24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bodaboda kulipia mapato kwa leseni ya abiria

bodabodaNa ELIYA MBONEA-SIMANJIRO

WAMILIKI wa Pikipiki za kubeba abiria maarufu kama Bodaboda,  wametakiwa kuanza kujiandaa kwa mfumo wa ulipiaji mapato kupitia leseni ya usafirishaji wa abiria.

Kauli hiyo ilitolewa kwenye mafunzo ya madereva wa pikipiki yaliyofanyika juzi katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, mkoani Manyara na Mkuu wa Wilaya, Zephania Chaula.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti na Usafirishaji wa Nchi Kavu na majini (Sumatra), Chaula alisema mfumo huo utawezesha kuongeza mapato zaidi kupitia sekta hiyo ya usafirishaji wa pikipiki.

“Mapato haya yanatarajiwa kuanza kutozwa hivi karibuni na tutatoa taarifa mitaani ili pasiwepo na mmiliki wa pikipiki ya biashara atakayesema hakusikia tangazo husika,” alisema Chaula na kuongeza:

“Katika hili mnapaswa kujiandaa kwani haikwepeki nyinyi kulipia mapato kwa mfumo huu wa leseni ya usafirishaji wa abiria, Serikali inataka kujitegemea kupitia mapato ya wananchi na si kuomba misaada nje ya nchi,” alisema.

Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Manyara, Nelson Mmari, aliyataja malengo ya mafunzo hayo kuwa yalilenga kufikisha elimu kwa wamiliki wa pikipiki za biashara kuwa na lesseni ya usafirishaji itakayotolewa na halmashauri ya wilaya.

“Mmiliki wa pikipiki ya biashara yenye magurudumu mawili au matatu anatakiwa kulipia mapato kupitia leseni ya usafirishaji na endapo atakiuka au kutolipa, atatozwa faini ya Sh 50,000 mpaka Sh 100,000, kufungwa jela miezi sita au mwaka mmoja,” alisema Mmari na kuongeza:

“Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro amewaeleza vizuri kwa hiyo nitumie fursa hii kuwasisitiza zoezi hili linatarajiwa kuanza hivi karibuni wilayani hapa,” alisema.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Manyara, Mary Kipesha, aliwahimiza wamiliki hao wa pikipiki kuanza kulipia mapato hayo ili kuepuka kukamatwa na kujisababishia usumbufu.

Nao baadhi ya wamiliki wa pikipiki waliohudhuria mafunzo hayo, waliiomba Serikali kuwapatia muda wa kulipia mapato hayo kwa leseni ya usafirishaji kabla ya kuanza kuwakamata na kuwatoza faini..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles