27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

JK atengwa kura ya maoni

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

EVANS MAGEGE NA VERONICA ROMWALD,

RAIS Jakaya Kikwete sasa ametengwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika matamanio yake ya kutaka Katiba mpya ya Tanzania ipatikane kabla ya kumalizika kwa mwaka 2015.

Pamoja na Ukawa, kundi jingine lililoonyesha kujitenga naye katika matamanio yake hayo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho kimeitaka Tume ya Uchaguzi kuahirisha zoezi la upigaji kura ya maoni hadi pale daftari la wapiga kura litakapokamilika.

Viongozi wa Ukawa jana waliitisha mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) na kutangaza kuwa wanachama na mashabiki wake hawatashiriki upigaji wa kura ya maoni ya kupitisha Katiba Mpya unaotarajiwa kufanyika Aprili 30.

Katika tangazo lao hilo, walisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa mchakato uliotumika kufikia upigaji wa kura ya maoni ni batili.

Akitoa tangazo hilo kwa niaba ya viongozi wenzake wa Ukawa, Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wana Ukawa wataungana na wananchi wote wanaopinga mchakato huo kuhakikisha Katiba Mpya haipiti.

Alisema katika mkutano wa viongozi wa Ukawa uliofanyika wiki hii Dar es Salaam, waliafikiana kuendelea na msimamo wa kususia mchakato mzima wa uandikaji wa Katiba mpya kwa sababu haufuati matakwa ya wananchi.

“Ukawa hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya na tunawaomba Watanzania waungane nasi katika msimamo huu wa kupinga mchakato batili unaofanywa na CCM,” alisema Profesa Lipumba.

Aidha, Prof. Lipumba alisema mwenendo wa uandikishaji wa daftari la wapigakura hauridhishi kwa sababu wananchi wa Zanzibar wanakabiliwa na hatari ya kufanyiwa uamuzi na wenzao wa Tanzania Bara wakati wa upigaji kura ya maoni.

Alisema visiwa vya Zanzibar na mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kupangwa mwisho katika uandikishaji huo kutawachanganya wananchi wengi na huo unaweza kuwa mkakati wa CCM wa kupenyeza wananchi wa Tanzania Bara kupiga kura ya maoni upande wa Zanzibar.

Maelezo hayo Prof. Lipumba yaliungwa mkono Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Dk. Emanuel Makaidi, ambaye alisema mchakato wa upigaji kura ya maoni umeanza kufanyiwa kazi na CCM.

Alisema tayari baadhi ya wananchi wa Tanzania Bara wameanza kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya kujiandikisha.

Makaidi alimshambulia kwa maneno makali Rais Jakaya Kikwete kwa kueleza kuwa ana tabia ya ukigeugeu kwenye uamuzi wa msingi na kwenda mbali kwa kumfananisha na kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hayati Mobutu Sese Seko.

“Sijawahi kuona rais kigeugeu kama huyu na hata nikimlinganisha na Mobutu Sese Seko naona yeye ni zaidi yake. Tumekutana kwenye jukwaa la vyama vya siasa na tukakubaliana asitishe mchakato, lakini tulipoachana mwenzetu akatugeuka.
“Sasa tunawaomba wananchi watuunge mkono katika msimamo huu wa kutokuipigia kura Katiba Mpya,” alisema Dk. Makaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, alisema Ukawa umechukua uamuzi wa kujitenga ili kupisha kile alichokiita zoezi haramu linaloendeshwa kwa ajili ya kupata Katiba haramu ambayo haijaridhiwa na wananchi.

Mbowe aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Ukawa za kususia upigaji kura ya maoni na kuonya kuwa endapo Katiba mpya itapitishwa na wananchi, nchi inaweza kuingia kwenye machafuko.

Aliilaumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwaandikisha wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura bila kuwaelimisha.

“NEC wanafanya kazi hii bila kujifahamu, kwani hata baadhi ya makamishina wake hawajui mfumo wote wa teknolojia ya BVR. Sisi wanasiasa hatujaelimishwa mfumo huo umetengenezwa kwa programu ipi, nasema hivyo kwa sababu hata wakati wa uchaguzi mkuu mawakala wetu watakuwapo kituoni kama picha kwa kuwa hawafahamu mambo ya Teknolojia ya Mawasiliano ya aina hiyo,” alisema Mbowe.

Wakati Ukawa ikitangaza msimamo wake huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nacho kimeitaka Tume Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha upigaji kura ya maoni hadi pale daftari la wapiga kura litakapokamilika.

Mkurugenzi wa LHRC, Hellen Kijo Bisimba, aliyasema hayo mbele ya waandishi wa habari jana, alipokuwa akizungumzia changamoto zinazoikabili NEC kufanikisha uandikishaji wapigakura kwenye daftari hilo.

Alisema kazi iliyo mbele ya NEC ni ngumu na kwamba tume hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni muda, uteuzi wa maofisa wanaosimamia kura ya maoni, vituo vya upigaji kura na usajili wa kamati.

Changamoto nyingine alizozitaja ni utangazaji wa matokeo, pingamizi la matokeo, ulipaji wa gharama za awali za ushauri, upigaji kura kwa walio nje ya vituo pamoja na ukataji wa rufaa.

Alisema changamoto hizo zinatokana na upungufu ulioko kwenye Sheria ya Kura ya Maoni iliyopitishwa na Bunge mwaka 2013 na kurekebishwa 2014, ambayo ndiyo itakayotumika Aprili 31, wakati wa upigaji kura.

Bisimba alisema ndani ya sheria hiyo, kifungu 34 (2) cha sheria hiyo kimetoa fursa kwa kura za Wazanzibari watakaopiga wakiwa upande wa Bara kuhesabika kama zimepigwa Zanzibar.

Alisema kifungu hicho kimewekwa kwa lengo la kulazimisha kutimia kwa asilimia 50 ya upande wa Zanzibar kutokana na kuwapo kwa viashiria kuwa Katiba mpya itakataliwa na Wazanzibari.

“Tuna hoja kwamba kama kura za Wazanzibari watakaopiga upande wa huku Bara zitahesabika kama zimepigwa Zanzibar, je, kura za wa Bara watakaopiga wakiwa Zanzibar zitahesabika upande wa Bara au wa Zanzibar?,” alihoji.

Alisema sheria hiyo inaipa ruhusa Tume kupanga siku nyingine kwa ajili ya kurudiwa kwa upigaji kura ndani ya siku 60 endapo kura ya NDIYO itakuwa pungufu ya asilimia 50 ya jumla ya kura zote halali kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 35 (3).

“Kifungu hiki kimetumia neno ‘inaweza’ badala ya ‘italazimika’, hivyo kimeipa uhuru Tume kutekeleza agizo hilo, kwa hiyo hiki ni kitanzi kwa wananchi, ikizingatiwa Katiba pendekezwa ina upungufu mwingi,” alisema.

Alisema upungufu ulioonekana kwenye sheria hiyo unaonyesha haja ya sheria nzima kurejeshwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles