30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa atabiri siasa ngumu

Edward Lowassa
Edward Lowassa

PENDO FUNDISHA NA ELIUD NGONDO, MBEYA

WAZIRI Mkuu mstaafu na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewataka wafuasi wa chama hicho kuwa na ujasiri pindi wanapokuwa wakipigania haki zao.

Amesema kwamba, Chadema imetoka mahali pagumu kisiasa na sasa inaelekea pagumu zaidi na kwamba kinachotakiwa ni kwa wanachama kutokuwa waoga ili waweze kufanikiwa.

Lowassa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la uongozi la kanda ya nyanda za juu kusini (NYASA).

Pamoja na kuhudhuria kikao hicho, Lowassa anatarajia kuanza ziara ya siku nne katika mikoa yote ya nyanda za juu kusini kuanzia leo.

Katika ziara hiyo itakayohusisha mikoa ya Songwe, Rukwa, Njombe na Iringa, mwanasiasa huyo atakutana na viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge na madiwani.

Katika mazungumzo yake jana, Lowassa alisema wanaChadema wanatakiwa kuondokana na uoga na wasikubali kurudi nyuma katika mapambano ya kutafuta haki, huku viongozi wakijiandaa na chaguzi zinazokuja ukiwamo wa Serikali za mitaa.

“Chama kilipotoka kisiasa ni kugumu, lakini tunapoelekea ni kugumu zaidi. Hivyo basi, ni vema viongozi wakajipanga na kuangalia mikakati thabiti na imara itakayokiweka chama kwenye mstali sahihi na wenye kuleta tija kwa Watanzania,”alisema.

Awali, Lowassa alihudhuria ibada ya Jumapili  katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Forest uliopo mjini hapa.

Akiwa kanisani hapo, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura za ndio wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

“Wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana, makanisa yaliombea sana amani na hii ilitokana na ugumu wa kisiasa uliokuwapo wakati huo.

“Lakini, kwa sasa nchi inaelekea pagumu sana kisiasa na maombi yenu yanahitajika zaidi,”alisema Lowassa kwa kifupi.

Wakati Lowassa akisema hayo, Katibu wa Chama hicho, Nyanda za Juu Kusini, Franky Mwaisumbe, alisema wajumbe hao walikutana ili kujadili masuala mbalimbali ya kisiasa likiwamo suala la mikutano na maandamano ya amani waliyopanga kufanya Septemba mosi nchi nzima.

“Kabla ya oparesheni hii, chama kimeanza na mikutano yetu ya ndani ambayo mgeni rasmi ni mjumbe wa kamati kuu Taifa, Edward Lowassa.

“Lowassa atakapomaliza ziara yake ya siku nne katika kanda yetu, maandalizi yetu ya kuandamana Septemba mosi yataendelea.

“Taarifa nyingi zinatolewa juu ya upotoshwaji wa oparesheni hii ya Septemba mosi, lakini ninawaomba wananchi wasiwe na wasiwasi kwani hata sisi hatupendi kuona damu za watu wasio na hatia zikimwagika,”alisema Mwaisumbe.

“Pamoja na kujadili hilo, pia tulijadili namna ya kuimarisha misingi ya chama kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na kuangalia namna ya kuvunja makundi yaliyomo ndani ya chama.

“Pia tuliangalia namna ya kuongeza idadi ya wanachama watakaokisaidia chama kuwa na nguvu katika utendaji na kujiwekea misingi kuanzia ngazi ya mitaa na katika nafasi za kisiasa,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles