28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU ZA MASTAA KUGEUZA USIKU KUWA MCHANA

Hemed-PHD

Na KYALAA SEHEYE,

STAILI ya maisha ya mastaa wengi ulimwenguni inafanana lakini zaidi ni ile tabia yao ya kubadilisha usiku kuwa mchana kwa sababu mbalimbali, Juma3tata linakuondolea utata.

Siyo jambo la ajabu kwa mastaa kufanya kazi zao mpaka usiku mwingi kisha alfajiri kulala hadi mchana wa jua kali, muda ambao watu wengine huwa makazini wakitafuta riziki zao.

Ukiacha wanaofanya kazi nyakati za usiku, wapo wengine wanaokuwa kwenye majumba ya starehe, wakila bata usiku mzima, kisha kutumia mchana kupumzika.

Juma3tata lina ripoti iliyoshiba baada ya kuzungumza na mastaa wa fani mbalimbali Bongo na kueleza sababu za wao kubadili usiku kuwa mchana.

SHOO / BATA

Hemed Suleiman (filamu/muziki)

Kutokana na namna kazi ya muziki ilivyo, wasanii wa muziki hulazimika kukesha usiku kucha wakipiga shoo katika kumbi mbalimbali na kurudi majumbani alfajiri na hivyo kupumzika mchana.

Hilo linawekwa sawa na msanii wa filamu ambaye pia ni mwanamuziki, Hemed Suleiman ‘PhD’ aliyesema kwamba, muda wake wa kulala huwa kati ya 10 – 11 alfajiri.

“Kazi inasababisha iwe hivyo. Kuna wakati labda nina scene za kucheza usiku, kama ni nyingi basi nalazimika kulala mchana mzima ili usiku niweze kwenda kufanya kazi nzuri.

“Usisahau kuwa mimi pia ni mwanamuziki, wakati mwingine huwa natakiwa kwenye shoo, kama unavyojua tena shoo nyingi ni za usiku kuliko mchana. Hiyo ndiyo husababisha nishindwe kufuata utaratibu wa kawaida wa maisha ya binadamu unavyopaswa,” anasema Hemed.

Rubby (mwanamuziki)

Kwa upande wake Hellen George ‘Rubby’ amesema mastaa wengi hufanya shughuli zao usiku, huku wakati mwingine wakikutana kwenye kumbi za burudani.

“Kazi nyingi huwa tunafanya usiku, kama sina kazi basi nitakwenda kwenye kumbi za burudani. Unajua huko kunakupa msanii mwanga katika kazi zako. Ukitazama shoo ya mwenzako, lazima kuna vitu utajifunza.

“Mimi huwa nalala kati ya saa sita au saba kama sina mtoko, muda ambao huwa nautumia kuandika mashairi yangu, lakini kama nimetoka huwa nalala kati ya saa 10 – 11 alfajiri. Muda wa kuamka sina, nitatoka kitandani pale nitakapoona mwili wangu umepumzika vya kutosha,” anasema Rubby.

UTULIVU

Snura Mushi (filamu/muziki)

Sababu nyingine inayowafanya mastaa kubadilisha usiku kuwa mchana, inaelezwa kuwa ni kutafuta utulivu wa akili wakati wa kutunga kazi zao.

Hoja hii inaungwa mkono na msanii wa filamu na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Snura Mushi ambaye anasema: “Huwa natunga nyimbo zangu usiku. Ni muda ambao umetulia na kichwa kinaweza kufanya kazi na kufikiri vizuri. Usiku ni mzuri kwa kutunga maana hata vurugu za watoto nyumbani zinakuwa zimeshapungua kabisa.”

Snura anasema mara nyingi muda wa kulala huwa kati ya saa 9 – 11 alfajiri kulingana na namna atakavyokuwa amechoka, huku akiamka kati ya saa 6 – 7 mchana.

Hussein Tuwa (mtunzi wa riwaya)

Mtunzi mahiri wa riwaya nchini, Hussein Tuwa naye alipohojiwa na Juma3tata kuhusiana na ishu hiyo alikiri, akieleza sababu ni kutafuta utulivu wa kuumba maneno kwa utulivu.

“Riwaya ndiyo mama wa sanaa zote unazoziona. Kwa mfano filamu au muziki. Msanii wa filamu hawezi kuingia location kama hana mswada ambao utakuwa umeandikwa na mwandishi. Kadhalika hata msanii wa muziki, hawezi kuingia studio kurekodi kama hana mashairi.

“Kutokana na hayo dada yangu (mwandishi), lazima kichwa kitulie sana wakati wa kuandika riwaya. Mara nyingi huwa napenda kutulia usiku nikitunga kazi yangu. Lakini hata kama sitakuwa na kazi ya kuandika, kama mwanafasihi lazima nisome vitabu vingi na kutazama filamu mbalimbali ili kukuza ufahamu wangu.

“Nakumbuka wakati naandika kitabu changu cha Mkimbizi, asimilia 70 ya muda nilioandika ilikuwa usiku. Utulivu wa usiku ndiyo unaowafanya watunzi wengi wapende kutulia usiku na kupumzika mchana,” anasema Tuwa ambaye ni Rais wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya Wenye Dira Tanzania (Uwaridi).

Tuwa anaongeza: “Nashukuru kwamba kwa utulivu ninaoupata usiku, basi huwa naandika kazi nzuri ambazo zimeniongezea mashabiki wengi ndani na nje ya nchi, maana huwa naandika pia vitabu kwa lugha ya Kiingereza.

“Kwa kawaida huwa nalala kati ya saa 6 – 7 usiku kama sina kazi ya kuandika, lakini kama siku hiyo naandika naweza nikalala hata saa 11 alfajiri.”

Yusuph Mlela (msanii wa filamu)

Staa wa filamu za Kibongo, Yusuph Mlela anasema yeye huamua kulala mchana na kufanya kazi zake usiku kwa sababu ya kutafuta utulivu kama walivyotangulia kueleza Snura na Tuwa.

“Kwa kawaida huwa nalala saa 11 alfajiri na kama ikitokea nikawahi sana basi ni saa 9, kuamka ni kati ya saa 8 – 9 mchana ili kujiepusha na uzee wa wa usinginzi. Napenda kufanya shughuli zangu usiku, mchana inabidi tuwaachie watu walioajiriwa, usiku ni muda wa sisi tuliojiajiri,” anasema Mlela na kuongeza:

“Lakini pia kuna wakati mtu unataka kwenda kula bata, huwezi kufanya kazi muda wote, kama staa lazima upate muda wa kutoka ili kupanua mawazo na kukutana na watu tofauti.”

IRENE UWOYA (msanii wa filamu)

Uwoya anasema yeye huchelewa kulala kwa sababu ya mizunguko yake (mitoko) au kazi zake za kisanii zinazofanyika usiku wakati mwingine.

“Sina ratiba maalum, lakini kwa kawaida huwa nalala kati ya saa 10 – 11 alfajiri na kuamka kati ya saa 7 – 9 mchana. Sasa itategemea kama labda nilikuwa location kwa ajili ya kurekodi filamu au nimetoka na mambo mengine lakini usiku ni muda wangu wa kufanya mambo yangu na mchana ni muda wa kulala,” anasema Uwoya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles