24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Clinton vs Trump: Mijadala kabla ya mdahalo

trump_and_clinton

WAGOMBEA urais wa Marekani, Hillary Clinton na Donald Trump, usiku wa kuamkia jana walikabiliana katika mdahalo wao wa kwanza kati ya mitatu ya urais.

Kabla ya mdahalo huo, homa ilikuwa imepanda mno kwa kambi zote mbili kiasi cha kuzua ‘midahalo’ isiyo rasmi.

Kila upande uliporusha dongo, upande kinzani ulijibu mapigo katika kile kilichoonekana kujihami iwapo utaonekana kushindwa katika tukio hilo lililokuwa likisubiriwa kwa mamilioni ya watu si tu Marekani, bali pia duniani.

Kambi ya Clinton kuelekea juzi ilitoa angalizo: msimruhusu Donald Trump aondoke akiwa ameongopa.

Na kambi ya Trump ilijibu mapigo, ikisema vyombo vya habari vinampendelea mgombea wa chama cha Democratic na Clinton ni roboti kwa kufanyia mazoezi mdahalo huo.

Mdahalo huo umekuja huku mchuano wa kuelekea Ikulu ya Marekani ukiwa mkali, kwa wagombea kuzidiana kidogo katika baadhi ya majimbo, baada ya awali kushuhudia Clinton akiongoza kura za maoni kwa pengo kubwa tangu kumalizika kwa mkutano mkuu wa chama chake.

Wakati wa maandalizi ya kuelekea mdahalo huo uliofanyika saa tatu usiku za huko katika Chuo Kikuu cha Hofstra, kambi zote mbili zilidai wagombea wao hawatatendewa haki.

Kwa sababu hiyo, wasaidizi wa Clinton walimtaka msimamizi wa mdahalo (moderator), Lester Holt kutoachia uzushi na ujanja ujanja wa Trump.

“Tuna wasiwasi Donald Trump anaweza kuongopa, anaweza kutiririka uongo na hilo kuachwa lipite. Halipaswi kufumbiwa macho, kwani litasababisha Hillary kutumia muda mwingi kuweka kumbukumbu sawa na hivyo kumnyima muda wa kuzungumzia vitu vya msingi,” Meneja wa kampeni wa Clinton, Robby Mook, alisema.

Aidha Mook alimtaka Holt kumkumbusha Trump pale anapoongopa, hilo halipaswi kuachwa hivi hivi.”

“Kitu ambacho kinatutia wasiwasi si msimamizi,  ambaye anaweza kuchaguliwa na tume, kwa sababu, wataonekana wanasimamia kwa haki. Kinachotusumbua akili ni uwapo wa njama za kuamua mchezo nje ya uwanja,” Meneja wa kampeni wa Trump, Kellyanne Conway, aliunguruma katika mahojiano na MSNBC, akivilenga vyombo vya habari.

Lakini baadaye Conway alionesha ukinyonga alipotetea madai ya Trump kuwa Holt hatatenda haki kwa sababu yu mwanachama wa Democrat na mfumo haumtendei haki Trump.

“Sifahamu kama Trump anafahamu alikojiandikisha Lester Holt kupiga kura,” alisema Conway, ambaye alikwenda mbali kueleza kwanini Trump aliongopa.

“Hapana hakuongopa,” Conway alisema, huku akidai uongo huo unamaanisha anajua chama alichojiandikisha Holt.”

Kabla ya mdahalo huo pia kulikuwa na mjadala juu ya umuhimu wa kuwepo au kutokuwepo msimamizi wa mdahalo.

Baada ya kutoa mapendekezo ya mdahalo bila msimamizi, Trump alikuwa tayari ameashiria kuwa hapaswi kuwa Candy Crowley. Crowley anakumbukwa kwa kile kilichoitwa kujichomeka katika mdahalo wa urais wa mwaka 2012 baina ya Rais Barack Obama na aliyekuwa mgombea wa Republican, Mitt Romney. Crowley, alifukua rekodi za nyuma za Romney, zikionesha alichoongea si kweli!

Lakini pia kambi ya Clinton inakumbukwa wakati ilipomshukia Matt Lauer, mwajiriwa wa NBC anakofanya kazi Holt. Lauer, alishambuliwa vikali na vyombo vya habari kwa kuruhusu Trump kutiririka uongo bila kumbana wakati bilionea huyo mtata alipodai hakuunga mkono vita ya Irak wakati wa jukwaa la usalama wa taifa mapema mwezi huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume isiyo na Upande ya Mdahalo wa Urais, ambayo huchagua maeneo ya mdahalo na wasimamizi wa midahalo, Janet Brown, alikuwa na haya ya kusema:

Wakati linapokuja suala la kumbana mgombea kwa kusema uongo, Brown alionya, sidhani kama ni wazo zuri kung’ang’ania msimamizi wa mdahalo aweka rekodi sawa.”

Lakini Katibu wa Habari wa kambi ya Clinton, Brian Fallon amesisitiza kutoruhusu uzushi wa Trump upite bila kushughulikiwa, akiongeza kuwa Holt hapaswi kuruhusu hilo.

“Kuna uongo mwingi, ambao Donald Trump huusema bila haya. Si kitu cha kuuacha kipite hivi hivi na kuwaaminisha wapiga kura,” ilisema.

“Kwa sasa, sote tunajua anapenda kudanganya kuhusu rekodi yake kuhusu vita ya Irak, uvamizi wa Libya, mwasisi wa vuguvugu la kibaguzi la birtherism, na kuhusu masuala mengine mengi ambayo huyatamka mara kwa mara na sote tunayajua. “

Iwapo atayasema tena hafai. Ni mwongo mkubwa, haifai kuwa na Rais mwongo, hatostahili kupewa alama,” alisema.

Lakini Meneja wa Kampeni wa zamani wa Trump, Corey Lewandowski, aliponda wazo la kuwahusisha wasimamizi katika midahalo akisema wao si wawania urais, kazi yao inabakia kuhakikisha mdahalo inaenda vyema kwa wagombea wajibu maswali.

“Kuwataka wasimamizi wambane mgombea kwa madai kaongopa ni kuwaingiza katika mdahalo wa wagombea wawili usiowahusu. Inawafanya wawe sehemu ya mdahalo,” alisema

Aidha Lewandowski na timu ya Trump wametetea kauli yao kuwa Clinton hana tofauti na roboti kutokana na kambi ya Clinton kufanya maandalizi ya kukabiliana na Trump wawili.

“Watu wanataka kuwa na amiri jeshi mkuu na Rais wa Marekani mwenye kujiamini na kuweza kuiibu maswali na si kupandikiziwa programu kichwani kupitia maandalizi yote haya ya midahalo bandia, Conway alisema, akirejea maandalizi ya kambi ya Clinton kufanyia mazoezi na kuigiza namna atakavyokabiliana na Trump

“Hatutaki uongo wa Donald Trump na vitendo vyote vya kupoteza malengo ya kile kilichowakutanisha mdahaloni. Tunatarajia atabanwa akiongopa ili kumpa muda Hillary ajikite vyema kuzungumzia mambo ya msingi,” Mook alisema.

Lakini Conway alijibu mapigo kuwa waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje hana ubinadamu huku  Lewandowski akisema Clinton hana sera na changamoto inayomkabili wakati wa mdahalo ni kufanya juu chini aonekane yu binadamu wakati sio.

Mijadala yote hiyo inaonesa hofu ya kila upande, wakati Clinton akihofia uzushi wa Trump kuaminika na kumpa Trump maksi, kambi ya Trump inahofia kitendo cha bosi wao kubanwa na msimamizi.

Silaha kubwa ya Trump tangu wakati wa mchakato wa kura za uteuzi ndani ya vyama ni kuwadondosha kwa ndani na nje ya mdahalo kwa makombora ya maneno mazito ya ukweli na uongo.

Makombora ya aina hiyo, yakiwamo ya kupoteza malengo ni silaha kubwa ya Trump, anayehesabiwa kutokuwa na uzoefu wa masuala ya kisera kama alio nao mpinzani wake.

Rudy Giuliani, meya wa zamani wa New York na msaidizi wa Trump alimshauri Trump kutojaribu kuigiza na kushindana na utaalamu wa sera wa Clinton.

“Clinton amekuwa serikalini tangu nilipokuwa mtoto. Sikumbuki lini hakuwa serikalini kwa namna moja au nyingine,” Giuliani alisema.

“Kwa sababu hiyo, ana ujuzi mwingi mkubwa kuliko Trump. Lakini naamini atafanya vyema iwapo akifanya mdahalo yeye kama yeye,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles