27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

FBI inaposalimu amri kwa mtekaji aliyewachezea shere

katika mkutano na wanahabari baada ya kuachiwa mateka.
katika mkutano na wanahabari baada ya kuachiwa mateka.

NA JOSEPH HIZA,

MWEZI uliopita, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilitangaza kuufunga rasmi uchunguzi wake uliodumu kwa miaka 44 kuhusu tukio la mtekaji nyara aliyetoweka kusikojulikana baada ya kuruka kwenye ndege akiwa na dola za Marekani 200,000.

Jina lake halisi halijulikani lakini mara ya mwisho wakati akinunua tiketi ya ndege aliyoiteka Novemba 24, 1971, alijitambulisha kama Dan Cooper.

Anaelezwa na aliowashikilia mateka, ambao wengi wameeleza kufurahishwa na kuhitimisha kwa kesi hiyo kama mtu mtulivu, mwenye mwonekano wa umri wa miaka 40, aliyevaa suti ya kibiashara, tai nyeusi na shati jeupe.

Hadi sasa anakumbukwa huko Ariel, Washington kupitia ‘Siku ya Cooper’ tukio linalofanyika kila mwaka wakati wa wikiendi ya baada ya ile ya Utoaji Shukrani.

Aidha, kwingineko promosheni yenye jina la Cooper hufanyika katika migahawa. Na ametungiwa au kuhusishwa na filamu na vipindi kama vile Prison Break, NewsRadio, na umb3rs, pamoja na kitabu kiitwacho The Vesuvius Prophecy.

Kwanini mhalifu apate heshima na sifa zote hizo? Mtu asiyejulikana, kutoka kusikojulikana na aliyetoweka kusikojulikana?

Hii ndiyo dunia ya Kimagharibi, ambako wahalifu huweza kuenziwa na kuabudiwa wanapoonesha umahiri fulani, ambao hauwezi kufanywa na binadamu wa kawaida na ambao kwa kawaida huonekana tu ndani ya filamu za kufikirika!

Kwa sababu hiyo, kwa Cooper kama anavyojulikana, ameenziwa kutokana na kutengeneza simulizi ya kweli na ya kusisimua akiwa peke yake bila msaada wa yeyote, akizichezea shere mamlaka kama FBI.

Simulizi inaanzia aliponunua tiketi ya dola 20, kisha kupanda ndega chapa 305 ya Shirika la Ndege la Northwest Orient huko Portland, Oregon.

Akiwa ndani aliagiza pombe kali aina ya bourbon na soda, kisha kuanza kuvuta sigara. Pengine ni moja ya sababu zilizompatia utulivu, akili na ujasiri kwa kazi ya siri yake aliyoikusudia siku hiyo.

Alikaa kiti cha nyuma kabisa mwa ndege akiwa karibu na ya mhudumu wa kike; Florence Schaffner.

Dakika chache baadaye wakiwa angani, Cooper alitoa kikaratasi mfukoni kilichochapwa na kukipitisha kwa Schaffner, ambaye alidhani kina namba za simu za ‘mfanyabiashara’ huyo, alikiweka mkobani bila kukifungua. Lakini Cooper alimnong’oneza , “Bibie, ni vyema ukisome. Nina bomu.

Ili kumhakikisha uwapo wa bomu, alimfungulia briefcase aione, kabla ya kumpa maagizo akaongee na marubani kuwa wawasiliane na Uwanja wa Ndege wa Seattle kuufahamisha kutekwa na mtu mwenye bomu.

Na kwamba mtu huyo atailipua ndege hiyo, ikiwa na abiria wote 36 na wafanyakazi sita, iwapo hatapatiwa dola 200,000, miavuli minne pamoja na kujaziwa mafuta itakapofika Seattle ili impeleke sehemu atakayoitaka.

Schaffner alifanya kama alivyoagizwa na madai ya Cooper yakawasilishwa na marubani uwanja wa ndege wa Seattle, ambao uliwasiliana na vyombo vya ulinzi ikiwamo FBI.

Mamlaka hizo zikiongozwa na FBI zikakubaliana kuokoa maisha ya waliokuwamo pamoja na ndege hiyo kwa kumpatia mtekaji mahitaji yake huku vikifanya mpango wa kumkamata.

Muda wote huu abiria wengine walikuwa hawajui kinachoendelea na ili kuepusha wasiwasi kutokana na kuchelewa kutua wakati madai ya Cooper yakishughulikiwa ardhini, wakatangaziwa kulikuwa na tatizo la kiufundi hivyo itawalazimu wachelewe mpaka litakapo shughulikiwa.

Hatimaye FBI walifanikiwa kukusanya noti 10,000 za dola 20, zote zikiwa jumla ya dola 200,000 kutoka benki za karibu na kuzichukua picha na walipata miavuli minne kutoka Jeshi la Anga karibu na uwanja huo wa ndege kabla ya kuwasiliana na ndege juu ya utayari wa vitu hivyo.

Baada ya kupewa orodha ya vitu hivyo, Cooper, akatoa amri apatiwe miavuli ya kawaida, akisema hataki ya kijeshi, kitu ambacho kiliwalazimu DBI wakazitafuta chapchap na walizipata kutoka kituo cha kujifunzia urukaji kwa miavuli.

Robo saa baadaye, ikiwa ni saa 11. 39 ndege ilitua Seattle na Cooper akamuamuru isimame sehemu pweke lakini yenye mwanga wa kutosha. Pia akamuamuru taa zote za ndani kuzimwa ili kutotoa nafasi kwa wadunguaji.

Baada ya Cooper kuhakikisha mahitaji yake yametimizwa aliwaruhusu abiria wote washuke pamoja na wahudumu wawili akiwamo Schaffner, akibaki na marubani wote wawili na wahudumu wanne akiwamo fundi, kabla ya kuamuru ndege ijazwe mafuta.

Baada ya kila kitu kuwa tayari Cooper aliwapa maagizo marubani kuhusu anakotaka apelekwe na namna ya kusafiri, ikiwamo kasi ya kilomita 190 kwa saa na kuruka umbali wa futi 10,000 kutoka ardhini.

Pia aliwaeleza kuwa anataka waondoe mgandamizo ndani ya ndege, matairi yabaki kama inatua na mlango wa nyuma ubakie wazi na mabawa ya ndege ya pembeni yawekwe kwenye nyuzi 15.

Baada ya majadiliano wamiliki wa ndege hiyo, Northwest Orient walikataa suala la ndege kubaki mlango wa nyuma, wakisema ni hatari kiusalama. Cooper huku akijiamini aliwaeleza ni salama, lakini hakutaka kubishana nao. Alijua cha kufanya, kwani ndege iliporuka tu alifungua mlango huo.

Wakati ndege ikiwa angani, watu watatu yaani fundi na marubani wawili walikuwa mbele kabisa kwenye chumba cha marubani huku Cooper pekee, akiwa na mhudumu mmoja sehemu ya abiria.

Mara tu baada ya ndege kuruka, ndege mbili za kivita aina ya F-106 nazo ziliruka kuifuatilia ndege hiyo, kwa namna ambayo zisingeonekana na Cooper au mtu yeyote aliyeko ndani ya ndege, moja ikiwa juu na nyingine chini ya ile ya akina Cooper.

Baada ya muda Cooper alimuamuru mhudumu akaungane na wenzake chumba cha marubani na akamfungia akibaki peke yake katika sehemu ya kukaa abiria.

Takribani saa mbili kamili usiku king’ora kililia kwenye chumba cha marubani kuashiria kuwa mlango wa nyuma kwenye mkia wa ndege umefunguliwa.

Dakika chache baadae sehemu ya nyuma ya ndege ilitikisika kwa nguvu na kuwa kama inainuliwa juu na marubaini wakabaini hilo na ili kuepusha ndege isidondoke marubani iliwalazimu waishushe ndege chini na kutua kwenye uwanja wa ndege wa Reno, Nevada takribani majira ya saa nne na robo usiku.

Baada ya ndege kutua tu maofisa wa FBI na polisi waliizunguka na kuingia ndani kufanya upekuzi na ndani ya dakika chache wakagundua D.B Cooper hakuwepo ndani ya ndege, alishahuka kusikojulikana, kitu ambacho kiliwakanganya na ikabidi warudi na kuigiza walikopitia ili wachunguze aliposhukia kwa kufuata muda uliotumika. Mahali walipabaini lakini Cooper hawakumuona.

Na huo ndio ukawa mwanzo wa msako mrefu uliowafikisha hadi mwezi uliopita ukitimiza miaka 44, miezi saba na siku tangu tukio hilo kwa FBI kutangaza kufunga faili la Cooper. Au kwa lugha zao FBI walisema nguvu na rasilimali inazoshughulikia kesi ya D.B. Cooper zimaelekezwa katika chunguzi nyingine.

Baada ya ile ya kijeshi kukataliwa, FBI ilimpatia minne ya kiraia miwili ikiwa ya kufundishia darasani tu na mingine miwili ilikuwa ya kufanyia mazoezi ya kuruka. Kwa mustaajabu wa FBI, ilibainika Cooper alitumia ile isiyoweza kuruka na kujumuisha eneo aliloangukia, umbali huku usiku huo ukiwa na ngurumo na radi, inaamini hakunusurika.

Aidha katika moja ya chunguzi zao, walizobaini ikiwamo kuchezewa shere juu ya idadi ya miavuli ambayo iliwaaminisha FBI kwamba Cooper alipanga kuruka na wahudumu watatu kumbe sivyo na hivyo kupotezwa maboya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles