24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Almanusura Ukuta

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

* Viongozi wa dini, Mama Maria Nyerere, wahariri wahusika,

* Lowassa afichua siri yake na JPM

 VIONGOZI wa dini, mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere   na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, zimetumika kusimamisha maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) yaliyopangwa kuanza leo.

Maandamano hayo yaliyokuwa yameandaliwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yalilenga kupinga kauli ya Rais Dk. John Magufuli aliyepiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.

Taarifa ya kusimamishwa  maandamano hayo ilitolewa   Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipozungumza na waandishi wa habari.

Mbowe alisema  maandamano hayakusimamishwa  kwa sababu ya kuliogopa Jeshi la Polisi bali ni kutokana na ushauri uliotolewa na watu mbalimbali.

“Tumefikia uamuzi huu baada ya kukutana na kuombwa na viongozi mbalimbali wa roho pamoja na taasisi nyingine, zikituomba tuahirishe operesheni Ukuta kwa wiki mbili au tatu.

“Viongozi hao walituahidi kukutana na Rais Magufuli   kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa siasa uliopo nchini.

“Siku 30 tulizoongeza tumewaambia viongozi wetu wa dini kuwa tumeziongeza kwa sababu tunawaheshimu na hatukuwa na nia ya kumwaga damu.

“Hata Kamati Kuu ya chama chetu nayo imepokea kwa heshima ushauri wa viongozi hao wa roho wanaolinda amani ya nchi yetu.

“Pamoja na makubaliano tuliyofikia na viongozi hao wa dini, kama jitihada zao hazitazaa matunda katika kipindi hicho, mikutano na maandamano hayo ya amani yatafanyika Oktoba mosi mwaka huu,” alisema Mbowe.

Mbali na Mama Maria Nyerere na viongozi hao wa dini, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alizitaja taasisi nyingine zilizowashawishi kusimamisha maandamano yao kuwa ni   Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Nyingine ni  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)  na Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA).

“Kutokana na uzito wa suala lenyewe, Mama Maria Nyerere hivi karibuni alifanya juhudi kubwa ambako alikutana na aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa na Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama chetu, Edward Lowassa na akamuomba tuahirishe maandamano yetu.

“Kwa hiyo, tunawaomba viongozi na wanachama wetu nchi nzima, waendelee na maandalizi mbalimbali kwa ajili ya Ukuta katika maeneo yao kwa kuwa hakuna atakayekuwa salama kama mfumo wa vyama vingi utaendelea kukandamizwa.

“Mimi ni miongoni mwa watu ambao walitamani kesho (leo) tuingie barabarani, lakini lengo letu ni kupata watu wengi wanaotuunga mkono katika kusaka suluhu.

“Kwa hiyo, tukisema tuendelee kukomaa na kuingia barabarani, itaonekana nia yetu ni kuua watu na kumwaga damu suala ambalo si lengo letu,” alisema.

Katika mkutano huo, Mbowe alionyesha jinsi anavyoshangazwa na kitendo cha majeshi ya ulinzi kutumika kupambana nao huku wakiwa hawaoni umuhimu wa kukaa kwa ajili ya mazungumzo.

“Wamekuwa wakihubiri amani, lakini matendo yao hayaendani na amani wanayoihubiri kwa sababu hawaoni umuhimu wa kukutana na sisi,” alisema.

UKAWA KURUDI BUNGENI

Wakati huo huo, Mbowe alisema katika mazungumzo yao na washauri hao, waliwaomba wawaruhusu wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), warudi bungeni kwa kuwa mchango wao unahitajika.

“Kwa hiyo, Septemba 4 na 5 wabunge wote wa Ukawa watakutana Dodoma kujadili ushauri huo wa viongozi wa dini na namna ya kurudi bungeni

“Wenzetu CUF walikuwa na mkutano mkuu, hivyo tutakutana nao Dodoma katika siku hizo kwa ajili ya mazungumzo ya namna ya kurudi bungeni,”alisema Mbowe.

Mei mwaka huu, wabunge wa Ukawa walisusa kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti wakipinga kile walichokiita   kuburuzwa na Naibu Spika, Dk.Tulia Ackson.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu mpango wa chama hicho kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya zuio la mikutano ya siasa, Mbowe alisema timu ya wanasheria wa Chadema wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu wamekwisha kupeleka mashauri 15 mahakamani yakihusu jinsi demokrasia inavyokiukwa.

Mbowe pia alisema baada ya kutangaza maandamano ya Ukuta mwezi mmoja uliopita, viongozi wao 28 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali na zaidi ya wanachama 230 wamefunguliwa mashtaka  yanayohusu uchochezi.

LOWASSA ATOBOA SIRI

Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kile walichozungumza na Rais Magufuli walipokutana mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kanisa la Mtakatifu Petro  Dar es Salaam, Lowassa alisema hawakuzungumza suala la msingi zaidi ya salamu na kuahidiana kuwasiliana.

Jumamosi iliyopita akiwa katika ibada ya Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Lowassa alishikana mkono na Rais Magufuli kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Hatukuongea jambo lolote la msingi zaidi ya salamu na tukaahidiana kuwasiliana hivyo nasubiri mawasiliano ya Rais Magufuli.

“Lakini pia, mitandao ya jamii inaandika mambo mengi sana ambayo ni just accusations (shutuma tu), ningekuwa na muda ningefafanua hili.

“Kuhusu lile tukio la mimi kupeana mkono na Rais Magufuli, hakuna mkristo yeyote anayeweza kukataa kumpa mkono mwenzake mbele ya viongozi wakuu wa dini.

“Ni nani ambaye ni mkristo angeweza kukataa kupeana mkono wa amani kanisani, tena mbele ya kardinali na maaskofu wanane?

“Sikuwa na nguvu ya kuukataa mkono ule,”alisema Lowassa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles