24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wa Escrow warudi kwa kasi

Mtzd Jumanne template.indd*Zitto, Profesa Semboja watoa neno kwa JPM

*Profesa Muhongo arusha mpira kwa Tanesco

Na WANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MOTO wa sakata la mgogoro wa kisheria kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kupitia Tegeta Escrow umerudi kwa kasi.

Hali hiyo imekuja siku chache baada ya Tanesco kutakiwa kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.4 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 320.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi uliotolewa wiki iliyopita na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID),  kutoa hukumu ya kulipwa kwa kiasi hicho cha fedha  ambacho kinajumuisha na riba ya deni la tozo ya uwekezaji.

Uamuzi huo umetolewa miaka mitatu tangu Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Dola za Marekani milioni 200 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 300 kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Fedha hizo zilitolewa na kwenda kwa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) kwenda kwa mmiliki wake, Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini.

Zitto aja juu

Kutokana na hali hiyo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameibuka na kuhoji hatua ya Rais Dk. John Magufuli, kutofanyia kazi suala la IPTL ambapo alidai matapeli wamekuwa wakiendelea kuitia hasara nchi.

Alisema kutokana na hali hiyo Mahakama ya ICSID kuamua Benki ya Standard Chartered kulipwa zaidi ya Sh bilioni 300 pamoja na riba itaiifanya Tanesco kuingia hasara kwa kile alichokiita wizi wa fedha za Tegeta Escrow, huku Rais Magufuli akishindwa kuchukua hatua.

“Kwa nini Rais Magufuli hafanyii kazi suala la IPTL? matapeli hawa wataendelea kuipa hasara nchi yetu mpaka lini? sasa Mahakama ya ICSID imeamua kuwa Benki ya Standard Chartered ilipwe Shilingi bilioni 300 na riba. Tanesco wanaingia hasara hii kwa sababu ya wizi wa fedha za Tegeta Escrow.

“Tanzania hapo ni hasara tupu mmelipa matapeli fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, mmewapa mtambo wa kuzalisha umeme matapeli hao na mnaendelea kuwalipa Capacity Charges mpaka sasa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo mbunge huyo alimwomba Rais Dk. Magufuli , achukue hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani watu wote waliohusika na kuitia nchi hasara katika sakata la Tegeta Escrow.

Pamoja na hali hiyo alimshauri kuitwaa mitambo ya IPTL kisheria na kuimilikisha kwa Tanesco sambamba na kumkamata Harbinder Singh Seth na wafuasi wake wote na kuwafikisha mahakamani.

“Benki iliyotumika kupitisha fedha za Tegeta Escrow ndio ilipe hilo deni tunalotakiwa kulipa. Rais aamue kusimama na Watanzania sasa,” alisema Zitto.

WAZIRI WA NISHATI

MTANZANIA lilimtafuta Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ili kupata ufafanuzi wa uamuzi huo na namna Serikali ilivyoupokea, lakini simu yake iliita bila kupokewa.

Hata hivyo baada ya kutumiwa ujumbe mfupi, Profesa Muhongo alijibu kwa kusema. “Waulize Tanesco hiyo ni kesi yao,” alisema.

Awali Kaimu Msemaji wa Wizara hiyo, Asteria Muhozya, alipotafutwa naye alisema suala hilo linawahusu Tanesco wenyewe hivyo wizara haina jambo lolote la kuzungumzia.

“Wizara haiwezi kuzungumzia lolote kuhusu hukumu hiyo, suala hilo linawahusu Tanesco hivyo wanaotakiwa kujibu swali lolote ni Tanesco wenyewe, kwa hiyo siwezi kuzungumza lolote,” alisema Muhozya.

PROFESA SEMBOJA

Mchambuzi wa masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia aliwahi kuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Tanesco, Profesa Haji Semboja alishauri wanasheria kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ili kulinusuru Taifa.

“Kama tunavyojua kosa lilishafanyika huko nyuma, Serikali ilingizwa mkenge na baadhi ya wajanja wachache ambao walijipatia na kugawana fedha cha muhimu tutafute suluhisho kunusuru hasara hiyo kubwa.

“Tanzania tuna wanasheria wazuri sana ambao wakikaa kujadiliana na kisha kukata rufaa naamini tutashinda tu kesi hiyo,”alisema Profesa Semboja.

Alisema uamuzi uliotolewa na baraza hilo unatokana na uendeshaji mbaya wa kesi hiyo na mifumo isiyo mizuri ya zamani.

“Lakini sasa hivi mambo mengi yamebadilika hivyo Watanzania tukubaliane  kwanza kuwa tatizo tayari limetokea na kwa sasa juhudi zielekezwe kwenye kukata rufaa ya shauri hilo,” alisema.

GAVANA NDULU

Kwa kuwa akaunti hiyo ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), gazeti hili lilimtafuta Gavana wa benki hiyo Profesa Benno Ndulu ili kujua hatima ya fedha hizo, alimtaka mwandishi kuwatafuta Tanesco ambao ndiyo wahusika.

“Akaunti gani unaiulizia…. Kesi yenyewe unaijua? pata taarifa kwanza Tanesco, uliza Tanesco juu ya kesi yenyewe,” alijibu gavana Ndulu katika ujumbe wake mfupi kwa njia ya simu.

Gazeti hili lilipowatafuta viongozi wa Tanesco ili kuzungumzia suala hilo, mmoja wa viongozi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema wanaohusika kuzungumzia suala hilo wako mkoani Kagera.

“Mkurugenzi (Felchesmi Mramba) pamoja na timu ya viongoz wote wapo mkoani Kagera na wamekwenda kukagua athari za tetemeko mimi siwezi kusema chochote kwa sasa,” alisema.

Mramba alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni.

Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa inawakilishwa na mawakili wa kampuni za nchi za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax Law Partners.

Inaelezwa kuwa Agosti 2005, benki ya SCB-HK ilinunua kwa bei yapunguzo ya dola za Marekani 76.1 kutoka Benki ya Malaysia ya Danaharta baada ya kushindwa kurejesha deni la muda mrefu kutoka IPTL.

Inaelezwa kuwa bei halisi ya deni hilo ilikuwa ni dola milioni 101.7 kwa mujibu wa ushahidi uliopo ambapo IPTL ilikopa dola milioni 100 mwaka 1998 kutoka kwa ubia wa mabenki ya Malaysia ili kujenga mtambo wa kufua umeme wa megawati 100 wa Tegeta.

Chini ya makubaliano hayo SCB-HK ilipewa kandarasi kadhaa ikiwemo haki ya kulipwa deni la 1997, ambapo mkataba wa utekelezaji na hatia ya makubaliano ya dhamana iliyosainiwa na kati ya IPTL na Serikali.

Awali Tanesco iliipeleka IPTL kwenye baraza hilo la usuluhishi la kimataifa baada ya shirika hilo kubaini lilikuwa likilipishwa kiwango kikubwa kuliko tozo ya uwekezaji na bei ya umeme.

Novemba 28 mwaka  2014, Bunge la 10 lilitoa maazimio manane kuhusu sakata hilo huku Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira  wa (VIP), aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda Pan African Power Solutions Ltd (PAP) na VIP.

Mbali na hilo Bunge pia liliazimia mawaziri wa wakati huo wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa kati huo, Eliachim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

Kutokana na maazimio hayo mawaziri hao walipoteza nyadhifa zao, huku Profesa Muhongo akijiuzulu wakati Tibaijuka uteuzi wake ukifutwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles