31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mapenzi ni zaidi ya I love you… I love you too

THAMANI ya pendo la kweli halipo katika kinywa pekee, matendo yakizungumza ndiyo hudhihirisha kile kilichopo moyoni. Yapo mambo ya kujifunza ili kuweza kuwa na uhusiano bora.

Ndiyo mada tunayoijadili hapa ambayo nilianza nayo wiki iliyopita. Ni muhimu kutambua na kuthamini penzi la kweli la mwenzi wako. Ukilijua hilo, maana yake utaijua nafasi yako kwa mwenzako na kuisimamia vema.

Usipojitambua hutaona thamani ya mapenzi, hutaona umuhimu wako kwenye ndoa. Muunganiko wenu hautakuwa wa maana kama hutatambua thamani yako.

Lazima mwanamke asimame katika nafasi yake na mwanaume  asimamie nafasi yake. Kuna baadhi ya watu wakishaingia kwenye ndoa wanaona kila kitu kimeshaisha. Hawaoni umuhimu wa kufikiria kuwa bora zaidi kwenye ndoa.

Ndugu zangu, nyumba hujengwa tena hujengwa kwa umakini wa hali ya juu. Huwezi kumuona mwenzako mpya kama wewe  hujaonyesha upya katika mambo yako. Mvute mwenzi wako ili akuone kweli unahitaji kuwa mpya, hapo utatengeneza nafasi kwake ya kubadilika kwenye nyendo zake.

 

TAFUTA FURAHA YA MWENZAKO

Kati ya mambo yanayoharibu ndoa ni pamoja na kugombana mara kwa mara. Kuna wengine huwa hawawezi kuzungumza sana, kama umemkosea, ataishia kukuambia mara mbili au tatu, baada ya hapo anaamini umeelewa.

Ikitokea ukajua umekosea na mwenzi wako amekujulisha au ukamuona hana furaha, ni jukumu lako kuhakikisha furaha yake inarejea tena. Mpeleleze, jichunguze, ni wapi umekosea? Haraka sana unachukua hatua ya kurekebisha makosa yako. Usiruhusu mwenzako kuwa amenuna muda wote kwa sababu yako. Tafuta amani yake.

 

KUWA MWEPESI KUOMBA MSAMAHA

Hakuna kitu kinachoumiza kama mmoja anapokosea na akajua mwenzake anajua kuwa amekosea halafu aache kulipa uzito tatizo hilo. Binadamu tumeumbwa na maumivu moyoni. Ikiwa mwenzako amekukosea na akabaki kimya, maumivu yake huwa mara mbili.

Mwingine anaweza kufikia hatua ya kuzungumza na mwenzake kuhusu tatizo husika akitarajia mwenzi wake atamsikiliza na pengine kukaa chini na kujadiliana pamoja lakini inakuwa kinyume chake.

 

MSISIMKO WA MAHABA

Rafiki zangu, usishangazwe na tatizo la msisimko wa mahaba. Ni kutokana na makosa ambayo unayafanya kwenye uhusiano wako. Wakati mwingine, unaweza kuwa chanzo au mwenzi wako akasababisha hilo kutokea.

Hali hiyo ikitokea, kamwe usiwaze kuhusu kuachana. Achana na fikra za talaka, si kwamba umemchukia mwenzi wako, si kweli kuwa mapenzi ndiyo yanakuwa yameisha. Mapenzi yapo moyoni, hivyo kamwe usiwaze kuachana kunapotokea matatizo ya namna hiyo kwenye uhusiano.

 

NINI CHA KUFANYA?

Jambo la kwanza kabisa kuliingiza ubongoni mwako ni ufahamu kuwa tayari kuna tatizo katika ndoa yenu. Tatizo ambalo linahitaji utatuzi wa haraka.

Katika utatuzi wenyewe, kunawahitaji wote lakini ikitegemea zaidi upande wako kwa sababu tayari umeshagundua kuna tatizo.

  • Chunguza tatizo

Lazima ujichunguze, angalia nyumba yako kwa makini. Mchunguze mwenzi wako, kisha ujue ni wapi kwenye makosa. Kujua chanzo ni mwanzo wa kuelekea kwenye kutafuta ufumbuzi.

 

  • Badilika

Inawezekana wewe ndiye uliyekosea, yamkini pia ni mwenzi wako ndiye mwenye makosa, vyovyote ilivyo, kikubwa cha kuzingatia hapo ni kwamba, tayari mpo kwenye matatizo ambayo wewe umeshayagundua na upo tayari kuyasahihisha.

Badilika kifikra. Kama ulikuwa una majibu mabaya kwake, anza kumjibu vizuri. Hata kama yeye ndiye mwenye makosa, haijalishi maana hapa sasa unatafuta amani ya nyumba yenu. Mtazame kwa picha tofauti, ondoa fikra za upungufu wa msisimko kwake.’

Matayarisho ya akili yatakusaidia wakati ukielekea kwenye kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo lako/lenu.

Usikose sehemu ya mwisho ya mada hii wiki ijayo.

Jiandae kusoma kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitaingia mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles