30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake 270 wafariki kwa uzazi

pregnancyphoto

Na Walter Mguluchuma, Katavi

ZAIDI ya Wanawake 270 wamefariki dunia mkoani  hapa katika kipindi cha mwaka  2015/16, kutokana na vifo vinavyotokana na uzazi.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Katavi, Dk. Obeid Mahenge, katika tamasha la vijana lililoandaliwa na Shirika la Marie  Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa lengo la kutoa elimu kuhusu uzazi wa mpango katika Manispaa ya Mpanda.

Alisema matumizi ya njia za uzazi wa mpango  mkoani Katavi kwa mwaka jana ilikuwa ni asilimia  41.1 tu kiwango ambacho ni cha chini kikilinganishwa na kiwango cha taifa cha asilimia 60.

“Aidha imani potofu na taarifa zisizo sahihi kuhusu  uzazi wa mpango zimesababisha wanawake wengi  kuwa waoga wa kutumia njia hizi na kuishia kushika  mimba zisizotarajiwa.

“Wanawake wana haki ya kutumia njia ya uzazi wa  mpango kwa ajili ya afya zao na familia zao kwa ujumla hivyo wanaume mnatakiwa kuwa bega kwa  bega na wake zenu kwani mwisho wa siku   mtafaidika wote kwa kuwa na familia yenye afya  bora,” alisema.

Mratibu wa Marie  Stopes Tanzania, Kanda ya  Nyanda za Juu Kusini, Noelia  Mbeyela alisema  wanawake wengi nchini wamekuwa wakipata  mimba za utotoni jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Alisema kitendo hicho husababisha kupoteza maisha  wakati wa kujifungua na kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), kutokana na kutojua kujikinga   na maambukizi hayo.

“Lakini pia, ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya uzazi wa mpango ni mdogo ni wanawake pekee  wamekuwa wakiifuata lakini bila ushiriki wa wanaume ni kazi bure.

“Athari ya kuzaa katika umri mdogo ni kwamba msichana anachukua jukumu la kuanza kulea familia  wakati hajafikia umri wa kutunza familia na matokeo yake imekuwa ikiathiri uchumi wa nchi kwa kuwa  na wategemezi wengi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles