25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Atokwa haja ndogo mahakamani baada ya kuhukumiwa miaka 40 jela

jail

Na WALTER MGULUCHUMA-KATAVI

MSHTAKIWA wa kwanza, Nzira Luhemeja (42), alitokwa na haja ndogo mahakamani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 40 jela kwa kukutwa na nyama ya Kiboko kilo 70 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Tukio hilo lilitokea juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani  Katavi, ambapo  Hakimu Odira  Amwol alimhukumu pia Vicenti Makelele (32) katika kesi moja iliyowakabili wakazi hao wa Kijiji  cha  Mwamkulu wilayani humo.

Hakimu Amwol alisema anawatia hatiani washtakiwa hao baada ya kuridhika na  ushahidi uliotolewa na upande wa  mashtaka  uliokuwa unaongozwa na Mwendesha  mashtaka wa Tanapa, Elieza Chitalya, ambao ulikuwa na mashahidi wanne huku washtakiwa  wakijitetea wenyewe.

Wakati akisoma hukumu hiyo, Mahakama  ililazimika  kusimama kwa dakika 10 baada  ya mshtakiwa wa kwanza   Luhemeja kutoa haja ndogo huku jasho likimtiririka.

Polisi walimwondoa kizimbani mshtakiwa huyo na kumpeleka chooni na baadaye kesi iliendelea.

Awali katika kesi hiyo, mwendesha mashtaka alidai kuwa washitakiwa walikamatwa na askari wa wanyamapori waliokuwa doria Julai 21 mwaka huu, katika eneo  la Mto Katuma ndani ya Hifadhi ya  Taifa ya Katavi wakiwa na nyama hiyo  yenye uzito wa kilo 70, yenye thamani ya Sh milioni tatu.

Katika utetezi wao, mshtakiwa wa  kwanza, Luhameja alikana kukamatwa  na nyara hizo za Serikali na kudai kuwa  yeye alikamatwa wakati akiwa  njiani anakwenda kuoga katika mto  Mafunsi nje ya Hifadhi ya Katavi.

Mshtakiwa wa pili, alidai kuwa  hakukamatwa na nyama hiyo ya  Kiboko  bali askari wa Tanapa walimkamata  wakati akiwa njiani kwenda kuvua  samaki Mto Mafunsi.

Kabla ya hukumu kutolewa, hakimu aliwapa washtakiwa nafasi ya kujitetea.

Katika ombi lake, mshitakiwa wa kwanza aliomba mahakama imwachie  huru kwani hakutenda kosa hilo bali   alisingiziwa na askari wa  Tanapa, kwani hata majirani zake wanajua hana tabia hiyo.

Kwa upande wake, mshtakiwa wa pili aliiomba mahakama isimpe adhabu ya  kifungo, bali impe adhabu ya kulipa  faini kwani ana wategemezi wengi akiwamo mzazi wake ambaye ni mzee sana.

Katika hukumu hiyo, washtakiwa wote wawili walihukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles