27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm agoma kutoa siri, Omog atamba kikosi imara

hans-van-der-pluijmADAM MKWEPU Na MASYENENE DAMIAN-DAR/SHINYANGA

KOCHA mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, amegoma kuweka wazi siri ya mabadiliko atakayofanya ndani ya kikosi hicho kabla ya kuwavaa watani wao wa jadi Simba, huku akidai kuwa watahakikisha wanashinda kwa namna yoyote.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, juzi walionja kipigo cha kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa bao 1-0, wakicheza ugenini dhidi ya Stand United katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kocha huyo raia wa Uholanzi ambaye ameipa Yanga ubingwa mara mbili mfululizo, juzi hakuwachezesha mabeki wakongwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani kwa kuhofia pambano la watani wa jadi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema hana sababu ya kuwapa presha ya pambano la jadi wachezaji wake, badala yake atafanya kila linalowezekana ili kuendeleza ushindi kama walivyofanya msimu uliopita.

“Hatuna furaha baada ya kufungwa na Stand, lakini tunahitaji maandalizi na kukiboresha kikosi kabla ya mchezo ujao kwani hakuna lisilowezekana kwenye soka ingawa mchezo utakuwa mgumu,” alisema.

Alisema mechi ijayo ni lazima washinde kwa namna yoyote kwa kuwa ni mchezo muhimu kwa upande wao, ili kuendeleza matumaini ya kutetea ubingwa wanaoshikilia kwa misimu miwili mfululizo.

Pluijm pia aliwatuliza mashabiki wa Yanga na kuahidi kuwa wachezaji watacheza kufa au kupona Jumamosi dhidi ya mahasimu wao Simba, ili kupata ushindi utakaowarejeshea furaha.

Kikosi cha Yanga kilitua visiwani Zanzibar jana mchana na kuelekea Pemba, ambako kitajichimbia kwa muda kusaka makali ya kuwaliza mahasimu wao kama walivyofanya msimu uliopita.

Kambi ya Pemba imekuwa ya mafanikio makubwa kwa Yanga hasa wanapokabiliwa na mchezo dhidi ya Simba, ambapo msimu uliopita wakitokea visiwani humo waliweza kunyakua pointi zote sita kwa Wekundu wa Msimbazi.

Wakati Yanga ikienda kujifua Pemba, kocha mkuu wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, ametamba kuwa kikosi chake kipo kamili kila idara kuwavaa watani wao wa jadi.

“Tumeanza msimu mpya na tunafanya vizuri tangu Ligi Kuu ianze, ushirikiano ndani ya timu yetu ni mzuri hivyo ni lazima kikosi kiwe imara,” alisema Omog.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles