27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM apongeza Mbowe kuhamishwa

mbowe_bunge*Awapa ofa wananchi kukaa bure nyumba za Serikali

Na JONAS MUSHI

-DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litoe nje vitu vya mmiliki wa Mbowe Hotels Limited, Freeman Mbowe kwa kile kilichoelezwa kushindwa kulipa kodi ya pango iliyofikia Sh bilioni 1.172 , Rais Dk. John Magufuli amempongeza Mkurugenzi wa Shirika hilo, Nehemia Mchechu kwa hatua hiyo.

Pamoja na hali hiyo ametoa siku saba kufukuzwa kwa wapangaji wote wa NHC watakaoshindwa kulipa kodi ya pango, zikiwemo wizara, taasisi za Serikali, watu binafsi na watumishi wa umma.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota, Rais Dk. Magufuli,  alisema hatua zinazochukuliwa na Mchechu zitasaidia upatikanaji wa fedha za kuwekeza kwenye miradi mipya.

“Nakupongeza kwa hatua unazoendelea kuchukua. Wale wapangaji wote ni lazima walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo (jana) wapangaji wote wa Serikali, Wizara ya Ujenzi,  wizara gani kule ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni yao,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Wasipolipa endelea kuwatoa nje kama ulivyomtoa yule jamaa (Mbowe),” alisema na kusababisha watu kushangilia huku wakiangua vicheko.

“Endelea hivyo hivyo usiogope kumtoa nje mtu yeyote. Awe amepangishwa ni wa CCM mtoe nje, awe ni wa Ukawa mtoe nje, awe mtumishi wa Serikali mtoe nje, awe mtumishi huyo ni waziri mtoe nje, awe ni Rais mtoe nje,” alisema Rais Magufuli.

Alisema anashangaa kuona watumishi wa Serikali wakishindwa kulipa madeni ya kodi za pango wakati kila siku wanaomba safari za nje huku wakilipana posho.

“Ukipanga na ukashindwa kulipa kodi jiandae kuondoka. Nataka uendelee kuwatoa na nakueleza kweli Nehemia sitanii ‘take it from me and I am very serious’ (nisikilize mimi sifanyi mzaha) ” alisisitiza.

Alisema madeni hayo yangekusanywa yangelisaidia shirika hilo kuwekeza katika maeneo kama la Magomeni Kota ambalo limekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.

“Inawezekana ungekuwa na hizo fedha ungeshajenga katika eneo hili kuliko kuanza kumtafuta mwekezaji kwa ujanjaujanja. Haiwezekani eneo kama hili (Magomeni Kota) la ekari 33 unazitoa hivi hivi na ni mali ya Serikali,

“Afadhali umtoe mke wako umpe mzaramo mtani wangu akae naye,” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakiangua kicheko.

Alimsisitizia Mchechu kuharakisha kuzitoa wizara zinazodaiwa kwenye majengo yake ili ziharakishe kwenda kujenga Dodoma yaliko makao makuu ya nchi.

Awali Rais Magufuli,  alisema alibaini ukweli kuhusu eneo hilo kwamba lilitaka kuuzwa kwa mwekezaji kinyemela na kuwaacha bila kitu wakazi hao.

Ujenzi kuanza ndani ya miezi miwili

Rais Dk. Magufuli alitumia mkutano huo kuwaomba radhi wakazi 644 wa kaya zilizobomolewa katika eneo hilo na kutelekezwa bila kutimiziwa makubaliano yao, huku akiwaahidi kuanza kwa ujenzi wa makazi yao ndani ya miezi miwili kutoka sasa.

“Kwa niaba ya Serikali nawapa pole na nawaombeni radhi sana nataka niwahakikishie hayatatokea tena kama kulia mmelia sana na hamtalia tena.

“Serikali tulifanya mchakato wa kisheria wakulirudisha eneo hili chini ya Serikali na nimechukua maeneo yote ya aina hii ili madhambi na makosa yaliyotokea hapa yasitokee tena.

“Eneo hili hakuna wakuligusa bila idhini yangu na ndani ya miezi miwili nitaanza kujenga majengo katika eneo hili na majengo ya kwanza yatakuwa ya kuwapangisha wakazi 644,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ndani ya mwezi mmoja zitatolewa fedha za mradi huo na kwamba anataka ukamilike ndani ya mwaka mmoja ili wakazi hao wapangishwe.

“Nataka kandarasi atakayepewa hii kazi aifanye kwa kasi ndani ya mwaka mmoja yawe yamekamilika,” alisema Rais Magufuli huku akimtolea mfano mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga majengo 6 ya ghorofa nne ya vyumba vya kulala wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kipindi cha miezi sita,” alisema.

Wakazi kukaa bure

Kutokana na hali hiyo alitoa ofa kwa wakazi hao na kusema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano waitaishi bure kwani kwa muda wote tangu nyumba hizo zilipobomolewa mwaka 2012 walikuwa wakihangaika.

Rais Magufuli alisema wakazi hao walisumbuliwa kwa miaka mitano tangu nyumba hizo zibomolewe mwaka 2012 na zitakapokamilika watapangishiwa kwa miaka mitano bila kulipa kodi.

Alisema katika kipindi hicho cha miaka mitano Serikali itaanda mpango wa kuwauzia kwa bei nafuu wapangaji watakaotaka kununua nyumba hizo.

“Nimeguswa na mateso mliyoyapata na sisi Serikali tumejipanga na namwomba Mungu kama nitakuwa hai niwakabidhi hati za nyumba hizo mimi mwenyewe.

“Hii Serikali ilikuwa imefika mahali ambapo mambo yanaenda ovyo ovyo unakuta Beach (fukwe)  imeuzwa sasa sijui watu wataogelea wapi na walibakisha kuuza Ikulu tu,” alisema.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, alisema kwa kiasi kikubwa Rais amepotoshwa kuhusu uuzwaji wa eneo hilo.

Alisema ukweli wa eneo hilo ni kwamba lilishapata mwekezaji aliyemtaja kwa jina la Blue Marine na kwamba tangu mwaka 2014 nyaraka zake zilikuwa TAMISEMI zikisubiri kuidhinishwa kuanza ujenzi.

“Rais amepotoshwa na watendaji wake kwa asilimia 90 ambao wamekuwa wakitaka eneo hili kwa manufaa yao, lakini ukweli ni kwamba mwekezaji alikuwa anasubiri kusainiwa kwa nyaraka aanze ujenzi hata kesho,” alisema Jacob.

Hata hivyo alikiri kuwa hawana nguvu ya kushindana na Rais kwani hati za eneo hilo tayari zipo chini yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles