23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein atangaza elimu bure Zanzibar

Dk.-Ali-Mohamed-SheinELIAS MSUYA NA IS-HAK OMARI, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametangaza rasmi kufuta michango yote katika elimu ya msingi kuanzia Julai mwaka huu.
Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itabeba gharama zote ikiwa kama mkakati wa kuinua elimu.
Hayo aliyasema jana wakati akihutubia mamia ya wananchi katika sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa njia bora za kuinua kiwango cha elimu ya Zanzibar, ambapo aliwataka wazazi na walezi kujiandaa kwa kuliendeleza hilo ikiwa ni sehemu ya matunda ya mapinduzi ya mwaka 1964.
“Kuanzia mwaka huu elimu ya msingi itakuwa bure, wazee na wazazi nao watatibiwa bure. Serikali ndiyo itakayolipa gharama hizo. Kuhusu elimu ya sekondari na mambo mengine tutayatolea maelezo wakati mwingine.
“Mzee Abeid Amani Karume alikuwa ni kiongozi aliyesimamia sekta ya elimu kwa ufanisi mkubwa mara baada ya kufanyika mapinduzi kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata elimu, kwani fursa hiyo waliikosa kwa kipindi cha miaka mingi waliyotawaliwa na wakoloni,” alisema Dk. Shein.
Alisema Serikali yake katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio makubwa, huku akitoa takwimu za mafanikio ya Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (Mkuza II) na Dira ya Maendeleo 2020.
Dk. Shein aliingia madarakani mwaka 2010 baada ya Wazanzibari kupiga kura ya maoni ya kupitishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokihusisha Chama cha Wananchi (CUF) ambapo Katibu wake mkuu, Seif Sharif Hamad amekuwa makamu wa kwanza wa rais.
Akizungumzia kukua kwa uchumi wa Zanzibar, Dk. Shein alisema pato la taifa hilo limekuwa kutoka Sh bilioni 942 mwaka 2010 hadi kufikia Sh bilioni 1,442 kwa mwaka 2013 sawa na ongezeko la asilimia 53.
“Uchumi wetu umekua kutoka asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2013. Kwa mwaka 2014 mfumuko wa bei ulibaki katika wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 6.1 mwaka 2010,” alisema Dk. Shein.
Aliongeza kuwa uchumi wa Zanzibar unatarajia kukua kwa wastani wa asilimia 7.8 na pato la taifa litaongezeka hadi kufikia Sh bilioni 1,555.1.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Dk. Shein alisema Serikali yake imekusanya mapato ya Sh bilioni 997 kwa kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi 2013/2014 ikilinganishwa na Sh bilioni 484 zilizokusanywa kati ya mwaka 2006/2007 hadi 2009/2010 ikiwa ni ongezeko la asilimia 106.
Kuhusu zao la karafuu, alisema kwa miaka mitatu jumla ya tani 11,477 zenye thamani ya dola za Marekani 130.82 (Sh bilioni 222.7) ziliuzwa ikiwa ni ongezeko la tani 2,792 sawa na asilimia 32.1.
Akizungumzia uwekezaji kwa miaka hiyo minne, alisema jumla ya miradi 141 imeidhinishwa chini ya Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).
Alisema miradi hiyo itakapokamilika itaingiza mtaji wa dola za Marekani 1,469 na kutoa ajira 5,969.
Kuhusu utalii, Dk. Shein alisema idadi yao imeongezeka kutoka watalii 132,836 mwaka 2010 hadi 274,619 mwaka 2014 ikiwa ni ongezeko la asilimia 107.
“Hivi sasa inaandaliwa sera ya urithi wa utamaduni itakayotoa mwongozo wa matumizi bora ya maeneo ya urithi ili kuimarisha shughuli za utalii,” alisema Dk. Shein.
Alitaja pia mafanikio katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, kilimo na uvuvi.

MAPOKEZI YA RAIS KIKWETE
Miongozi mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete ambaye aliingia uwanjani hapo saa nne kamili na kupokewa kwa shangwe kubwa.
Msafara wa Rais Kikwete ulizunguka uwanjani hapo na baada ya kufika karibu na jukwaa kuu, alishuka na kusimama kwenye jukwaa dogo ambapo aliimbiwa wimbo wa Taifa na kupewa heshima na gwaride lililoandaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama.
Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, aliingia uwanjani saa 4:15 akiwa kwenye gari la wazi la kijeshi akiongozwa na msafara wa pikipiki sita.
Baada ya kuzunguka uwanja na kuwasalimia wananchi, Dk. Shein alikagua gwaride na kupanda jukwaa kuu.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinga, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda na Jaji Mkuu Othman Chande.
Wengine ni marais wastaafu wa awamu ya pili na ya tatu, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi na mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na maofisa mbalimbali wa Serikali.
Sherehe hizo zilitawaliwa na gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Kikosi Maalumu cha Kupambana na Magendo (KMKM), Zimamoto na Valantia.
Vilevile kulikuwa na ngoma za asili ya visiwa vya Zanzibar na Bara na watoto waliopambwa kwa rangi za bendera ya Tanzania na ya Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles