Madaktari wa Tiba za Michezo Tanzania (TASMA), zilisema waliamua kumkimbiza Okwi Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya kuzimia, kwani inaonekana amepigwa kipepsi kwenye shingo na kugusa mishipa ya fahamu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Daktari wa Simba, Yassin Gembe, alisema mchezaji huyo anaendelea vizuri na ataendelea na mazoezi kesho.
Gembe alisema mchezaji huyo alipofikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili juzi jioni, alifanyiwa vipimo vyote ambavyo vilionyesha kutokuwa na tatizo lolote.
“Vipimo alivyofanyiwa Okwi vimeonyesha hakuna tatizo lolote kubwa, ila ilikuwa ni mshituko alioupata uwanjani baada ya kugongana na Morris, ndiyo sababu kubwa iliyofanya apoteze fahamu,” alisema Gembe.
“Okwi alifanyiwa vipimo na kupumzishwa kwa muda, lakini tuliweza kuondoka naye usiku na sasa hali yake imerejea kama zamani,” alisema Gembe.
Kwa upande wake Okwi, alisema anamshukuru Mungu kwa kuendelea vizuri, huku akiwashukuru wale wote waliokuwa wanamtumia meseji kujua afya yake.
“Nawashukuru kwa maombi yenu na meseji zenu ambazo zilinifariji, naendelea vizuri na mapambano yanaendelea,” alisema Okwi.
Wachezaji wa timu hiyo jana walipewa mapumziko ya siku moja, ambapo leo wataendelea na mazoezi kwa ajili ya michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles