24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mwinyi: Lowassa Mungu atakusaidia

Pg 3NA ELIYA MBONEA, MONDULI
RAIS mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, amemuomba Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), aendelee kusaidia wananchi kwani na yeye Mungu atamsaidia.
Mwinyi alitoa kauli hiyo wilayani hapa juzi kwenye Jubilee ya miaka 20 ya Sekondari ya Wasichana ya Maasae aliyoifungua Mei 27, mwaka 1995 ikiwa ni maalumu kwa wasichana wa jamii za wafugaji na waokota matunda.
Akizungumza katika jubilee hiyo, Rais mstaafu Mwinyi, alisema ni kawaida ya binadamu kufanya mema kwa ajili ya ujira lakini kwa alichokiona shuleni hapo kwa miaka 20 iliyopita ni wema usio na malipo kwa watoto wa Tanzania.
Kutokana na mabadiliko aliyoyakuta kutoka majengo mawili mwaka 1995 hadi maabara nne, maktaba moja, madarasa 12, mabweni 11 na zahanati moja, Mwinyi aliwataka watu kuiga mfano wa Lowassa na Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi.
“Lowassa endelea kusaidia katika kazi ya shule na wewe Mungu atakusaidia.
“Niwaombe wadau wengine tusiwaachie akina Lowassa na Mengi mzigo huu wa kusaidia elimu ndani ya jimbo hili na nchini kwani nao wana kazi nyingi,” alisema Mwinyi.
Katika jubilee hiyo, Mwinyi alisikitishwa na hatua za kukataa kuwasomesha watoto wa kike zinazotekelezwa na baadhi ya wazee katika jamii za kifugaji na waokota matunda.
“Hili ni jambo la kusikitisha, tumesaidiwa miaka 20, lakini bado ipo jamii inakataa kuwapa watoto wa kike nafasi ya kusoma badala yake wanawaozesha. Ni kwanini wazazi hawa hawaoni wivu watoto wengine wanapopata elimu?” alihoji Mwinyi.
Awali, Lowassa alisema wananchi wa Monduli wataendelea kumkumbuka Mwinyi kwa mambo mengi aliyowafanyia.
“Napata tabu kuzungumza kabla ya Mzee Mwinyi, lakini nitajitahidi ili aone kuwa alinifundisha kazi vizuri kwani katika utawala wake, aliniteua kuwa Waziri wa Ardhi.
“Katika utawala wake, alitusaidia kuanzisha shule hii na alitoa hekari 700 kwa ajili ya chuo kikuu, lakini pia alichangia wakati huo shilingi milioni 46 za kuanzisha Saccos ya walimu wa Monduli,” alisema Lowassa.
Aidha, Lowassa aliwapongeza pia wafadhili kutoka nchini Marekani kwa kuiwezesha shule hiyo kuendelea kutoa elimu ipasavyo.
Naye Mengi aliyewahi kuchangia Sh milioni 200 katika sekondari hiyo, alisema jubilee ya miaka 20 ni ya mafanikio makubwa.
“Hii si miaka 20 ya kawaida, ni jubilee ya mafanikio makubwa sana kwetu kwani Mungu akikupa baraka, una kila sababu ya kuwasaidia na wengine.
“Nakushukuru sana wewe Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli kwa sababu umefanya makubwa Monduli na Tanzania. Mdogo wangu hongera sana kwa kazi kubwa unayoifanya,” alisema Mengi.
Naye Askofu Solomon Masangwa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, alisema kati ya wanafunzi waliomaliza shuleni hapo kutoka jamii za wafugaji na waokota matunda wapo walimu 200.
Alisema kila mwaka shule hiyo imekuwa ikichukua watoto 60 kutoka maeneo ya wafugaji yaliyopo Babati, Longido, Ngorongoro, Monduli, Simanjiro na Kiteto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles