24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Lema aendelea kugoma kula akiwa mahabusu

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)

Na JANETH MUSHI, ARUSHA

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ameendelea kugoma kula kwa siku ya tatu mfululizo tangu alipokamatwa Oktoba 26 mwaka huu, nyumbani kwake mjini hapa, akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Lema alikamatwa siku hiyo saa 12 alfajiri akiwa nyumbani kwake, Njiro,  na hadi sasa anashikiliwa katika mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Arusha.

Kutokana na kuendelea kugoma kula, Wakili wake, John Mallya amesema leo saa sita mchana atakwenda Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kufungua kesi ya kutaka mteja wake afikishwe mahakamani.

Akizungumza na MTANZANIA kwa   jana, Wakili Malya alisema katika kesi hiyo atashirikiana na Chadema kuwashtaki mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, Mkoa wa Arusha.

Tangu mbunge huyo akamatwe amegoma kula kwa  kile anachodai kupinga udhalilishwaji aliofanyiwa na polisi wakati wa kukamatwa.

Pia, Lema anasema alinyanyaswa mbele ya watoto wake nyumbani kwake huku wakijua yeye ni kiongozi na amechaguliwa na wananchi.

Neema, mkewe Lema, alizungumza na MTANZANIA jana na kuthibitisha kwamba  mumewe amegoma kula.

“Anaendelea kugoma kula mpaka sasa kwa sababu  hata sasa nimetoka polisi asubuhi kumpelekea chakula, lakini amekataa kula.

“Lakini nilipouliza pale polisi kuwa wanampeleka lini mahakamani, nilijibiwa wanaendelea kumhoji,”alisema Neema.

Juzi, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa alihojiwa dhidi ya matamshi ya uchochezi na kuwa atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika   uchunguzi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, Lema anatuhumiwa kuwachochea wakazi wa Arusha kuandamana Septemba mosi, mwaka huu kuhamasisha kile kinachoitwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

Jana, Kamanda Mkumbo alipotafutwa kwa simu   kujua ni lini mbunge huyo atafikishwa mahakamani, simu yake iliita bila kupokewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles