27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Jukwaa la Wahariri lapinga kufungiwa redio

Nevile-Meena--620x308Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa tamko na kusema kuwa limeshtushwa na kusononeshwa kutokana na  hatua ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuvifungia kwa muda usiojulikana vituo viwili vya redio.

Vituo vilivyofungiwa ni Radio 5 ya Arusha na Magic FM ya Dar es Salaam, uamuzi ambao ulitangazwa juzi.

Tamko hilo la TEF lilitolewa jana Dar es Salaam na Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena.

Alisema kwa muda wa miezi takriban kumi tangu alipoteuliwa kuwa waziri, Nape amejitokeza mara nne na kutangaza kufuta na kufungia vyombo vya habari.

“Alianza kulifuta Gazeti la Mawio, baadaye alitangaza kufuta mamia ya magazeti na majarida ambayo hayajachapishwa kwa muda mrefu, ikafuata adhabu ya kulifungia kwa miaka mitatu Gazeti la Mseto na sasa vituo viwili vya redio.

“Katika tukio la kufutwa kwa Mawio, tulihoji ukubwa wa kosa la gazeti hilo kiasi cha kufutwa. Leo hii tunahoji tena ukubwa wa makosa na pengine historia ya redio husika siku zilizopita. Ndiyo maana tunasema hili la sasa ni mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa habari.

“TEF inachukulia hatua hii kama mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini na tunashindwa kuelewa dhamira ya Serikali ya awamu ya tano kwa sekta ya habari nchini. Kinachoonekana ni kutumia kila aina ya sheria iliyopo kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Kimsingi TEF hatuoni nia (spirit) ya malezi katika uamuzi wa waziri huyo,” alisema Meena.

Kutokana na hali hiyo, alisema msimamo wa TEF, unasikitishwa na utaratibu uliotumiwa na waziri kufikia uamuzi huo, umekuwa wa makosa yaleyale ya siku zote.

“Pamoja na kwamba vyombo vya habari hufanya makosa, lakini hata pale makosa yanapotokea taratibu za kuyashughulikia lazima zizingatie misingi ya utawala bora, haki na demokrasia.

“Mfumo wa kushughulikia matatizo au kasoro za kitaaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi kwani unamfanya waziri kuwa na mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata kama mtizamo huo unakinzana na misingi ya taaluma,” alisema.

Meena alisema kuwa uamuzi wa Waziri Nape unaonekana hauna nia njema ndani yake kwani kifungu cha 28 cha sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) alichotumia kutoa adhabu hiyo, hakimlazimishi kufungia vituo vya redio kama alivyofanya.

“Kosa la vituo hivyo kwa mujibu wa waziri ni uchochezi, lakini hakuweka bayana maudhui ya vipindi au habari ambazo zilivifanya vituo hivyo ‘kutiwa hatiani’ na baadaye kufungwa kwake kwa muda usiojulikana. Kwa sababu hiyo si rahisi kwa  waandishi wengine wa habari kujifunza kwa makosa ya wenzao kwa kuwa mchakato uliotumika kushughulikia suala hilo umebaki kuwa siri ya waziri.

“Tunapinga uamuzi wa Serikali kuvifungia vituo hivyo bila sababu na tunatoa mwito kwa Waziri Nape kutafakari upya suala hili na kuachana kabisa na dhamira hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu,” alisema Meena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles